Hakuna mtu anayeweza kufanikiwa yeye mwenyewe, ndiyo maana mimi huwa nakataa sana neno SELF MADE MILLIONAIRE (yaani milionea aliyejitengeneza mwenyewe).
Ukweli ni kwamba hata uwe na akili kiasi gani, hata uwe na malengo na mipango bora kiasi gani, hata uweke juhudi kubwa kiasi gani, huwezi kujitengeneza wewe mwenyewe na kuwa milionea au bilionea. Unahitaji ushirikiano kutoka kwa wengine. Na hata kufika mpaka pale unapochagua kwamba unauendea umilionea, kuna wengi waliokusaidia kufika hapo.
Hivyo tuweke hayo mambo ya ‘self made’ pembeni na sasa tuangalie ni namna gani tunaweza kutengeneza mahusiano bora na wale wanaotuzunguka ili waweze kutusaidia kufikia ndoto zetu. Huwezi kufanya kila kitu wewe mwenyewe, na ili ufanikiwe unahitaji watu waliojitoa kufanya kile ambacho unataka kufikia.
Ipo misingi mitatu, izingatie vyema;
Msingi wa kwanza; thamini watu.
Thamini sana watu, hawa ndio watakaokufikisha popote unapotaka. Hawa ndiyo watakaokuwa washirika wako kibiashara, ndiyo watakaokuwa wateja wako, ndiyo watakaokuwa majirani zako. Ni muhimu uwathamini watu kwa sababu utawahitaji kwenye kila hatua ya maisha yako. Hata kama umepiga hatua kubwa kiasi gani, usiwadharau wengine, huwezi kujua ni wakati gani utamhitaji mtu fulani. Wathamini watu na pale unapohitaji ushirikiane nao, wape kile ambacho wanastahili kupata kama mlivyokubaliana.
Hakuna kitu ambacho mtu yeyote anapenda duniani kama kuonekana wa thamani. Ukitaka kupata wateja wa kudumu kwenye biashara yako, wathamini. Ukitaka kupata watu bora wa kushirikiana nao wathamini. Mtu akithaminiwa anafurahi sana na atajitoa kufanya kile anachotakiwa kufanya.
Msingi wa pili; sifia juhudi.
Katika mahusiano yako na wengine, hasa wale ambao mnafanya kazi pamoja, au wanaokufanyia kazi, sifia juhudi ambazo mtu anaweka. Watu wanapenda kufanya kile ambacho wamesifiwa kwamba wanafanya vizuri. Hivyo kama unataka mtu aendelee kuweka juhudi zaidi, sifia zile juhudi anazoweka. Huenda hapati majibu bora kwa wakati huo, ila kama anaweka juhudi kubwa, atapata tu majibu mazuri. Wewe sifia zile juhudi anazoweka, ataziongeza na hatimaye kupata majibu bora.
SOMA; TATU MARA TATU, Vitu Vitatu Vyakufanya Kila Siku Ili Kuwa Na Maisha Bora Yenye Furaha Na Mafanikio.
Msingi wa tatu; tuza ufanisi.
Watuze watu kulingana na kile ambacho wamekamilisha kufanya. Usiwatuze watu kwa upendeleo wa aina nyingine yoyote bali kile ambacho wamekifanya. Hii itajenga msingi sahihi kwa watu kupata sawasawa na wanachozalisha. Ukikosea katika kutoa tuzo au zawadi, utaharibu kabisa kile unachotaka kufikia. Watu wakiona kwamba wale wanaofanya vizuri kweli ndiyo wanaopewa zawadi basi na wao watakazana ili wapate zawadi. Ila watu wakiona watu wanapewa zawadi kwa upendeleo basi na wao watatafuta njia zitakazowaletea upendeleo ili na wao wazawadiwe.
Mafanikio yako yapo mikononi mwa wengine, ni wewe kujua jinsi ya kuwashawishi wakupe mafanikio hayo. Tumia misingi hii mitatu ili kupata ushirikiano bora kutoka kwa wengine na uweze kufikia ndoto zako.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)