Sasa tunaishi kwenye zama za taarifa ambapo wale ambao wana taarifa sahihi kwa wakati sahihi na kuchukua maamuzi sahihi ndiyo wanaofanikiwa kwenye jambo lolote wanalofanya. Ni zama za kipekee sana ambazo tunaishi sasa ambapo mtu mmoja anaweza kushindana na kampuni kubwa.
Mtu mmoja mwenye kompyuta iliyounganishwa na mtandao wa intaneti anaweza kuwafikia watu wengi kuliko gazeti lenye wafanyakazi 50. Hii ndiyo nguvu ya zama hizi za taarifa, ambapo kompyuta na mtandao wa intaneti umeleta mabadiliko kwenye kila eneo la maisha yetu.

Kila mtu analijua jina la BILL GATES, huyu ni mtu tajiri namba moja duniani na pia mwanzilishi wa kampuni kubwa ya kompyuta inayoitwa MICROSOFT. Linapokuja swala la kompyuta na mtandao wa intaneti, basi wote tunaweza kukubaliana kwamba Bill Gates anajua hayo kuliko wengi wetu. Hivyo tuna wajibu wa kumsikiliza na kujifunza kutoka kwake.

Mwaka 1998, wakati mtandao wa intaneti ulikuwa bado haujapamba moto kama sasa, wakati huo wachache na hasa wenye uwezo mkubwa ndiyo walikuwa wanamiliki kompyuta, Bill Gates aliona mbali sana, aliona dunia ambayo karibu kila mtu atakuwa anatumia kompyuta yake mwenyewe. Aliona jinsi ambavyo kompyuta na mtandao wa intaneti utakavyoathiri kila eneo la maisha yetu, kuanzia kazi, biashara na hata afya zetu.
Lakini wakati huo wengi hawakuona hilo, wengi waliendelea kufanya biashara kwa mazoea. Bill Gates aliandika kitabu BUSINESS @ THE SPEED OF THOUGHT kuwaamsha wale ambao hawakuona mapinduzi haya makubwa. japokuwa kitabu hiki amekiandika muda mrefu, nimeona mengi ambayo bado huku kwenye nchi zetu zinazoendelea hatujaweza kuyafanyia kazi.

Biashara nyingi bado zinaendeshwa nje ya mtandao wa intaneti, yaani wafanyabiashara wengi bado hawapatikani kwenye mtandao wa intaneti na hawajaweza kutumia maendeleo haya ya kiteknolojia katika kurahisisha biashara zao.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki cha Bill Gates ambapo tunakwenda kujifunza namna tunavyoweza kutumia kompyuta na mtandao wa intaneti kufanya kazi zetu, biashara zetu na hata maisha yetu kwa ujumla kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa.

Karibu tujifunze kwa pamoja.

1. Hakuna wakati ambapo biashara zimekuwa na ushindani mkali kama sasa, na ushindani huu unatokana na urahisi wa kuingia kwenye biashara. Hivyo njia ya uhakika ya mfanyabiashara kujiweka mbele ya wengine ni kuwa bora sana kwenye kile anachofanya, na kuwa bora kunatokana na taarifa anazopata na namna anavyozifanyia kazi. Wafanyabiashara wenye taarifa sahihi kwa wakati sahihi na kuchukua hatua mapema ndiyo wanaunufaika na fursa zinazojitokeza kila wakati. Pata taarifa sahihi ili uweze kufanikiwa kwenye biashara unayofanya.

2. Taarifa zinazopatikana kwa sasa ni nyingi kuliko muda ambao mtu anaweza kupata wa kuzichambua na kuzifanyia kazi. Hivyo tatizo siyo tu kutokuwa na taarifa, bali kuweza kuchambua taarifa muhimu kutoka kwenye taarifa nyingi. Hapa Bill Gates anasema ni lazima uwe na mfumo mkuu wa taarifa kwenye biashara yako (DIGITAL NERVOUS SYSTEM). Kama ulivyo ubongo wako, unakusanya taarifa kutoka kila eneo la mwili wako na kuchukua hatua ili uweze kuwa hai. Hivyo ndivyo unavyopaswa kuitengeneza biashara yako, uwe na mfumo ambao utakusanya taarifa, kuzichakata na kuzitumia katika kufanya maamuzi sahihi.

3. Mzunguko wa taarifa kwenye biashara ndiyo uhai wa biashara. Haitoshi tu kuwa na taarifa, bali kama taarifa hizi atakuwa nazo kiongozi na wale wa chini yake hawana, haiwezi kuwa na msaada. Kila mtu anayehusika anapaswa kuwa na taarifa sahihi ili aweze kufanya maamuzi sahihi. Kuna ule ufanyaji biashara wa kizamani ambapo mmiliki wa biashara alikuwa anaficha baadhi ya taarifa wafanyakazi wake wasizijue, hii ina madhara makubwa kuliko faida. Pale kila anayehusika kwenye biashara anapojua kila kinachoendelea, anakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya maamuzi yatakayoiwezesha biashara kukua.

SOMA;  KITABU CHA JULY; MIMI NI MSHINDI, Ahadi Yangu Na Nafsi Yangu.

4. Kama unafikiri una taarifa za kutosha kuhusu biashara yako, jaribu kujibu maswali haya kuhusu biashara yako;
a/. Wateja wako wanafikiriaje kuhusu bidhaa au huduma unayotoa kwenye biashara yako?
b/. Ni matatizo gani ambayo wateja wako wanataka yatatuliwe?
c/. Ni vitu gani vipya wanataka uongeze kwenye biashara yako?
d/. Ni changamoto gani ambazo mshirika wako wa kibiashara(kama yupo) anazipata kupitia biashara mnayofanya kwa pamoja?
e/. Ni maeneo gani ambayo washindani wako wa kibiashara wanapata faida kubwa ambayo wewe bado hujayajua?
f/. Je mabadiliko kwenye mahitaji ya wateja wako yanaweza kukusukuma wewe kubadili biashara unayofanya>
g/. Ni masoko gani mapya yanajitokeza ambayo bado hujaingia?
Kama huna majibu ya kutosha kuhusu maswali hayo basi huna taarifa za kutosha kuhusu biashara yako.

5. Hakuna kampuni inayoweza kujitamba kwamba iko salama kwenye soko lake, kwa ulimwengu wa sasa wenye ushindani mkali, kitu chochote kinaweza kuigwa. Biashara makini lazima mara zote iwe inaangalia mwenendo wa soko lake. Unaweza kufanya hivi kama utakuwa na taarifa za kutosha.

6. Kila kampuni/biashara ni lazima iweze kutumia mtandao wa intaneti katika kukusanya, kusambaza na kutoa taarifa zake. Hivyo kila biashara inahitaji kuwa na tovuti, hapa ndipo nyumbani kwa biashara, ambapo wateja wanaweza kujua kuhusu biashara hiyo. Pili kila biashara lazima iwe na mfumo wa barua pepe (email) ambapo watu wote wanaohusika kwenye biashara hiyo wanaunganishwa pamoja kwenye mfumo huo. Tatu kila biashara inahitaji kuwa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo sehemu kubwa ya wateja wapo huko.

7. Pamoja na matumizi makubwa ya mtandao wa intaneti, haitakiwi kuondoa umuhimu wa ana kwa ana. Bado kampuni inapaswa kufanya vikao vya ana kwa ana, lakini vinakuwa vimerahisishwa na mtandao wa intaneti. Kwa mfano kabla ya watu kuhudhuria kikao wanakuwa wameshatumiwa ripoti kupitia email zao na wanakuja wakiwa tayari wameipitia na maoni yao kuhusu hali inavyokwenda.

8. Kila biashara ni sawa na mwili wa binadamu, ambapo kuna vitu muhimu vinavyofanya uhai wa mwili uendelee kuwepo. Mfano moyo unasukuma damu inayosambaza virutubisho mwilini, na mapafu yanayoleta hewa ya oksijeni ambayo ni muhimu kwa maisha. Kwenye biashara moyo ndiyo uzalishaji ambao unatoa bidhaa au huduma ya biashara husika. Na mapafu ndiyo usimamizi wa biashara ambao unafanya biashara iendelee kuwa hai. Ili biashara iweze kufanikiwa, lazima mifumo hii iweze kufanya kazi kwa pamoja. Unapokuwa na taarifa sahihi kuhusu biashara yako, unaweza kuwa na usimamizi mzuri.

9. Mtandao wa intaneti unamwondoa mtu wa kati kwenye biashara nyingi. Kabla ya ujio wa intaneti, kati ya mzalishaji na mlaji kulikuwa na mtu wa kati, au watu wa kati ambao walikuwa wakitoa bidhaa na huduma kutoka kwa mzalishaji kwenda kwa mlaji. Lakini mtandao wa intaneti unamwezesha mlaji kununua moja kwa moja kutoka kwa mzalishaji.
Kwa mfano zamani kampuni za mawakala wa usafiri wa ndege, zilikuwa zikipata faida kubwa kwa kuwasaidia watu kukata tiketi za ndege, lakini sasa hivi karibu kila shirika la ndege linamwezesha mteja kukata tiketi yake mwenyewe akiwa nyumbani kwake kupitia mtandao wa intaneti kwenye tovuti ya kampuni.

10. Njia pekee ambayo mtu wa kati anaweza kuendelea kunufaika ni kuongeza thamani kwenye biashara husika. Huwezi kuendelea kuwa mtu wa kati kwa kufanya kile ambacho mteja anaweza kufanya mwenyewe kupitia mtandao wa intaneti. Badala yake mtu wa kati anahitaji kuongeza thamani ambayo itafanya mteja kupata huduma bora zaidi.
Kwa mfano wa kampuni ya uwakala wa safari za ndege, badala ya kumsaidia mtu kukata tiketi pekee, wanahitaji kumshauri mtu kuhusu usafiri bora, kumweleza kuhusu kule wanakotaka kwenda na mengine mengi muhimu. Kama hutaweza kuongeza thamani unaondolewa sokoni.

11. Mtandao wa intaneti umetoa uhuru mkubwa sana kwa wateja kuweza kupata kile ambacho wanakitaka, kile hasa kinachoendana nao. Zamani wafanyabiashara ndiyo walikuwa na nguvu ya kuamua ni nini wazalishe na mtu alilazimika kununua hata kama hakiendani naye kama anavyotaka. Uwepo wa wazalishaji wengi, na urahisi wa kupata taarifa unawapa wateja uhuru wa kutafuta kile hasa wanachotaka. Hivyo unahitaji kuwa na taarifa za kutosha kuhusu wateja wako ili uweze kuwa nao kwa muda mrefu, kwa kuwapa kile wanachotaka.

12. Kwa biashara zinazotoa huduma, mtandao wa inateni unatoa nafasi mbili, ni ama uwe mtoaji wa ujazo mkubwa kwa gharama ndogo, au utoe kile ambacho kinaendana na mteja moja kwa moja kwa gharama kubwa. Hapa unachagua kati ya kutoa kitu cha kawaida, ambacho kitawafaa wengi kama utauza kwa bei rahisi au utoe kitu cha kipekee ambacho kinaendana na wateja wachache ambao wapo tayari kulipa gharama kubwa. Unahitaji kuwa na taarifa ndiyo uweze kuamua unakwenda upande upi. Kila upande una faida na hasara zake.

13. Mtandao wa intaneti hauwezi kuondoa nafasi ya watu, bali inafanya watu kuwa bora zaidi kwenye kazi zao. Haina maana kwamba ujio na ubora wa intaneti kadiri siku zinavyokwenda utaondoa kabisa uhitaji wa watu, badala yake utawawezesha watu kufanya maamuzi bora zaidi. Biashara bado zinahitaji watu kuendesha na hivyo hakuna haja ya kuhofia nafasi za watu kuchukuliwa na teknolojia. Ila wale ambao hawataichukua teknolojia hii na kuitumia, nafasi zao zitapotezwa.

14. Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo tunavyozidi kugundua matumizi bora zaidi ya mtandao wa intaneti. Hii ina maana kwamba hapa tulipo bado hatujajua matumizi yote ya mtandao huu, kadiri siku zinavyokwenda ndiyo tunajua zaidi. Kwa mfano wakati mtandao huu unaanza, watu walikuwa wakitumia email na tovuti pekee, ni zaidi ya miaka kumi baadaye ndipo watu waligundua mitandao ya kijamii kupitia mtandao huu. Hatujui miaka kumi ijayo itakuwaje, lakini itakuwa bora kuliko ilivyo sasa, hivyo usikubali kuachwa nyuma. Wale walioona mitandao ya kijamii ni mambo ya vijana, wanajuta sasa, kuwa tayari kujifunza na kubadilika.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Sign-Posts On The Road To Success (Alama Muhimu Kwenye Safari Ya Mafanikio).

15. Mtandao wa inateni unatuwezesha kutengeneza jamii mpya za watu ambao tunaendana. Sasa hivi hulazimiki kuungana na ile jamii inayokuzunguka, badala yake unaweza kutafuta jamii inayoendana na kile unachoamini na mkawa pamoja kupitia mtandao wa intaneti. Makundi ya kwenye mitandao ya kijamii kama facebook na wasap yanawaleta pamoja watu wanaoamini kitu kimoja. Tumia nafasi hii kujenga jamii ya watu wanaoendana na biashara yako au kupata taarifa za kutosha kuhusiana na biashara yako.

16. Mtandao wa intaneti umerahisisha sana ufanyaji wa kazi kwenye biashara na makampuni. Zamani ilikuwa ukitaka kufanya kitu kwenye biashara yako ni mpaka uajiri mtaalamu wa kukifanya na hivyo kumlipa mshahara pamoja na kuingia gharama nyingine kama za posho za makazi, matibabu na kadhalika. Lakini mtandao wa intaneti umerahisisha sana hili, huhitaji tena kuajiri kwa kila jukumu la biashara yako. kuna majukumu unaweza kutafuta mtu kupitia mtandao wa intaneti, akafanya na likikamilika mkataba wenu unaishi hapo.
Kwa mfano kama unataka kutengeneza tovuti ya biashara yako huhitaji kuajiri msanifu wa kukutengenezea tovuti hiyo, badala yake unaweza kutoa jukumu hili kwa mtu anayetoa husuma hizo, akakutengenezea na mkishamaliza kila mtu anafanya mambo yake. Taarifa kama hizi unazipata kupitia mtandao wa intaneti.

17. Mtandao wa intaneti unatoa uhuru mkubwa wa mtu kuamua kujiajiri mwenyewe bila ya kuungana na wengine na kuwa washirika. Kwa mfano zamani mwanasheria alihitaji kujiunga na wenzake ili kuanzisha kampuni ya kisheria, au daktari kuungana na wenzake ili kutoa huduma za kitabibu. Walifanya hivi ili kusaidiana kutafuta wateja. Lakini sasa hivi kwa kuwa na kompyuta na mtandao wa intaneti na taarifa za kutosha, mwanasheria mmoja anaweza kuwa na kampuni yake ya kisheria, au daktari mmoja anaweza kutoa huduma za kitabibu kwa wateja wengi atakaopata kupitia mtandao huu.
Karibu kila utaalamu unaweza kunufaika na matumizi ya mtandao wa intaneti, kuanzia ualimu, uhasibu, ubunifu, usanifu, uinjinia, udalali na kazi nyingine.

18. Mtandao wa intaneti umefupisha muda ambao bidhaa inatumia tangu kuzalishwa mpaka kufika sokoni. Zamani bidhaa ilizalishwa, kisha inachukuliwa na mtu wa kati, na ndipo inapelekwa kwa mteja. Lakini sasa hivi mteja anaweza kununua moja kwa moja kutoka kwa mzalishaji. Hii inafupisha mzunguko wa wauzaji wa jumla na rejareja. Kwa kuwa na taarifa sahihi, biashara inaweza kuchukua hatua mapema na kunufaika na fursa. Dunia ya sasa watu wanataka bidhaa bora, kwa bei nafuu na wanataka bidhaa hizo sasa. Ni wewe mfanyabiashara kujua na kuchukua hatua.

19. Kila kampuni huwa inafanya makosa, kila biashara inapitia nyakati ambazo ni ngumu na changamoto ni kubwa. Biashara yoyote lazima itegemee nyakati kama hizi na hivyo kukusanya taarifa za kutosha ili kuweza kujua ni wakati gani sahihi wa kuchukua hatua. Ni lazima biashara iwe n adata za kutosha kuhusu uzalishaji wake, wateja wake, mauzo yake, faida zake. Na taarifa hizi zinapaswa kuwa kwenye mfumo ambao mabadiliko yoyote yanayotokea yanaonekana haraka. Kwa mfano kuwa na chati zinazoonesha mwenendo wa biashara, mambo yanapobadilika ni rahisi kuonekana.

20. Habari njema kwako, kwa kuwa na kompyuta, na mtandao wa intaneti una uwezo mkubwa wa kufanya chochote unachotaka, unayo dunia kwenye mikono yako. unaweza kumfikia mteja yeyote pale alipo, ni wewe kuwa na taarifa sahihi na kuchukua hatua sahihi. Hakuna ambacho huwezi kukifanya kupitia mtandao huu wa intaneti, hasa kwenye kukuza biashara yako;
Unaweza kuuza vitabu, nyimbo, video, nguo, viatu, mazao, huduma na vingine vingi. Uwepo wa mitandao ya kijamii umefanya kuwafikia wengi zaidi kupitia mtandao huu. Usikubali kuwa mtumiaji tu wa mitandao hii, badala yake anza kuifanya kuwa sehemu ya biashara yako. Kama hujui unawezaje kutumia mitandao hii kuboresha biashara yako karibu nikushauri namna bora ya kutumia mtandao kuboresha biashara yako. Nitafute kwa wasap kwenye namba 0717396253, karibu sana.

Hakuna uhuru mkubwa tunaoufaidi sasa kama mtandao wa intaneti, hakuna mapinduzi makubwa tunayoyashuhudia kama mapinduzi ya taarifa, usibaki mtazamaji, ingia ucheze.
Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita