Huwezi kuijua thamani ya fedha mpaka pale umeifanyia fedha hiyo kazi, umeumia na kusumbuka kisha ukaipata fedha. Hapo ndipo utaona thamani yake na kuiheshimu fedha hiyo. Hivi ndivyo hali ilivyo kwetu wanadamu, tunathamini kile ambacho tunajua hatukipati kwa urahisi.

Na ndiyo maana wale wanaopata fedha kwa urahisi huwa wanazitumia hovyo pia. Kwa mfano watu wanaoshinda bahati na sibu hujikuta wametumia fedha zote na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida. Au wale wanaorithi mali, hujikuta wakiuza mali hizo na kurudi kwenye maisha magumu.

Najua unajua hili, lakini kwa nini nakuambia tena leo?

Kwa sababu nataka uwafundishe wale wanaouzunguka, ukianza na familia yako na ndugu zako, kuhusu thamani ya fedha. Najua una mafanikio, na hata kama bado hujakaa vizuri kifedha kwa sasa, siku siyo nyingi utakaa vizuri.

Kwa jamii zetu za kiafrika, mtu mmoja akishafanikiwa kwenye familia, basi wengine wanaona ahueni, hawajisumbui tena kwa sababu wanajua yule aliyefanikiwa atakuwa anawapa kile wanachotaka. Sasa wewe ukiwa mtu wa kuwapa ndugu na watu wako wa karibu fedha, huwasaidii bali unawaharibu kabisa. Huwafundishi thamani halisi ya fedha, na siku wewe ukishindwa kuwapa basi utakuwa umewafanya vilema.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Ni Kiasi Gani Cha Fedha Unahitaji Kuwa Nacho Ili Kuwa Na Maisha Bora Na Yenye Furaha?

Madhara makubwa sana yanakwenda kwa watoto wetu, wewe mzazi kwa kuwa na mafanikio makubwa kunaweza kumbwetesha mtoto. Wewe mwenyewe unaweza kumbwetesha kwa namna unavyompa fedha au yeye mwenyewe anaweza kujibwetesha kwa namna anavyopiga mahesabu yake. Anapoona mali na kujua kabisa zile ni zake baada ya wewe kufariki, inamfanya ajione yupo kwenye upande salama, anaweza asijisumbue sana.

Unahitaji kuondoa fikra za namna hii kwa watoto wako, wafanye waielewe thamani ya fedha kwa kuhakikisha wanatoa thamani fulani ndiyo wapate fedha, hata kama ni wewe unawapa. Usiwazoeshe kupata fedha nyingi bila ya sababu a msingi au bila ya usimamizi makini. Unaweza kuona unamsaidia kwa sasa, lakini ukawa unamharibia mno kwa baadaye.

Wape watoto wako nafasi ya kufanya makubwa kwenye maisha yao kwa kuwafundisha thamani halisi ya fedha kadiri umri wao unavyokwenda. Na siyo thamani ya fedha pekee, bali thamani ya kila kitu kwenye maisha yao. Ni muhimu wakue na mtizamo sahihi kwa sababu dunia haina huruma, haijalishi huyu katokea familia ya hali ya juu au ya hali ya chini. Inatoa changamoto sawa kwa wote, ni vyema watoto wako wakawa tayari kukabiliana na changamoto hizo.

Wafundishe watoto wako thamani halisi ya fedha na namna inavyopatikana, msingi huu utawawezesha kuwa na maisha bora na uhuru wa kifedha watakapokuwa watu wazima.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)