Mara nyingi huwa tunaruhusu vitu vidogo vidogo sana kuharibu siku zetu. Na sio vitu vile vinaharibu, bali sisi wenyewe tunaharibu siku zetu kutokana na vitu hivyo.

Na vitu hivi vidogo vinatokana na mjumuiko wetu na watu wengine.

Labda umempigia mtu simu hakupokea, na hata baadae hakukupigia tena. Au umemtumia ujumbe na hajakujibu.

Labda umemsalimia mtu hakuitika, au umemuuliza kitu vizuri na akakujibu vibaya sana.

Labda kuna mtu wako wa karibu kafanya sherehe lakini hakukualika, au amekualika lakini hakukupa nafasi nzuri.

Vitu vyote hivi ni rahisi kukuvuruga wewe, kuanza kufikiria ya kwamba wewe umedharaulika na unaonekana huna maana. Unaweza kufikiri hali yoyote ile mbaya uwezavyo, lakini huko ni kujiumiza wewe mwenyewe.

Ukweli ni kwamba hakuna mtu aliyepania kukuumiza wewe, iwe kwa kukudharau au kwa kutokupa kipaumbele.

Kila mtu anapitia changamoto zake, na kwa changamoto hizi anajikuta anasahau baadhi ya mambo. Au anajikuta akitoa maneno ambayo sio mazuri, lakini sio kwa lengo la kuumiza wengine.

Na hata ikatokea kwamba mtu ameamua kukuumiza, basi ujue yeye ameumizwa zaidi kuliko hata anavyokuumiza wewe.

Hivyo wakati wowote ambapo mambo haya madogo madogo yanajitokeza, usikubali yakuvuruge, elewa kwamba watu wana nia njema sema hali wanazopitia zinawapa changamoto.

Ukielewa hilo na ukaweza kulifanyia kazi, utapunguza sehemu kubwa ya changamoto ulizokuwa unajitengenezea wewe mwenyewe.

SOMA; Tabia Kumi Za Kufanya Kila Siku Ili Kuufanya Mwaka 2015 Kuwa Mwaka Wa Mafanikio Makubwa Sana Kwako.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba nimekuwa naruhusu vitu vidogo vidogo vivuruge maisha yangu. Na nimekuwa nikifanya hivyo kwa kuamini kwamba watu wameamua kuniumiza. Sasa nimeelewa kwamba hakuna mtu aliyeamua kuniumiza, kila mtu anapitia changamoto zake na anajitahidi kufanya kile anachoweza. Kuanzia sasa sitakubali mambo haya madogo yaharibu siku yangu.

NENO LA LEO.

“Even though we often mess up, most of us are doing the best that we know how with the circumstances that surround us.”
― Richard Carlson

Japokuwa mara nyingi tunakosea, wengi wetu tunajitahidi kadiri ya uwezo wetu kulingana na tunachojua na hali inayotuzunguka.

Usikubali siku yako iharibike kutokana na anachofanya mwingine, jua na yeye anakazana kadiri ya uwezo wake, lakini pia anakosea.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.