Maisha uliyonayo sasa ni matokeo ya maamuzi unayoyafanya kila siku kwenye maisha yako. Maamuzi yoyote unayoyafanya kila siku, yana uwezo wa kufanya maisha yako ya kesho kuwa mazuri au mabaya.
Kwa mfano, upo hapo na maisha yako hivyo kwa sababu ya maamuzi kadhaa ambayo ulishawahi kuyafanya kipindi cha nyuma. Maamuzi yako uliyokuwa ukiyafanya iwe kwa kujua au kutokujua ndiyo yaliyokufikisha hapo.
Kwa hiyo unaona ili kufanikiwa, maaumuzi mazuri ni kitu cha msingi sana. bila kuwa na maamuzi ya msingi itakuwa ni ndoto kubwa kufikia mafanikio. Ndio maana kila wakati unatakiwa ujiulize maamuzi ninayo yafanya sasa yanajenga maisha yangu au yanabomoa.
Ukishajua aina ya maamuzi sahihi unayotakiwa kuyafanya itakusaidia sana kubadilisha maisha yako. kwa kawaida wengi huwa ni watu wa kuharibu maisha yao kwa kufanya maamuzi yasiyo na miguu wala kichwa. Kwa kifupi wanafanya maamuzi yanayo wagharimu sana.
Ili kufanikiwa tunaona, ni lazima kujijengea maamuzi sahihi yanayokuongoza kwenye mafanikio. Kupitia makala hii leo, tutajifunza aina ya maamuzii ambayo ukiyafuata kila wakati yatabadilisha misha yako kabisa. Je, ni maamuzi yapi sahihi unayotakiwa kuyafata ili yakupe mabadiliko ya kweli?
1. Uamuzi wa kuchagua kufikiri.
Tatizo walilonalo watu wengi ni watu wa kuwaza tu na sio kufikiri. Naona unashangaa unawaza naongea kitu gani? Sikiliza, ipo tofauti kubwa kati  ya kufikiri na kuwaza.
Kufikiri ni mchakato unakufanya ukupe majibu juu ya suluhisho la matatizo yako. Unapokuwa unafikiri unakuwa unaweza ni nini ufanye ili uwaze kufanikiwa au kutoka kwenye hali ngumu uliyonayo.
Lakini unapowaza, unakuwa hutafuti sana suluhisho la mambo yako, zaidi unakuwa unaongozwa na matukio ya kawaida. Sasa ili uweze kufanikiwa ni lazima sana kwako wewe kufikiri na kupata majibu ya kie unachokitaka.
Ni muhimu kuchagua kufikiri kwa sababu hiyo itakupa mafanikio makubwa. Jiulize binafsi unafikiri au unawaza tu. Kama unawaza tu, elewa kufikia mafanikio yako itakuwa ni ngumu sana.
2. Uamuzi wa kuchagua kile tunachokizingatia.
Kile unachokizingatia sana kwenye akili yako ndicho unachokipata. Hauwezi kupata kitu ambacho hujakiweka kwenye akili yako. Kila wakati angalia ni kipi unachokizingatia sana na kukiwaza kila wakati kwenye akili yako? Kwani hicho bila shaka ndicho utakachokipata bila wasiwasi.
Unaweza ukawa shahidi katika hilo, hebu angalia yale mambo yote uliyoyatimiza kwenye maisha yako. Ukifatilia utagundua kwamba mambo hayo uliyazingatia sana kwenye akili yako kwa namna moja au nyingine ndiyo uliyoyapata. Hivyo, ni muhimu kuwa na uamuzi wa kuzingatia kile unachokitaka, utakipata hicho.
3. Uamuzi wa kuchagua kupanga mipango bora.
Kuchagua kufikiri vizuri na kuchagua kile tunachikizingatia hiyo peke yake haitoshi. Ili kuweza kubadilisha maisha yako kabisa pia unatakiwa pia kujiwekea mipango bora. Ni lazima kuweza kukaa chini na kupanga  kitu gani ni unachokitaka katika maisha yako.
Ukiishi tu kiholela bila kujiwekea mipango mizuri hiyo itakusumbua sana hata kufikia mafanikio yako makubwa. Watu wenye mafanikio makubwa ni watu wa kuishi kwa mipango mizuri ambayo badaae huamua kuisimamia mpaka itimie.
4. Uamuzi wa kuchukua hatua.
Kupanga mipango mizuri pekee hakutasaidia kama hatua sahihi hazitachukuliwa. Hivyo, hatua ni kitu cha muhimu sana ambacho kila wakati unatakiwa kukizingatia ii kuweza kufanikiwa. Bila kuzingatia kuchukua hatua kwa hakika hiyo inakuwa ni sawa na kazi bure.
Kumbuka kwa kuzingatia kila wakati uamuzi wa kuchagua kufikiri, uamuzi wa kuchagua kile tunachokizingatia, uamuzi wa kuchagua mipango bora na uamuzi wa kuchukua hatua dhidi ya maisha yako, hiyo itakusaidia sana kwako wewe kuweza kufanikiwa na kubadilisha maisha yako.
Nikutakie siku njema na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku.
Kwa makala nyingine nzuri, tembelea DIRA YA MAFANIKIO kuweza kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,