Rafiki, chukua jiwe, liweke ndani na acha muda uende, jiwe litaendelea kuwa pale pale. Lipe jiwe hilo chochote unachoweka kulipa, maji, chakula, mbolea na vingine vingi, bado jiwe litabaki kuwa vile vile.

Lakini chukua mti na uweke ndani kisha upe yale muhimu, mti huo utakua na muda siyo mrefu utakuwa hauenei tena pale ulipouweka.

Leo tunakwenda kujifunza dalili za maisha ambazo pia ni dalili za mafanikio, na dalili hizo ni ukuaji. Kitu ambacho kinakua kina maisha na kinafanikiwa pia. Ila kitu ambacho hakikui hakina maisha, na hakiwezi kufanikiwa.

Dalili za kwamba wewe utafanikiwa ni kama unakua, kama ulivyo leo ni bora kuliko ulivyokuwa jana au mwezi uliopita au mwaka uliopita, basi unakua na unafanikiwa. Lakini kama leo huna tofauti na jana, au mwezi uliopita au mwaka ulipopita, maana yake hukui na pia hufanikiwi. Binadamu tunapaswa kukua, tunapaswa kuendelea, tunapaswa kubadilika na tunapaswa kufanikiwa.

Ufanye nini?

Leo jifanyie tathmini kwenye maisha yako, je unakua na kubadilika au upo pale pale maisha yako yote.

Je kuna tofauti yoyote kwenye maisha yako ya leo na maisha yako ya mwaka jana?

Je namna unavyofanya kazi zako leo ni bora zaidi kuliko ulivyokuwa unafanya mwaka jana?

Vipi kuhusu biashara unayofanya, je ni kama ilivyokuwa mwaka jana au sasa hivi ni bora zaidi.

Fanya tathmini hii kwenye kila eneo la maisha yako, kisha chukua hatua stahiki.

Kumbuka kitu chochote chenye maisha, kitu chochote chenye mafanikio, kinakua. Hakikisha wewe pia unakua kila siku ili uweze kuwa na maisha bora na yenye mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK