Kama bado hujaingia kwenye biashara na kama bado hujajua ni biashara ipi bora kwako kufanya, au kama umekuwa unafikiria kukuza biashara yako na kuanzisha biashara nyingine, huwa unafikiria mambo makubwa sana kabla ya kuingia kwenye biashara hiyo.
Tunafikiria mambo makubwa tukiamini kupata wazo bora la biashara inabidi tutumie nguvu kubwa sana. Hii ni sawa lakini siyo mara zote unahitaji kutumia nguvu hizi kubwa, hasa kwenye ulimwengu wa sasa ambapo mambo yanabadilika kwa kasi kubwa sana.
Biashara tayari unayo hapo ulipo, huhitaji nguvu kubwa kuweza kuifikiria biashara hiyo, bali unahitaji kufungua macho yako na uweze kuiona. Hapo ulipo na kwa kile ambacho unafanya, kuna vitu ambavyo watu wanavitegemea sana kutoka kwako. Kuna vitu ambavyo watu wakishindwa wanakuja kwako, na wanakuwa hawana wasi wasi kwa sababu wanajua watapata suluhisho.
Jua vitu hivi na angalia ni jinsi gani unaweza kuvitoa kwa ubora zaidi kwa wengine, huku ukitoza kiasi kidogo cha fedha. Kila mmoja wetu ana ujuzi na uzoefu ambao anaweza kuutumia kutengeneza kipato zaidi. Ni kujua ujuzi huu na wale ambao wanauhitaji na kisha kuweza kuwapatia ujuzi huo.
Na katika kupata wateja, huhitaji kuanza na wateja elfu moja ndiyo useme umeshakuwa na biashara, huhitaji hata wateja 100, wala siyo lazima wawe 10, unaweza kuanza na wateja watatu pekee. Pata watu watatu ambao wapo tayari kulipia ule ujuzi au uzoefu ulionao ambao wengine wanauhitaji. Wapatie wateja hawa watatu huduma bora na zitakazowasaidia. Na hapo utaweza kuwafikia wengi zaidi.
Uzuri wa dunia ya sasa ni kwamba kama unataka kuanza biashara yako mwenyewe, huhitaji kutumia muda mwingi kukaa darasani kujifunza biashara. Au kutumia gharama kubwa kufanya utafiti na kuja na wazo bora la biashara. Badala yake unaweza kuanza na kitu kidogo ambacho tayari unakifanya sasa, na ukaweza kutengeneza biashara kubwa.
Kuanzia leo unaweza kuanza na kukuza biashara kubwa kutoka kwenye wazo ambalo wengi hawafikirii linaweza kuwa biashara. Unachohitaji ni kuwa tayari kutoa thamani kubwa na kuboresha zaidi kila siku. Anza kidogo na endelea kukua kuwafikia wengi zaidi. Hii ni njia bora ya kuanza na kukuza biashara hata kama huna mtaji mkubwa.
Leo jiulize je ni ujuzi au uzoefu au maarifa gani ambayo wewe unayo na wengine wanayahitaji sana? Je unawezaje kuwafanya watu wengine walipie ujuzi au maarifa hayo uliyonayo wewe? Anzia hapo na utajenga biashara kubwa.
TUPO PAMOJA,
Kocha Makirita Amani.
SOMA; Njia tano za kujua kama wazo lako la biashara ni bora.