Utawasikia wafanyabiashara wengi wadogo wakilalamika kwamba biashara ni ngumu sana. Watakupa kila sababu kwa nini biashara zao hazisongi mbele. Na unaweza ukakubaliana nao kabisa.
Ila sasa nenda kwenye biashara hiyo asubuhi, nenda na noti ya shilingi elfu kumi na unataka kitu cha shilingi mia tano. Unaweza hata ukatukanwa, mfanyabiashara atakushangaa unampaje noti ya elfu kumi asubuhi, ASUBUHI.
Kwa kifupi ni sawa na kukuambia unapokuja kununua kitu, hasa asubuhi, njoo na chenji yako, njoo na fedha iliyochenjiwa tayari au kama huna usije. Maana hata utakapompa hiyo elfu kumi, atakuambia chenji sina.
Sawa, labda tukubaliane kwamba chenji ni tatizo, lakini mbona ni tatizo asubuhi, jioni hakuna shida, ila asubuhi ndiyo shida. Bado huoni hapo tatizo ni zaidi ya chenji?
Kama unafanya biashara ndogo, au una watu wanaifanya, leo hii katoe kabisa somo la chenji. Kuwa na chenji sio jukumu la mteja, ni jukumu lako wewe binafsi, au wanaoendesha biashara yako. na kama jioni chenji zinapatikana, basi hakikisha na asubuhi zinapatikana.
Kama wewe ni mfanyabiashara makini na unaielewa biashara yako, unajua ni vitu gani vinanunuliwa sana wakati gani na mahitaji ya chenji ni kiasi gani. Basi jukumu lako ni kuhakikisha mahitaji hayo yanafikiwa. Andaa chenji mapema, zile unazokuwa nazo jioni fanya ndio za kuanzia. Na kama hitaji ni kubwa sana, unaweza kwenda kuomba hata benki, kama upo karibu na benki.
Hili la chenji ni jambo dogo sana lakini linawarudisha wengi nyuma. Na kama huwezi kujali kuhakikisha mteja anapata huduma na chenji yake, je unaweza kujali kuhusu kile mteja anachopata?
Hebu chukua hatua sasa, na ondokana kabisa na sababu hii ya chenji.
Kila la kheri.
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
ahsante sana coach.
LikeLike