Hakuna kitu kikubwa na kizuri ambacho ni rahisi kufanya au kupata.

Chochote unachofanya au unachotaka, mwanzoni utakufana na upinzani, tena mkubwa sana.

Upinzani huu utatoka kwa watu, utatoka kwenye mazingira yanayokuzunguka, na pia unaweza kutoka ndani yako mwenyewe.

Utakapoanza kufanya utaona kama vile kila kitu kipo kinyume na wewe. Utaona kama kila kinachotokea ni kwa ajili ya kukuondoa wewe kwenye njia uliyoingia.

Huu ni mtihani wa kwanza na muhimu sana kwenye kile ambacho unakitaka. Kama ulikuwa umetamani tu, hutaweza kuvuka hapa, utaacha mara moja. Lakini kama ulikuwa umeamua kweli ya kwamba hiki ndio unachotaka, na upo tayari kukipata, ije mvua lije jua, mwishowe vikwazo vyote vitaanguka na kukuachia wewe uhuru.

Kama ni watu wanakupinga mwishowe watakubali tu. Kama ni hali ilikuwa ngumu mwishowe inakuwa nzuri. Kuendelea kwako kufanya licha ya kila kitu kuonekana kukupinga, ndio kitu pekee kitakachokuhakikishia kupata kile unachotaka.

Je ni kitu gani ambacho umekuwa unataka kufanya lakini unaona kama dunia nzima inakupinga? Badilika sasa na uache kutamani tu, bali uwe unataka kweli na ujitoke kufanya mpaka ukipate. Kwa sababu mwishowe, mambo yote yatakupisha wewe upate kile ambacho umekuwa unapigania.

SOMA; Njia Ya Uhakika Ya Kuwafanya Watu Wakupe Kile Unachotaka.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba chochote nitakachoanza kufanya nitakutana na changamoto, ambazo zinatuwa zinanipinga kuendelea. Lakini mimi najua hata changamoto hizi ziwe kubwa kiasi gani, mwishowe zitaanguka zote na kuniachia mimi ushindi. Nimejitoa kweli kupata kile ninachotaka, najua hakuna kinachoweza kunizuia.

NENO LA LEO.

If you have a positive attitude and constantly strive to give your best effort, eventually you will overcome your immediate problems and find you are ready for greater challenges.

Pat Riley

Kama una mtizamo chanya na unakazana kuweka juhudi mara zote. Utajikuta unayavuka matatizo unayokutana nayo na kuwa tayari kwa changamoto kubwa zaidi.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.