Habari za leo rafiki?

Karibu kwenye mazungumzo yetu ambapo tunakwenda kushirikishana mambo mbalimbali ambayo ni muhimu kwetu ili kuweza kuishi maisha bora, ya furaha na mafanikio makubwa.

Katika mazungumzo ya leo tutakwenda kuangalia upande wa hukumu ambazo tumekuwa tunazitoa kila siku. Kama kuna kitu ambacho binadamu tupo vizuri, basi ni kwenye kuhukumu. Huwa hatukubali kitu kipite hivi hivi bila ya sisi kuweka hukumu zetu, kuamua ni nini hasa.

Tatizo la hukumu hizi ni kwamba ni za upande mmoja. Yaani tunakuwa na taarifa chache sana kabla hatujatoa hukumu zetu, na hivyo kwa sehemu kubwa hukumu zetu zinakuwa siyo sahihi. Kama kila mmoja wetu angepewa nafasi ya kuwa hakimu wa mahakama, wengi sana tungewafunga watu bila hata ya makosa.

Kabla hatujaingia ndani kwenye hili la hukumu na jambo muhimu kuzingatia, nitakushirikisha mfano mmoja ambao nilijifunza kwa mtu.

Bwana mmoja anasema alikuwa amepanda kwenye basi, basi lilikuwa na watu wachache na kila mtu alionekana kuwa amechoka na wametulia kuelekea majumbani mwao. Walipofika kituo cha mbele alipanda baba mmoja na watoto wadogo wawili. Baada ya watoto wale kuingia kwenye gari, hali ya hewa ilibadilika ghafla, watoto wale walikuwa wanapiga kelele, kukimbia kila kona ya gari na kuwasumbua watu wengine. Walikuta mtu anasoma gazeti na kumnyang’anya. Walikuwa wanaruka ruka kila kona. Na kwa wakati huo baba yao alikuwa amekaa kwenye kiti ametulia tu.

Yule bwana alipata hasira sana, kwa nini huyu mtu watoto wake hawana maadili, wanasumbua halafu hachukui hatua yoyote? Alianza kufikiria ni jinsi gani mtu yule alivyo na malezi mabovu kwa watoto wake, ambao hawana heshima hata kidogo. Hali iliendelea vile na hakuna hatua iliyokuwa inachukuliwa, ndipo bwana yule uzalendo ukamshinda na kuamua kumwambia mtu yule kwa nini asiwatulize watoto wake?

Bwana yule alionekana kama kustuka kutoka kwenye mawazo mazito, akamjibu sijui hata niwaambieje hawa watoto, maana tumetoka hospitali sasa hivi na mama yao amefariki, ila mpaka sasa hawajajua. Kwa jibu hili yule bwana aliingiwa na huruma sana na mtazamo wake ulibadilika kabisa. Alianza kuona huruma ni kwa jinsi gani watoto wale watakua bila mama, na kuona huruma jinsi mtu yule atawalea watoto wake mwenyewe. Baada ya kujua hili, hakuona tena walichokuwa wanafanya watoto wale kama ni kelele, bali aliona wanastahili kuwa na furaha angalau kwa wakati huo mfupi.

Kupitia mfano huo unaona ni jinsi gani ilivyo rahisi kuhukumu, hasa pale unapokuwa na taarifa chache za upande mmoja. Kutokana na kile ulichosikia au kuona, ni rahisi kufikia hukumu, lakini mara nyingi inakuwa siyo hukumu sahihi.

Kitu muhimu unachotakiwa kuzingatia kabla ya kuhukumu ni kuujua ukweli. Na ukweli utaujua baada ya kusikiliza kila upande na kuchambua ni kipi hasa kinachangia kwa jambo fulani. Katika kila jambo, iwe ni zuri au baya, kuna sababu nyingi ambazo zipo chini ya jambo hilo. Bila ya kuzichimba na kuzijua sababu hizo utakuwa unatoa hukumu kwa watu ambazo siyo sahihi.

Ubaya wa hukumu hizi zisizo sahihi ni kukuzuia kujua ukweli na pia kukukosesha ushirikiano mzuri na wengine. Unashindwa kuujua ukweli kwa sababu wewe unachagua taarifa chache na kuziamini na kisha kuja na hukumu yako. kwa taarifa hizi chache unafikiri unajua kumbe ukweli upo mbali sana. Pia unakosa watu wa kushirikiana nao kwa sababu unapohukumu bila ya kuujua ukweli unaishia kuwatenga wengine na hivyo kutokuwa na mahusiano bora.

Tabia hii ya kuhukumu bila ya kupata taarifa sahihi pia inapelekea wengi kuibiwa na kutapeliwa. Anakuja mtu anakutengenezea maelezo mazuri sana na ya kuvutia na wewe unahukumu haraka kwamba ni mtu mzuri na makini. Unajitoa kwa kumpa kile anachokitaka na baadaye ndiyo unakuja kugundua ya kwamba alichokuwa anakueleza awali siyo sahihi.

Tujifunze kuchukua muda na kupata taarifa sahihi, kuhoji zaidi na kudadisi. Kupata taarifa za pande mbalimbali kabla hatujatoa hukumu zetu wenyewe. Kwenye kila unachoona au kusikia, kuna mengi yanaendelea na yamechangia. Usihukumu kwa kutumia taarifa chache ulizonazo.

Nakutakia kila la kheri katika kutekeleza hili ulilojifunza leo, kuwa na subira kabla hujahukumu na pata taarifa zaidi, ujue ukweli ndipo ufanye maamuzi yako.

Rafiki na kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz