Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Karibu tena jumapili ya leo tuendelee kushirikishana misingi muhimu kwenye falsafa yetu hii mpya ya maisha. Kupitia falsafa hii tunaishi yale maisha ambayo tunayapenda na hivyo kuwa bora kwetu bila ya kujali wengine wanachukuliaje.
Kuna changamoto moja kubwa sana ya maisha ya kila mtu, na leo tutajadili vizuri changamoto hii. Na kama ilivyo kwenye maisha, popote penye changamoto ndio penye fursa kubwa, kwa changamoto yetu hii pia tutaona fursa kubwa ya kuwa na maisha bora sana, kitu ambacho kila mmoja wetu anakipigania.
CHANGAMOTO KUBWA YA MAISHA.
Changamoto kubwa ya maisha yetu ni kwamba tunayo maisha mamoja tu. Yaani tunaishi mara moja tu, na maisha yakiisha ndio basi tena. Hatuwezi kurudi tena duniani kuja kuishi mara ya pili. Ni mara moja na imetoka.
Kwa nini hii ni changamoto? Hii ni changamoto kwa sababu kila siku mpya ya maisha yako ni maisha mapya kwako, huna uzoefu wa maisha hayo. Ulipokuwa mtoto ulikuwa na uzoefu wa utoto, ukakua ukapata uzoefu mwingine, leo kama una miaka 30 na una uzoefu wa miaka 30 na na ukifikia miaka 40 na utatengeneza uzoefu mwingine mpya. Hii ina maana kwamba hakuna siku utasema unajua ufanye nini kwa sababu una uzoefu huo.
Kama tungekuwa tunapata maisha haya mara mbili, yaani unazaliwa unakua, halafu ukifa unarudi tena kuja kuanza upya, ungekuwa na uzoefu mzuri, ungejua kwenye miaka fulani inabidi niepuke kufanya vitu fulani. Hupati nafasi hii ya kurudia tena kule ulikopita, hivyo unapita mara moja tu.
HAKUNA ANAYEJUA ANACHOFANYA.
Mara nyingi huwa tunawaangalia wengine na kuona labda wao maisha yao yako vizuri kuliko ya kwetu. Tunaona kama vile wao wanayajua maisha kuliko sisi tunavyoyajua. Wakati mwingine tunaweza kuwaona wana bahati kubwa sana kwenye maisha, kuwa na kazi/biashara nzuri, kuwa na familia bora na hata kuonekana kuwa na vitu vizuri.
Lakini ukipata nafasi ya kuingia ndani ya maisha ya watu hawa, utaona ni jinsi gani fikra zako juu yao zilivyo na makosa. Ukiangalia maisha yao ya ndani sio kwamba wanajua sana kile wanachofanya, sio kwamba wana uhakika sana na maisha yao na sio kweli kwamba kila kitu kinakwenda sawa kwao.
Na wao wanapitia changamoto kama unazopitia wewe, wanapanga mambo ya kufanya lakini hayawi kama walivyopanga na wana changamoto nyingi kwenye kazi zao, biashara zao na hata maisha yao.
Tofauti ya wao na wewe inaweza kuwa kwamba wao wamechagua kuishi maisha licha ya hivi wanavyokutana navyo, wakati wewe umeamua kuyaweka likizo kutokana na changamoto unazokutana nazo.
Ukweli ni kwamba hakuna mtu anayejua kwa uhakika ni nini anafanya kwenye maisha haya. Tunaweka malengo na mipango mizuri sana lakini hatujui kesho ni nini kinakwenda kutokea. Tunajipanga sana ili maisha yetu yaende kama tunavyotaka lakini mambo mengine yanatokea na kuharibu mipango yetu.
HAKUNA ANAYEJUA KESHO.
Kitu kingine kikubwa sana kinachofanya changamoto hii kuwa kubwa ni kwamba hakuna anayejua nini kitatokea kesho. Pamoja na mipango yetu mizuri, pamoja na malengo tuliyojiwekea, bado hatujui kesho ni kitu gani kitakwenda kutokea. Hivyo tunaweza kuwa na siku bora sana leo na kuona tunajua ni nini tutafanya kesho, lakini kesho likaibuka jambo tofauti kabisa linalotufanya tufanye tofauti na tulivyopanga kufanya.
Tunafanya maamuzi mengi leo, tunachagua vitu vya kufanya leo kwa imani kwamba kesho mambo yatakuwa mazuri. Tunachagua kusoma fani fulani leo, tunachagua kufanya kazi fulani leo, tunachagua kufanya biashara fulani leo, tukiamini kesho mambo yatakuwa mazuri, lakini sio mara zote yanakwenda kama tulivyofikiria yatakwenda.
Ulifikiri fani unayosomea itakupa kazi bora lakini hupati kazi uliyofikiri. Ulifikiri kazi uliyopata itakupa maisha bora na kuifurahia lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda unaona inazidi kuwa mzigo. Ulifikiri biashara uliyoingia kufanya ingekuwa na wateja wengi sana na faida ingekuwa kubwa, lakini umekutana na changamoto kubwa ambayo inapelekea biashara kufa.
Katika hali kama hizi ndio unaweza kujiona wewe tu ndio hujui unachofanya, na wengine wote wanajua kile wanachofanya na maisha yao ni mazuri.
JINSI YA KUTUMIA CHANGAMOTO HII KUWA NA MAISHA BORA.
Je kutokujua unachofanya ndio kukubali kuwa na maisha ya hovyo? Hapana, hili sio lengo letu. Kwa sababu hujui kesho ni nini kitatokea haimaanishi usiweke malengo. Kwa sababu hujui kesho inakujaje haimaanishi uishi hovyo leo. kwa vyovyote vile ni lazima tujue kwamba maisha yataendelea hata kama hatujui kesho imebeba nini na hivyo ni muhimu sana kuendelea kuweka malengo na mipango mizuri ya maisha yako.
Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili kuwa na maisha bora japo hujui kile unachoifanya.
1. Usijilinganishe na wengine.
Hakuna anayejua anachofanya, hivyo hata wale unaojilinganisha nao au unaoshindana nao pia hawajui wanachofanya. Na kikubwa sana unachojilinganisha nacho ni kitu cha nje. Yaani unajilinganisha nje ya mwenzako kwa ndani yako, hii itakuletea majibu mabaya sana na yatakutesa. Huwezi kujua nini kinaendelea ndani ya mtu hata kama utaonaje nje yake. Kujaribu kushindana na mtu ambaye hajui anachofanya, na wewe mwenyewe hujui unachofanya ni kujitumbukiza kwenye shimo.
2. Fanya maamuzi ambayo ni bora kwako na nenda nayo.
Kwa kuwa hujui ni kipi kitakachotokea, basi hakikisha maamuzi yoyote unayofanya ni bora kwako. Hakikisha hata kama mambo yatakwenda tofauti na ulivyotegemea bado utakuwa tayari kuendelea kukomaa. Ukifanya kitu ambacho unaiga au umelazimishwa kufanya, unapokutana na changamoto ni rahisi sana kukata tamaa. Ila unapofanya maamuzi wewe mwenyewe kwamba hiki ndio unachotaka, hata utakapokutana na magumu utaweza kuendelea kwa sababu hiki kimetoka ndani yako.
3. Unapokosea usikate tamaa, rekebisha na songa mbele.
Kuna watu wanapokosea hujiumiza sana, hujilaumu na kujiona hawafai. Lakini hujui unachofanya, umekuwa unajaribu tu vitu mbalimbali. Hivyo unapokosea badala ya kupoteza muda wako kujiumiza na kujilaumu, elewa ni sehemu ya maisha yako, elewa ni sehemu ya kujifunza na songa mbele. Makosa maana yake ni kujifunza vitu ambavyo hukuwa umejifunza awali.
4. Utakosea tena na tena.
Kujifunza na kujiandaa bado hakutaondoa makosa yako yote. Kutumia uzoefu wako wa nyuma na hata wa wengine bado hakutaondoa makosa yako ya mbeleni. Kadiri unavyoianza siku mpya unakutana na changamoto mpya. Kwa maamuzi ambayo utafanya huwezi kupatia yote, kuna mengine mengi ambayo utakosea. Ni lazima ulijue hili, na sio kulijua ili kukubali uzembe, bali unalijua ili kujiweka sawa na hata pia kuwa tayari kupokea matokeo na kusinga mbele.
5. Maisha ndio haya, yaishi kwa ukamilifu.
Kwa kujua kwamba unaishi maisha haya tu, kwa kujua kwamba hujui unachofanya, kwa kujua kwamba wengine pia hawajui wanachofanya, ni vyema ukachagua kuishi maisha yako kwa ukamilifu. Usisogeze maisha yako mbele, kwa kufikiri kwamba utaanza kuishi baada ya kumaliza kitu fulani, nani anakuhakikishia hilo. Usiweke furaha yako kwenye vitu, kwamba ukipata au ukifikia ndio utakuwa na furaha. Maisha unayo leo, yaishi vyema, yaishi kwa ukamilifu, fanya kile unachopenda, fanya kwa ubora, leo hii na kama kesho utapata nafasi nyingine utakuwa bora zaidi ya ulivyo sasa.
Ni rahisi kufikiria kama maisha yangekuwa yamenyooka, ni rahisi kufikiria wengine wanajua wanachofanya ila wewe hujui. Ila ukweli ni kwamba wote hatujui tunachofanya, wote hatujui kesho itakujaje. Lakini hili halituzii kuishi leo kwa ubora na furaha. Kulijua hili kunatuandaa vyema kukabaliana na lolote litakalojitokeza. Kutokujua tunachofanya ni nafasi kubwa sana kwetu kufanya kile tunachopenda kufanya.
Ongeza msingi huu muhimu7 kwenye falsafa yako mpya ya maisha ili uwe na maisha bora na unayoyafurahia.
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,