Maisha siyo tu kuamka asubuhi, kufanya kile ambacho umezoea kila siku, kulala na kuamka tena kesho yake kurutia utaratibu huo. Kuna makusudi makubwa sana ya maisha ambayo kila mmoja wetu ni lazima ayajue na kuweza kuyafanyia kazi.

Hapa ndipo mwandishi Dan Millman ametushirikisha makusudi manne ya maisha ambayo kila mmoja wetu anahitaji kuyajua na kuyaishi ili aweze kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Katika kitabu hiki, mwandishi ametushirikisha makusudi hayo ambayo ni kama ifuatavyo;

Kusudi la kwanza ni kujifunza masomo tunayopitia kwenye maisha. Mwandishi amelinganisha maisha yetu kama darasa ambapo kila siku na kila wakati tunajifunza. Na hivyo moja ya kusudi lako ni kuhakikisha unajifunza vyema sana masomo hayo ili uweze kukua zaidi. Kila changamoto na ugumu tunaopitia kwenye maisha ni sehemu ya masomo yetu. Na kadiri tunavyoelewa masomo haya, kwa kutatua changamoto na magumu tunayokutana nayo ndivyo tunavyoboresha maisha yetu na kuwa na busara.

Kusudi la pili ni kutafuta kazi na wito wako, kujua umuhimu wa kujijua wewe mwenyewe na kuweza kufanya maamuzi sahihi kwako na kwa maisha yako. katika kusudi hili mwandishi anatushirikisha jinsi ya kuzitumia kazi zetu au wito wetu kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi na hivyo kuyafanya maisha yetu kuwa bora pia.

Kusudi ya tatu ni kujua njia ya maisha yako. hapa mwandishi anatushirikisha jinsi ya kujua ni ipi njia sahihi kwako kupita hapa duniani. Hapa anatuwezesha kujua ni kipi hasa tumekuja kufanya hapa duniani ili tuweze kukifanya kwa ubora na maisha yetu yawe bora zaidi.

Kusudi la nne ni kutumia wakati tulionao sasa. YAANI SASA HIVI. Hapa mwandishi anatuonesha nguvu kubwa tuliyonayo kwenye wakati wa sasa. Hapa mwandishi anatushirikisha mbinu za kuacha kufikiri zaidi kuhusu jana, ambayo tayari imeshapita, anatuasa tuache kufikiri zaidi kuhusu kesho ambayo bado haijafika, na badala yake tufikiri zaidi kuhusu sasa, na kufanya kwa ubora sana kile tunachofanya sasa ili tuweze kukifurahia na kuboresha maisha yetu. Wakati pekee ulionao wa kuishi ni sasa.

Yafuatayo ni mambo 20 kati ya mengi niliyojifunza kwenye kitabu hiki ambayo kama tukiyafanyia kazi maisha yetu yatakuwa bora zaidi. Karibu tujifunze kwa pamoja na tuchukue hatua mara moja;

1. Hukuja hapa duniani kukimbiza mafanikio pekee, uko hapa duniani kujifunza na maisha ya kila siku yatakupa mafunzo mengi sana ambayo yatakuwezesha kukua, kubadilika na kuamsha madhumuni yako makubwa hapa duniani. Na katika kujifunza hapa duniani, huwezi kufeli kama upo tayari kujifunza. Kama ambavyo jiwe lililopo kwenye mto linang’arishwa na mawimbi ya maji, na wewe pia unang’arishwa na mawimbi ya maisha.

2. Kila unachokutana nacho kwenye maisha yako ni somo, na masomo haya yanaanza kwa urahisi na kuongezeka ugumu kadiri unavyokwenda. Changamoto ni kwamba kama hutajifunza masomo yale rahisi mapema, unakosa nafasi ya kupata yale masomo magumu, ambayo ndiyo yangekufanya ukue sana. Na mbaya zaidi kadiri unavyochelewa kujifunza yale masomo rahisi, yanaanza kuwa magumu. Kadiri unavyochelewa kutatua changamoto ndogo, inazidi kuwa kubwa. Tatua kila changamoto kwa wakai wake, na jifunze kupitia kila changamoto.

3. Je unataka maisha yako yawe rahisi? Yasiwe na changamoto yoyote? Basi usioe/usiolewe, usiwe na watoto, usichukue majukumu yoyote, kila mara fanya kwa kiwango kidogo sana, usijitolee kwa jambo lolote. Kwa hivi maisha yako yataonekana rahisi. Lakini swali ni je sisi binadamu tumekuja hapa duniani kutafuta maisha rahisi? Au tumekuja hapa kukua na kuwa imara na wenye busara? Usiombe kuwa na maisha rahisi, omba kuwa na uwezo mkubwa wa kutatua changamoto unazokutana nazo.

4. Kama dunia ni shule na maisha yako ni darasa, basi kuna kozi ambazo unatakiwa kuzisoma na lazima uzifaulu ili uwe na maisha bora na yenye mafanikio. Na hapa kuna kozi 12 muhimu sana ambazo kila mmoja wetu lazima azisome na kufaulu. Kozi hizo ni; nidhamu, afya, mawazo, fedha, dhamira, hisia, ujasiri, kujijua mwenyewe, mapenzi, upendo, huduma na kujithamini. Haya ni maeneo muhimu sana kwenye maisha yako.

5. Tunajifunza mambo mengi sana, tunapata maarifa mengi sana, lakini changamoto ipo kwenye kuyageuza maarifa haya kwenda kwenye vitendo. Kuweza kugeuza kile unachojua kuwa maisha yako. baadhi ya watu wanachukua hatua bila ya kufikiri, na wengi sana wanafikiri bila ya kuchukua hatua. Kila mmoja wetu ana nguvu kubwa sana ndani yake ambayo kama akiweza kuitumia anaweza kubadili na kuboresha zaidi maisha yako. muhimu ni kujijua vyema ili kuweza kutumia nguvu hii.

6. Mwili wako ndiyo rasilimali muhimu sana ambayo unaimiliki. Rasilimali hii ndio itakayokuwezesha wewe kuishi yale maisha unayotaka. Na ili rasilimali hii ilete tija kwako ni lazima uijali, ni lazima uipe huduma zote muhimu ili iweze kufanya kazi. Afya yako ya mwili na afya ya akili ni muhimu sana kwako kuweza kuufanya mwili wako kuwa na nguvu ya kupambana na changamoto za kila siku za maisha.

7. Chochote ambacho unafanya kwenye maisha yako, kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Kifanye kwa ubora kiasi kwamba hakuna mwingine anayeweza kukifanya kwa ubora zaidi ya hapo ulipofikia wewe. Hii ndio siri ya uhakika kabisa ya kuweza kufanikiwa kwenye jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako. hata kama kazi yako ni kufagia bara bara, ifagie kwa ustadi mkubwa kiasi kwamba mtu akipita aseme hapa kuna mtu kaifagia hii barabara kwa utofauti kabisa.

8. Kazi ni tofauti na wito, kazi ni kile unachofanya ili kupata fedha, au kipato. Wakati wito ni kile unachofanya kwa sababu unapenda kufanya na kwa sababu kina mchango kwa watu wengine. Mara nyingi tunafanya kazi ili tulipwe na kuweza kuendesha maisha yetu, na tunafanya wito ili kuridhisha nafsi zetu na kuwasaidia wengine. Ukiweza kufanya wito wako ndio ikawa kazi yako, yaani ukalipwa kwa kufanya kile ambacho unapenda kufanya, utakuwa na maisha bora sana na ya furaha.

9. Kabla ya kujua wito wako ni nini, kabla ya kuchagua ni kazi ipi itakuwa bora kwako, kwanza kabisa jijue wewe mwenyewe. Ni jambo la kusikitisha lakini watu wengi wanakwenda maisha yao yote bila ya kujijua wao wenyewe. Jijue unapendelea nini, una madhaifu gani, ni maeneo gani uko vizuri. Na baada ya hapo ndipo unaweza kufanya maamuzi kazi gani inaweza kuwa bora kwako.

10. Hakuna kazi moja ambayo ni bora kuliko kazi nyingine. Kila kazi ni bora na kila kazi ni mbaya, hii inatokana na mtu mwenyewe. Kama unafikiri udaktari ndio kazi bora, basi jua kuna madaktari wanauchukia sana udaktari, ila wapo tu ili wapate fedha. Kama unafikiri ualimu ndio kazi bora, kuna walimu hawataki hata kusikia kazi hiyo, ila hawana jinsi kwa sababu wanataka kipato. Hivyo chagua kazi ambayo itakuwa bora kwako, kwa jinsi unavyojijua, na sio kwa sababu watu wanasema hii ni bora zaidi. Hivyo pia kwenye biashara, hakuna biashara moja bora kwa wote, kuna biashara bora kwa mtu fulani, tafuta ile ambayo ni bora kwako kwa unavyojijua.

11. Kwa kazi au biashara yoyote ambayo unaifanya, hakikisha unatoa thamani kwa wengine, hakikisha unatoa huduma ambayo inafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Kwa njia hii utapata hamasa ya kufanya zaidi na hivyo kufikia mafanikio makubwa. Lakini kama utafanya kazi au biashara kwa sababu tu unapata faida na hivyo kutokujali wengine wananufaika au kuumia, hutaweza kufika mbali.

12. Kuna siri kuu mbili za kufanikiwa kwa wale ambao wamejiajiri au wanafanya biashara. Siri ya kwanza kuwa vizuri sana kwenye kile ambacho unafanya, na kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Kwa sababu kama sio bora, hakuna atakayejisumbua kuja kwako, watakwenda kwingine wanakopata ubora, kila mtu anataka ubora. Siri ya pili kitangaze kile ambacho unafanya vizuri sana. Hakikisha kila mtu anajua kile unachofanya na hivyo ajue akipata shida inayohusiana na kitu hiko suluhisho analipata kwako. Haina maana kuwa unapika maandazi matamu sana halafu unayafungia ndani, lazima watu wajue kama maandazi yako. itangaze kazi yako vizuri.

13. Kila mmoja wetu hapa duniani ana wito wake binafsi, kuna vitu ambavyo anaweza kuvifanya vizuri sana kuliko watu wengine wote hapa duniani. Na japo dunia ina watu wengi, hakuna wawili ambao wanafanana kwa kila kitu, hata watoto mapacha. Moja ya kusudi lako kubwa ni kujua ni njia ipi unapaswa kupita ili kufikia lile dhumuni lako la maisha.

14. Kuna njia tisa za maisha ambazo kila mmoja wetu anapita kwenye moja au zaidi ya njia hizi. Njia hizo ni kama ifuatavyo, ubunifu, ushirikiano, kuonekana, uimara, uhuru, maono, uaminifu, kutambuliwa, uadilifu. Njia hizi zinatokana na zile tabia ambazo zimetawala sana maisha yetu na hizi ndio zinafanya maisha yetu na kile tunachofanya kuwa tofauti.

15. Haijalishi unaishi wapi na wala haijalishi umezaliwa kwenye utajiri au umasikini, bado una jukumu na uwezo wa kufikia maisha bora sana kwako. Muhimu ni kujua njia yako ni ipi na kuanza kuifanyia kazi.

16. Sasa ndio wakati muhimu sana kwako. Jana imeshapita na haitarudi tena, kesho haijafika na hivyo kuifikiria hakutaiathiri kwa vyovyote. Sasa ndio wakati pekee ulionao, ambapo unaweza kufanya chochote unachotaka. Upe wakati huu kipaumbele kikubwa kwenye maisha yako.

17. Kila wakati unaoupata ni zawadi kubwa sana kwa maisha yako, tumia kila wakati vizuri. Wakati mmoja unaweza kubadili siku, siku moja inaweza kubadili maisha, na maisha yaliyobadilika yanaweza kuibadili dunia. Usikubali wakati wowote upite bila ya kufanya jambo muhimu kwako.

18. Chochote unachofanya kwenye wakati wowote, weka mawazo yako yote kwenye kitu hiko. Kama unakula, weka mawazo yako yote kwenye chakula unachokula, ipate ile ladha halisi ya chakula, maana hiki ndio kitu muhimu kwa wakati huo. Usile huku unaangalia tv, au unatumia simu, kwa kufanya hivi unakosa mambo yote mawili.

19. Japokuwa ni muhimu sana kuweka malengo makubwa ya mbeleni, maamuzi unayohitaji kufanya ni ya wakati uliopo sasa. Unahitaji kufanya maamuzi ya hali unayopitia sasa. Kuhusu mambo ya baadae utafanya maamuzi wakati huo utakapofika. Wakati huu ni muhimu sana kwako, utumie kufanya yale ambayo ni muhimu.

20. Kitu kikubwa unachotafuta kwenye maisha yako, tayari unacho hapo ulipo, kwa wakati huu ulionao sasa. Kikubwa unachotafuta ni uhuru na furaha, na vyote vinaanza na wewe, vinaanzia ndani yako na unavyo hapo ulipo sasa. Utapata uhuru na furaha kwenye maisha yako kama utakuwa tayari kujifunza masomo unayopewa na maisha, kama utajijua wewe mwenyewe na kufanya kazi inayotokana na wito wako na pia kama utatumia muda ulionao vizuri, kwa kuweka mawazo yako kwenye kile unachofanya.

Hayo ndiyo makusudi makuu manne ya maisha yako, hakikisha unayafanyia kazi kila siku. Na fanya kusudi la nne kuwa ndio njia yako ya maisha. Chochote unachofanya weka mawazo yako pale, hata kama unatembea, tembea ukiwa umeweka mawazo yako kwenye kile unachofanya. Usifanye kitu chochote kama sio muhimu, kila unachofanya kwenye maisha yako ni muhimu na kinahitaji mawazo yako yawepo. Kama siyo muhimu usifanye.