Tabia Nne(4) Zitakazokuwezesha Wewe Kuwa Na Ufanisi Mkubwa Kwenye Kazi Zako.

Tunaishi kwenye dunia ambayo ina kelele nyingi sana. Katika kipindi hiki ambacho tunaishi, kwa siku moja unakutana na taarifa nyingi kuliko taarifa ambazo mtu aliyeishi miaka ya 1800 alikuwa anakutana nazo mwaka mzima, na wakati mwingine kwa kipindi chote cha maisha yake.
Tunaishi kwenye kipindi cha mapinduzi ya taarifa, kwa hivyo tungetegemea taarifa hizi ziwe msaada mkubwa kwetu kupiga hatua kwenye jambo lolote ambalo tunafanya, iwe ni kazi, biashara au hata maisha ya kawaida tu.
Lakini hali halisi sio, taarifa hizi nyingi zimekuwa kikwazo cha sisi kuweza kupiga hatua. Na ni kwa sababu hatujachukua muda wa kuchambua ni taarifa zipi muhimu kwetu na zipi sio muhimu.

KELELE ZOTE HIZI HUWEZI KUFANYA KAZI KWA UFANISI

 
Taarifa tunazokutana nazo ni nyingi sana, na nyingi zinashika hisia zetu, zinakazana kupata muda wetu, vichwa vyenyewe vya taarifa hizi vinavutia sana na hatimaye unajikuta ukisoma au kusikiliza taarifa hiyo. Unamaliza kufuatilia taarifa hiyo, hakuna cha ziada ulichoongeza na umepoteza muda wako.
Kama ingekuwa ni mara moja tu tungesema sio vibaya, lakini sasa ni kila wakati. Unaingia kwenye mtandao wa facebook unakutana na taarifa nyingi, hutaki kupitwa hata na taarifa moja, unaingia kwenye blogu mbalimbali, unapata taarifa. Bado kwenye simu yako ya yenye wasap kuna watu wanakazana kukutumia taarifa, na picha na video. Yaani mpaka unakuja kuimaliza siku una taarifa nyingi ambazo hazina umuhimu wowote kwako, na vibaya zaidi umepoteza muda wako mwingi.
Taarifa ambazo zilipaswa kuwa ukombozi kwetu, zimegeuka na kuwa sumu kwetu, na tatizo sio taarifa hizi, bali matatizo yanaanzia kwetu sisi wenyewe.
Mtu unaamka asubuhi na cha kwanza unachofanya ni nini, unakamata simu na kuanza kuperuzi mitandao, unapata habari mbili tatu za kukusisimua. Unatoka kuelekea eneo lako la kazi, njiani unaendelea kupata taarifa, unafika eneo la kazi na kabla hujaanza kazi unaangalia tena ni nini kinaendelea. Ufuatiliaji huu mzuri wa habari mbalimbali ungekuwa mzuri sana kama zingekuwa ni habari ambazo zinakuongezea maarifa na kukufanya uongeze thamani zaidi, lakini sivyo.
Unafuatilia habari nyingi huku uzalishaji wako kwenye kazi unayofanya ukiwa mdogo sana na hivyo kushindwa kutoa thamani ambayo itakufanya ulipwe zaidi. Unaweza kulalamika sana lakini taarifa hizi unazokazana kufuatilia ndio adui yako namba moja wa wewe kushindwa kuwa na ufanisi mzuri kwenye kazi.
Ufanye nini sasa?
Je umechoshwa na hali hii ya kuwa mtumwa wa taarifa? Je unaona kama huwezi kujizuia kuangalia simu yako kila baada ya dakika chache? Kama ndio karibu sana hapa utajifunza njia ambazo kama utazitumia utaweza kuondokana na tatizo hilo. Kama bado hujawa tayari kubadilika, na unaona unachofanya kipo sawa kwako unaweza kuishia hapa kwa sababu ukiendelea mbele utanichukia bure, kwa sababu nitakueleza ukweli ambao hutaki kuusikia. Ndio najua hutaki kuusikia kwa sababu kwa wakati fulani nilikuwa hapo ulipo wewe na nilikuwa nafikiri unavyofikiri wewe, lakini nilipohitaji kweli mabadiliko nilichukua hatua.
SOMA; Changamoto Mbili Kubwa Utakazokutana Nazo Wakati Wa Mabadiliko.
Leo nitakupa tabia unazohitaji kujijengea ili kuongeza uzalishaji wako katika ulimwengu huu uliojaa kelele nyingi za taarifa. Soma kwa makini nimesema tabia kwa sababu mara nyingi watu tunapenda MBINU, lakini nimejifunza kwamba mbinu huwa hazidumu, mbinu ni za muda mfupi. Sasa tukipeana mbinu hapa ambazo ni za muda mfupi, changamoto hii ya taarifa haiishi leo wala kesho, kwanza kadiri siku zinavyokwenda ndivyo taarifa zinavyoongezeka. Hivyo mbinu hazitakusaidia, unahitaji kujenga tabia.
Mbinu ni rahisi kujenga, lakini ni vigumu kudumu nazo. Tabia ni ngumu kujenga lakini ni rahisi kuishi nazo.
Zifuatazo ni tabia unazotakiwa kuanza kujijengea LEO ili kuongeza uzalishaji wako katika zama hizi za kelele nyingi.
1. Kuwa na orodha ya vitu utakavyofanya kwa siku husika.
Usianze siku yako kama mwendawazimu, kama unaanza siku yako bila ya kuipanga, umeamua kuipoteza siku yako. Kabla ya kulala, andika ni mambo gani utakwenda kufanya siku inayofuata, au unapoamka asubuhi na mapema, panga ni mambo gani unakwenda kufanya siku hiyo.
Kuwa na orodha ya vitu ambavyo utafanya, tena orodha iliyoandikwa, itakufanya uwe makini zaidi katika kutekeleza yale uliyoorodhesha. Na ili kuhakikisha unafuatilia orodha hiyo kwa umakini, mwisho wa siku weka alama ya vema kwa yale uliyofanikiwa kuyafanya na alama ya mkasi kwa yale ambayo hukufanya. Ukifanya hivi kila siku utajikuta unalazimika kufuata orodha yako.
Na orodha hii iandikwe kwenye kitabu chako cha kumbukumbu (notebook au diary).
Narudia tena kama unaianza siku yako unaipangilia hutakuwa na tofauti na mwendawazimu, kwa sababu kama huna cha muhimu cha kufanya utajikuta unapokea chochote ambacho dunia inakurushia kupitia habari nyingi zinazoendelea.
Unashangaa unaamka asubuhi na mapema, siku ya kazi badala ya kushambulia majukumu yako unaanza kushambulia watu kwenye mitandao, huyu kafanya hiki, huyu kakosea kile na mengine mengi ambayo sio muhimu kwako.
2. Usianze siku yako kwa habari.
Ndio, namaanisha hivi asubuhi na mapema usianze siku ya ko kwa kusikiliza au kusoma habari. Kama unapingana na hili acha tu kusoma na nenda kasome habari.
Siku moja nikiwa nafundisha semina niliwaambia watu hili na mtu akanipinga na kusema utawezaje kuanza siku bila ya kujua ni kitu gani kinaendelea. Nikamwambia sawa, umeamka asubuhi na kukimbilia gazeti na habari kubwa ni kwamba kuna mtu kamnyonga mke wake na yeye mwenyewe kajiua, sasa habari kama hii inakusaidia nini kwenye siku yako ya kazi? Sana sana inakufanya uianze siku yako ukiwa unajisikia vibaya na kama utaanza siku hivi huwezi kuwa na uzalishaji mzuri.
SOMA; AMKA Kila Siku Ukiwa Na Hamasa Kubwa Ya Kufikia Mafanikio Makubwa. Zoezi Moja Muhimu Kufanya Kila Siku.
Kama kuna habari muhimu kweli, labda ndio mwisho wa dunia au kuna vita imeingia hapo ulipo, utaijua tu, kwa sababu kila mtu atakuwa anachukua hatua. Lakini hizi habari za kawaida wala zisikupe shida.
Kwa hiyo tunakubaliana kwa hili, hakuna habari asubuhi. Kama unaweza kufanya hivyo siku nzima vizuri sana, kama huwezi pitia habari baada ya kazi zako za msingi.
Tumia muda mwingi kujifunza vitu ambavyo vitakuongezea maarifa na sio vitakavyokusisimua na kukuacha ukiwa unajisikia vibaya.
3. Kaa mbali na simu wakati wa kazi muhimu.
Lakini nitakosa dili kama sitakuwa na simu karibu. Hiko ni kitu kingine ambacho unajidanganya nacho na hivyo kujikuta unasumbuliwa kila mara kwa kuwa na simu yako karibu. Kama unafanya kazi ambayo inahitaji utulivu, ni vyema ukakaa mbali na simu yako, au izime au iweke kimya kabisa. Hii itakupa nafasi nzuri ya kuweka akili yako yote kwenye kazi unayofanya na sio kufikiria meseji iliyoingia nani atakuwa ameituma.
Na uzuri ni muda mfupi tu ambao utahitaji kufanya hivi na ukaongeza ufanisi mkubwa kwenye kazi zako.
Jibu kwa wale ambao wanafikiri kukaa mbali na simu watapoteza dili, sio kweli, hakuna dili utakayopoteza kwa kuwa mbali na simu yako kwa muda mfupi. Kama kuna mtu anakuhitaji kweli atakutafuta tu na pia atakupata.
Kwa mfano mimi sehemu kubwa ya kazi zangu nafanya kwa njia ya simu, hivyo nilikuwa nafikiri inabidi niwe na simu masaa 24. Nilipoanza kutenga muda wa kuwa mbali na simu, nilikuwa nakuta simu nyingi zimepigwa, kila nilipokuwa najaribu kuwapigia watu wale walionikosa, wengi wanakuwa wamesahau hata walikuwa wanataka nini.
Kuna siku mtu alikuwa ananitafuta kwa ajili ya kwenda kufundisha semina, nilikuwa mbali na simu na niliposhika simu nilikuta amepiga simu kama mara tano na akatuma ujumbe, tafadhali nitafute nina jambo la muhimu sana. Na likawa muhimu kweli.
Nataka nikutoe wasiwasi kwamba kuwa mbali na siku hakutakukosesha wewe dili, bali kutakufanya upate dili bora zaidi na wakati huo ukiwa na uzalishaji na ufanisi mkubwa.
Kuwa na orodha, usianze siku kwa habari, kaa mbali na simu, ni vitu vigumu kwako? Tumalizie na kingine muhimu.
4. Fanya kazi kwa vipaumbele na anza na majukumu makubwa na magumu.
Kama una majukumu matano ya kufanya kwa siku, yape kipaumbele, ni lipi muhimu zaidi na kubwa pia, na gumu. Halafu yafanye majukumu hayo kwa vipaumbele hivyo.
Umewahi kujikuta siku inaisha halafu hujui umefanya nini? Unajiona ulikuwa bize lakini mwisho wa siku huoni kitu kikubwa ambacho umekifanya? Basi hiyo inatokana na kukosa vipaumbele kwenye kazi zako.
SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.
Usikimbilie kufanya majukumu ambayo ni rahisi, mara nyingi haya yanakuwa na thamani ndogo, halafu yatachukua muda wako ambao ndio unakuwa na uzalishaji mzuri. Anza na yale majukumu makubwa asubuhi na ukiyamaliza utakuwa umeongeza uzalishaji wako na ufanisi pia.
Kumbuka hizi tumejadili hapa sio mbinu, bali ni tabia. Ni tabia kwa maana kwamba unahitaji kuzifanya kila siku. Inabidi ifike mahali iwe ni sehemu ya maisha yako kwamba ni lazima upange siku yako kabla hata hujaianza, usianze siku kwa habari, kuwa mbali na simu unapohitaji utulivu na pia kufanya mambo muhimu kwanza.
Mambo haya yanapokuwa tabia kwako utakuwa na uzalishaji mkubwa na ufanisi mzuri, halafu utakuwa na mafanikio makubwa sana kwenye kazi au biashara unayofanya.
Kama mambo haya ni magumu kwako kufanya unaruhusiwa kuendelea kufanya kile ambacho umezoea kufanya, lakini wakati unafanya hivyo tafadhali sana usituletee kelele kwamba maisha magumu, kipato kidogo na kelele nyingine nyingi ulizozoea kupiga. Una haki ya kuchagua maisha ambayo ni bora kwako kuishi, usikubali kuendelea na maisha ya kuburuzwa, panga maisha ambayo yatakuletea mafanikio.
Nakutakia kila la kheri katika kuongeza ufanisi wako kwenye kazi na biashara zako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
N;B Kila jumanne na alhamisi huwa natuma makala nzuri sana za kujifunza kwenye email. Kama unapenda kupokea makala hizi bonyeza maandishi haya na uweke email yako.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: