Unachagua kuharibu maisha yako mwenyewe pale unapokubali kuwa mwathirika. Pale unapoona ya kwamba mambo yanatokea kwako kwa sababu huna jinsi ya kupambana nayo, unapoteza nguvu zako zote na kushindwa kuchukua hatua. Pale unaporuhusu utu wako wa ndani kushindwa na mambo yanayotokea nje yako, kila siku unaona maisha ni mabaya kuliko siku iliyopita.
Ni rahisi sana kubeba tabia hii ya uathirika, kwa sababu watu wengi kwenye jamii zetu ni waathirika. Watu wanapenda kulalamika na kutafuta watu wa kuwapelekea lawama pale mambo yanapokwenda tofauti na walivyotarajia. Wewe usikubali hili, iwe mambo yamekwenda tofauti kutokana na mambo ambayo wengine wamefanya au hawajafanya, usikubali wao wawe ndiyo sababu ya maisha yako kuwa hovyo.
Una nguvu ya kuchagua ni aina gani ya maisha unayotaka kuishi, na kama hupati aina hiyo una muda wa kuendelea kupambana mpaka utakapoyapata. Badala ya kupoteza muda kulaumu wengine kwa vitu walivyofanya au walivyoshindwa kufanya kwako, tumia muda huo kuweka juhudi ili kuhakikisha unapata unachotaka.
Watu wengi wamekuwa waathirika wa wazazi wao, utawasikia wakisema kama mzazi/wazazi wangefanya/hawakufanya kitu fulani, ungekuta leo niko mbali sana. Inaweza kuwa kweli, lakini sasa umeshatambua hilo, kwa nini usichukue hatua?
Wengi zaidi wamekuwa waathirika wa wanasiasa na viongozi wengine. Hapa utasikia watu wakilaumu mifumo ya siasa jinsi inavyowazuia kutekeleza majukumu yao kama walivyopanga.
Kuna ambao wamekuwa waathirika wa mabosi au waajiri wao, ambapo wanashindwa kufanya kile ambacho wanajua ni muhimu kwao kutokana na mabosi wao.
Kwa vyovyote vile, haijalishi hali ya nje ni mbaya kiasi gani, haijalishi wengine wamekuangusha kiasi gani, usikubali kunyoosha mikono juu ya kwamba maisha yako yanashindwa kwenda kutokana na mtu mwingine. Kumbuka wewe ndiye mwamuzi wa mwisho wa maisha yako, amua kuwa na maisha bora kwa kuepuka kuwa mwathirika na kupambana mpaka uwe shujaa.
Ni kweli, njia siyo rahisi na changamoto ni nyingi, na hii ndiyo inafanya maisha ya mafanikio kuwa ya thamani kubwa kuliko maisha ya uathirika. Usikubali kuwa mwathirika, badala yake pambana uwe shujaa.
Maisha ya mafanikio ni kwa ajili ya mashujaa, na wewe ni mmoja wa mashujaa hao.
Kila la kheri.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.