Uhai wa biashara ni sawa na uhai wa binadamu. Ili mtu uendelee kuwa hai ni lazima mzunguko wa damu uwe sawa. Na ili biashara iendelee kuwa hai ni lazima mzunguko wa fedha uwe sawa. Mzunguko wa fedha ndiyo damu ya biashara yoyote ile.
Mzunguko wa fedha kwenye biashara unaanzia kwenye mauzo, bila ya mauzo hakuna mzunguko wa fedha na biashara inakufa.
Wafanyabiashara wengi wachanga huwa wanaingia kwenye biashara kwa mazoea tu, kwa sababu wameona wengine wanafanya au kwa sababu hawana kitu kingine cha kufanya. Huwa hawapati muda wa kukaa na kuweka mikakati bora kwa ukuaji wa biashara zao.
Leo hapa tutashirikishana mbinu kumi zakuongeza mauzo kwa wafanyabiashara, hasa wale ambao ni wachanga. Lakini pia zinawafaa wafanyabiashara wote. Karibu tujifunze.
1. Jua hasa ni tatizo gani biashara yako inatatua. Usiingie tu kwenye biashara kwa sababu umeona unaweza, jua ni kipi ambacho mteja anapata kutoka kwako.
2. Uza kile ambacho mteja anahitaji, na weka ubora wa hali ya juu sana. Kwa kuanza anza na yale mahitaji ya msingi ya wateja wako, kadiri unavyokwenda unaweza kuongeza mengine mapya.
3. Wafanye wateja wako kuwa watangazaji wa biashara yako. kwa kuwapa huduma bora sana na pia kuwashawishi kama wanawajua wengine wanaohitaji huduma au bidhaa unazotoa wawaambie.
4. Andaa vipeperushi vyenye huduma unazotoa na waombe wateja wako kuwasambazia wale ambao wanahisi wanaweza kuwa wateja pia.
5. Tengeneza mfumo wa kuwazawadia wateja wako pale wanapokuletea mteja mpya, siyo lazima iwe zawadi kubwa, jambo lolote dogo la kuwafanya wajione wa kipekee linafaa.
6. Chukua majukumu, kama kuna tatizo lolote linatokea litatue haraka, usiingie kwenye misuguano na wateja.
7. Weka bidhaa ambazo zinaweza kuuzika kwa pamoja, na shawishi wateja wanunue kwa pamoja kwa kuweka punguzo au zawadi. Kwa mfano kama unauza nguo, inaweza kuwa suruali bei yake, shati bei yake, ila ukasema atakayenunua suruali na shati basi kuna punguzo fulani, au anapewa zawadi ya tai, hapo utashawishi wengi kununua.
8. Ifanye biashara yako kuwa kitu ambacho watu wanazungumzia, kutokana na utofauti wake. Kadiri watu wanavyoizungumzia ndivyo wengi watakavyotaka kuifahamu. Ila ifanye izungumziwe kwa mambo mazuri na siyo mabaya.
9. Shiriki kwenye shughuli za kijamii kwenye lile eneo ambalo biashara yako ipo. Na shiriki kama biashara na hakikisha watu wanaifahamu vyema biashara yako.
10. Omba mawasiliano ya wateja wako, na kuwa na taarifa za wateja wako na mara kwa mara wasiliana nao hata kwa ujumbe kuwatakia wakati mwema. Kama alikuwa amesahau kuhusu wewe kwa kuona ujumbe wako ataifikiria biashara yako, na kama ana mahitaji atakuja. Ila usitume jumbe nyingi mpaka kuwakera watu.
11. Nyongeza; mwambie mteja ASANTE NA KARIBU TENA, neno dogo lakini lina athari kubwa sana, hasa unapolisema kwa kumaanisha kweli.
Fanyia kazi hayo na utaona mabadiliko kwenye biashara yako, na pia utazidi kupata mbinu nyingine nzuri zaidi.
Nakutakia kila la kheri.
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
shukrani sana kwa mambo hayo kumi na moja ya kuzingatia katika biashara ni mambo ambayo ni rahisi sana na ni wazi kuwa yanatekrezeka popote pale. kwahiyo ni jukumu langu kuyatekeleza kila siku ili kuikuza biashara yangu.
Pamoja sana.
LikeLike
Asante Mahule,
Yafanyie kazi hayo ili biashara iweze kukua zaidi.
TUPO PAMOJA.
LikeLike