Siku ya leo utakutana na watu wema, watu wenye roho nzuri na wenye kukutakia mema kwenye maisha yako na kile unachofanya.  Watu hawa watakufanya uone jinsi gani maisha ni mazuri na binadamu wanavyothaminiana. Watakupa hamasa ya kuendelea kufanya kile unachofanya kwa ubora zaidi.

Siku ya leo pia utakutana na watu ambao siyo wema, watu wenye roho mbaya ambao wanaangalia kila njia ya kukunyonya wewe. Utakutana na watu ambao watakukatisha tamaa kwenye kile unachofanya na ukajiona kama hujui unachofanya. Watu hawa watakuwa wanajaribu kukulaghai na kufanya mambo mengine ambayo yanakurudisha nyuma. Kwa kukutana na watu hawa unaweza kuiona dunia kama sehemu chungu sana ya kuishi na maisha hayana maana.

Ni muhimu kujua kwamba watu wa aina hizi wapo na utakutana nao mara kwa mara. Hivyo usikubali mipango yako ivurugike kutokana na tabia hizi za wengine. Wewe endelea na mipango yako na endelea kuweka ubora, ukikutana na watu wema furahia na unapokutana na wale ambao siyo wema jifunze.

SOMA; ONGEA NA COACH; Kuwa Mwema Kwa Watu Ambao Hawahitaji Wema Wako.

Tegemea kukutana na watu tofauti kila siku, na jua njia bora ya kuweza kuenda nao. Huna haja ya kushindana au kutaka kuwaonesha wengine kwamba unaweza kuwanyoosha. Watu ambao siyo wema wamekuwa vile kutokana na ujinga wao na kushindwa kuona fursa kubwa zilizopo duniani za kumwezesha kila mtu kupata kile anachotaka.

Kuwa mwema kwa wengine na wawezeshe kupata kile wanachotaka.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)