Kabla wengine hawajakuamini, ni lazima ujiamini wewe mwenyewe kwanza.

Kabla wengine hawajaamini kwenye ile biashara unayofanya na kuwa wateja, ni lazima wewe mwenyewe uiamini biashara hiyo kwanza.

Kabla wengine hawajakuamini kwamba unaweza na kukupa kazi au dili nzuri ni lazima wewe mwenyewe ujiamini kwamba unaweza.

Imani inaambukizwa, unachoamini ndicho ambacho wale wa karibu yako watakipata kutoka kwako.

Unapoamini kwenye kile unachofanya, unapata hamasa ya kukifanya kwa juhudi kubwa zaidi. Hata unapokutana na mtu na akakupinga, hatakuyumbisha kwa vyovyote vile kwa sababu wewe unajua kile unachofanya ni bora.

Lakini kama huamini kile unachokifanya, wanapotokea watu na kukupinga utatetereka kwa sababu imani yako siyo dhabiti.

Kwenye dunia hii ambayo imejaa ushindani na kukatishwa tamaa, imani ni muhimu sana katika kuyafikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Kile unachoamini ndiyo kinachowavutia wale ambao wanakuzunguka. Kama unaamini mambo hayawezekani, utazungukwa na watu ambao wanaamini hayawezekani. Kama unaamini mambo yanawezekana, wale wanaoamini hayawezekani hawataweza kuvumilia kuwa karibu na wewe na hivyo watakimbia.

Unahitaji imani isiyotetereka juu yako mwenyewe na juu ya kile unachofanya. Imani itakayowafanya watu wajisikie salama kuwa na wewe iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kawaida.

SOMA; SIKU YA 27; IMANI, Nguzo Muhimu Sana Ya Kufikia Mafanikio.

Hivyo tunaweza kusema bila ya shaka yoyote kwamba mafanikio makubwa yanaanza na imani. Swali ni je ni kipi unachoamini kuhusu wewe binafsi, kazi yako na hata biashara yako? Simamia kile unachoamini na utawavutia watu sahihi kwako ambao utaweza kushirikiana nao.

Imani lazima iambatane na matendo, hivyo usiishie tu kusema unaamini kitu fulani, bali fanya kile kinachoendana na imani yako. kwa kuweka matendo unaboresha zaidi imani yako kuwahamasisha wengi zaidi.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)