Kama kuna neno ambalo umeshalisikia mara nyingi kwenye maisha yako, huenda ni neno HAPANA. Hili ni neno ambalo wengi wamekuambia pale ambapo umekua unajaribu kufanya mambo ya tofauti au mambo makubwa kuliko ambavyo imezoeleka na wengine.

HAPANA ni neno kali na linalokatisha tamaa hasa pale linapotoka kwa mtu ambaye unamwamini sana au mtu wa karibu yako. lakini leo nataka nikuambie kitu kimoja kuhusu wanaokuambia hapana, wanakosea sana.

Watu wanaokuambia hapana wanakosea sana, na hawakosei kuhusu wao ila wanakosea kuhusu wewe. Inawezekana kabisa kwa ujuzi wao na uwezo wao, wameshakubali kwamba kitu fulani hakiwezekani. Ila hawajui kuhusu wewe.

Hawajui uwezo mkubwa ambao upo ndani yako,

Hawajui hamasa kubwa iliyopo ndani yako ya kutaka kuleta mabadiliko na kufanya makubwa.

Hawajui mapenzi makubwa yaliyopo ndani yako kuhusu kile unachotaka kufanya.

Na pia hawajui ni kwa kiasi gani umejitoa ili kupata kile ambacho unataka kufanya.

Watu hawa wanakosea sana na sisi tunakubali kuchukua makosa yao na kuwa ukweli wetu.

Ufanye nini?

Jichague wewe mwenyewe, jikubali kwa kile unachotaka kufanya na kupata, weka juhudi kuhakikisha unakipata. Endelea kufanya kila siku mpaka wale waliokuwa wanakuambia hapana washindwe kusema tena hapana. Lakini kumbukua hufanyi kwa ajili yao, bali unafanya kwa ajili yako mwenyewe.

Usipokee makosa ya wengine na kuwa yako, wewe ndiye unayejua ni nini hasa unachotaka, wewe ndiye unayejua uwezo ulionao, wewe ndiye unayejua ni kiasi gani upo tayari kujitoa. Hapana za wengine zisizime yote haya.

Fanyia kazi kile unachoamini na hakuna kitakachoweza kukurudisha nyuma.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; Mambo matano(5) muhimu ambayo hujawahi kuambiwa kuhusu ujasiriamali.