Karibu tena kwenye makala hizi za biashara leo ambapo tunapeana mbinu za kuboresha biashara zetu zaidi. Na leo tutaangalia njia bora ya kutatua mgogoro unaoweza kuibuka kati yako na mteja wako.

Kama ambavyo tumeshaona kwenye makala zilizopita, mara zote mteja yupo sahihi, na kama kuna ushindani wowote kati yako na mteja, mwisho wa siku mteja ndiye atakayeshinda, hata kama wewe utakuwa umeshinda, lakini yeye ataondoka na ushindi zaidi, maana anaweza kuamua asije tena kwako na akasambaza maneno ya uongo kwa wengine.

Kujifunza zaidi kuhusu njia hii bora, nakushirikisha mfano wa changamoto aliyoandika mfanyabiashara mwenzetu na jibu nililomwandikia.

SWALI; Ahsante coach. Ni kweli mteja yupo sahihi mm Nina changamoto iliyonikuta. kuna mteja nilimhudumia vizuri tu akaondoka na bidhaa kisha kukaa nayo siku kama tatu hivi. ya NNE anarudi na bidhaa anasema nimempa mbovu hivyo nimbadilishie. hapo mm binafsi nilishindwa kufanya hivyo ikabidi aondoke nayo hivyo hivyo japo hakuridhika. sasa katika mazingira hayo usahihi Wa mteja hupo kweli? Selemani.

JIBU; Habari Selemani,
Hiyo ni changamoto kubwa, na hapo ndipo unapohitaji kutumia busara zako kufanya maamuzi sahihi.
Kwanza unaweza kuangalia uhalali wa madai ya mteja, je ni kweli ilikuwa mbovu, je wakati anachukua hamkuangalia kama ni nzima au sio nzima. Kama mliangalia na wote mkaridhika basi huenda ameharibu yeye. Ila kama hamkuangalia hapo na wewe umechangia.
Kufanya maamuzi sahihi unaweza kuangalia gharama utakayoingia wewe kama utaamua kumpa nyingine, kama siyo kubwa sana unaweza kufanya hivyo, kama ni kubwa unaweza kumwambia utampa kwa bei nusu.
Kwa vyovyote vile fanya mazungumzo na mteja huyo sio kwa hali ya kujitetea kwamba kosa ni lake, bali kwa hali ya kuangalia tunatatuaje hili, na nina hakika mtaishia vizuri sana na kila mtu ataridhika na atakuwa mteja wa kudumu kwako.
Ukikazana kufanya yeye aonekane ndio ana makosa, hata kama ni kweli, bado inaweza isiwe na msaada mkubwa kwako. Hujui ni wangapi atakaoenda kuwaambia kuhusiana na hali hiyo. Na mbaya zaidi ataenda kuwaambia uongo, unaomfanya yeye asionekane mwenye kosa.
Haya ni maamuzi unayohitaji kufanya kwa kufikiri kwa kina, yanaweza kukugharimu kiasi fulani, ila yataimarisha sana biashara yako.
Kila la kheri.

Nina imani umepata picha nzuri ya jinsi ya kutatua mgogoro wowote kati yako na mteja wako.

Kwa kifupi ni kwamba tatua mgogoro kwa nia ya wote mshinde, yaani win win, usitake tu wewe ushinde, angalia ni jinsi gani mteja naye anaweza kushinda, hata kama makosa ni yake. Kama ukiangalia changamoto vizuri, ni lazima utaona sehemu ambapo mnakutana pamoja.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz