Kuna kitu unaficha, na tumeshakustukia, sasa tuambie ni kipi hasa unachoficha.

Unapoamua kufanya kitu kwa kawaida, kuna kitu ambacho unakificha.

Unapokataa kuweka ubora wa hali ya juu sana kwenye kitu chochote ambacho unakifanya, kuna kitu unakificha.

Na inawezekana unajua unachoficha au hujui.

Ila leo tunakwenda kuweka kila kitu wazi, ili usiendelee tena kuficha chochote.

Kama kitu ni muhimu sana kwako, kama kitu kinastahili muda wako ambao ni rasilimali muhimu sana, kwa nini uamue kukifanya kawaida? Kwa nini ukifanye kwa viwango ambavyo kila mtu anaweza kufanya? Haiingii akili j kabisa, ndio maana nakuambia kuna kitu unaficha.

Inawezekana unaficha ukweli kwamba hupo tayari kufanyia kazi kile ambacho ni muhimu sana kwako. Na hivyo unatafuta sababu ya kukufanya uendelee kufanya kile ambacho sio muhimu na hivyo kukifanya kwa kawaida. Hili ni tatizo kubwa kwa sababu unajinyima fursa nyingi za kuboresha maisha yako.

Inawezekana pia unaficha ukweli kwamba unatafuta njia ya mkato ya kupata mafanikio, ambayo haipo. Hujawa tayari kuweka juhudi kubwa ili kufanya kwa ubora wa hali ya juu, kwa sababu juhudi kubwa zinaumizwa, na wewe umeshawishika kuna njia ya mkato ya kuweza kufika kule unakotaka kufika. Hapa napo pia umepotea na unazidi kupotea.

Inawezekana pia unachoficha ni kutokujua hasa ni nini unachofanya kwa hapo ulipo. Kukosa malengo na mipango na hivyo kujikuta unafanya tu kwa sababu ndivyo unavyotakiwa kufanya au ndivyo wengine pia wanafanya. Hii pia ni hatari kubwa sana kwa sababu hutafika popote, kwanza unafikaje sehemu ambayo hata hujui unapokwenda?

Ni wakati sasa wa kuacha kuendelea kuficha na kila kitu kitoke hadharani. Leo jiulize kwa kina sana kwa nini unafanya kwa kawaida. Kwa nini hujawahi kuwaacha watu mdomo wazi kwa ubora mkubwa uliotoa, kwa nini hujawahi kufanya maisha ya wengine yawe ya tofauti sana kupitia unachofanya?

Kuendelea kufanya kwa kawaida, ni kujichimbia shimo ambalo baada ya muda tutakusahau kabisa. Kwa sababu dunia ya sasa ina wengi wanaoweza kufanya unachofanya wewe, na wako tayari kukifanya kwa viwango vya juu sana. Amua sasa kuacha kawaida na kuweka ubora wa hali ya juu.

SOMA; KAWAIDA Ni Tafsida Ya HOVYO…

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kila ninalofanya kwa kawaida kuna kitu ambacho ninaficha. Na kitu hiki ninachoficha mwishoni hakitakuwa bora sana kwako, kwani kitanipoteza kabisa. Kuanzia sasa nimeamua kuondokana na kufanya mambo kwa kawaida. Nitaweka juhudi kubwa kwenye jambo lolote ninalofanya na kuhakikisha nalifanya kwa utofauti mkubwa.

NENO LA LEO.

“Man’s biggest limiting factor is being okay with the average and being satisfied with the usual”
― Constance Chuks Friday

Kikwazo kikubwa cha mtu kufanikiwa ni kukubali kuwa wastani na kuridhika na kawaida.

Kuwa kawaida ni adui mkubwa sana wa mafanikio, ni lazima uweke juhudi kubwa ili kuwa tofauti, kufanya kwa ubora sana.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.