USHAURI; Ufanyeje Pale Familia Yako Inapopinga Ndoto Zako?

Changamoto ni sehemu ya kudumu ya maisha yetu, japo tunaweza kuona changamoto kama kikwazo chetu cha kuwa na maisha ya mafanikio, changamoto zitaendelea kuwepo kadiri tunavyoishi. Changamoto zako za kimaisha zitaisha pale maisha yako yatakapokwisha. Kama bado unaishi basi nikuhakikishie jambo hili moja, utakutana na changamoto.
Hivyo basi, kujifunza njia bora za kutatua changamoto tunazokutana nazo ni hitaji muhimu la kila binadamu.

Ni matumaini yangu kwamba wewe rafiki yangu ni mzima kabisa, uko vizuri ukiendelea kuweka juhudi kubwa kwenye kile ulichochagua kufanya kwenye maisha yako. Kwa juhudi kubwa unazoendelea kuweka, tegemea kupata matokeo bora sana.
 

KUPATA TIKETI YA KUSHIRIKI SEMINA HII PIGA SIMU NAMBA 0717396253 AU 0755953887


Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto, ambapo tunashauria namna bora ya kutatua changamoto tunazopitia kwenye maisha yetu. Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya ndugu wa karibu na familia kupinga ndoto yako. Yaani unakuwa na ndoto ya maisha yako, unakuwa na malengo na mipango mikubwa ya maisha yako, lakini watu wako wa karibu wanakuambia unachofikiria hakiwezekani au hakitakunufaisha. Badala yake wanakuja na ndoto nyingine ambazo haziendani na wewe.
Kabla hatujaangalia hili kwa undani na hatua za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu.

Mimi changamoto yangu ni familia yangu inanilazimisha nikaajiriwe niachane na biashara yangu ya library na ndoto zangu za kucheza soka nizifute. Bernard Z. P.

Hii ni changamoto kubwa kwenye safari ya mafanikio, kwa sababu mara nyingi familia zetu, hasa wazazi, wamekuwa wakitamani kuona maisha yetu yanakuwa bora sana. Hivyo wamekuwa wakikazana kutushauri namna bora ya kwenda na haya maisha ili tuwe na maisha bora. Sasa pale inapotokea ndoto yako inatofautiana na kile wazazi wanachofikiria, inakuwa changamoto kubwa.

SOMA; Kuwa Dereva wa Maisha Yako

Je ni hatua gani unazoweza kuchukua ili kutatua changamoto hii?

1.     Waelewe familia na wazazi wako.
Kabla ya kuchukua hatua yoyote, kwanza waelewe wazazi na familia yako. Elewa kwamba ndani ya mawazo yao wanataka wewe ufanikiwe, wanataka wewe uwe na maisha bora. Hivyo wanajitahidi kuangalia njia bora kwako kuweza kuwa na maisha mazuri.
Japokuwa wanataka uwe na maisha mazuri na ufanikiwe, haimaanishi wapo sahihi kwenye kile ambacho wanataka ufanye. Huenda kile wanachokushauri ufanye ndiyo kitu pekee wanachojua kinafaa. Hawajui kama kuna njia nyingine za kuwa na maisha bora na ya mafanikio.

Kwa mfano kwa wazazi na familia nyingi za Kitanzania, wanaamini sana kwenye ajira. Wanaamini mtu akishakuwa na ajira basi ana uhakika wa maisha. Licha ya changamoto zilizopo kwenye ajira, licha ya uhaba wa ajira uliopo, wao wanaamini ajira ndiyo kila kitu. Hata pale mtu anapokuwa na mpango wa kufanya biashara, au kujiajiri, hushauriwa kuanza na ajira kwanza.
Ni vyema ukaelewa hili kabla hujachukua hatua yoyote, maana litakusaidia katika maamuzi utakayofanya.

2.     Wasikilize na elewa hofu yao iko wapi.
Pale ambapo ndoto zako na za familia yako zinatofautiana, wasikilize na jua hofu yao iko wapi. Wazazi na familia yako wana hofu juu ya ndoto uliyochagua. Kuna kitu wanahisi utashindwa kufanya na hivyo maisha yako kuwa magumu.
Jua hofu yako iko wapi, ili utakapofanya maamuzi ya kwenda na ndoto yako, uweze kuitetea na kuisimamia kwa maisha yako yote.

SOMA; Mambo Yanapokuwa Magumu Unafanya nini?

3.     Kumbuka wewe ndiye utakayeishi maisha yako.
Wazazi na familia yako wanaweza kuwa na nia nzuri sana kwako, lakini ukweli ni kwamba, wewe pekee ndiye utakayeishi maisha yako. Hakuna mtu mwingine atakayekuja kuishi maisha yako kwa ajili yako. Hivyo unapofanya maamuzi, fanya ukijua utayaishi muda wote wa maisha yako.
Wazazi na familia wanaweza kukupa mipango mizuri sana ya namna ya kuishi maisha yako, lakini kumbuka wewe pekee ndiye utakayeyaishi. Kuyachukua mapendekezo yao ili kuwaridhisha, kutakufanya uishi maisha ambayo huyafurahii. Hivyo chagua kama unataka kuwa na maisha bora kwako au ya kuwaridhisha wengine.

4.     Kumbuka hakuna njia moja ya uhakika kwa wote.
Hakuna njia moja ya uhakika ya mafanikio kwa watu wote. Hakuna kitu kimoja ambacho kila mtu akikifanya basi atafanikiwa. Binadamu tunatofautiana, anachofanya mmoja akafanikiwa, mwingine anaweza kufanya akashindwa kabisa. Kuna ambao wanaweza kufanya ajira na wakawa na maisha bora, wengine wakifanya biashara ndiyo wanakuwa na maisha mazuri.
Hivyo licha ya ushauri utakaopewa, jua siyo kila kitu kitafanya kazi kwako, hivyo fanya maamuzi kutokana na vile vitu unavyopendelea kufanya na ambavyo upo tayari kujitoa kwa hali ya juu.

5.     Fanya maamuzi na yaishi maamuzi hayo, usijilaumu baadaye.
Ukishawaelewa wazazi na familia, kisha ukajiangalia wewe mwenyewe ni vitu gani unapendelea kufanya, sasa unaweza kufanya maamuzi ya maisha yako. Fanya maamuzi ambayo utaweza kuyaishi. Fanya maamuzi ambayo utayasimamia hata pale mambo yatakapokuwa magumu, na kwa uhakika yatakuwa magumu.

Kwa maamuzi utakayofanya, usijilaumu au kuyajutia pale unapopata matokeo ya tofauti na ulivyotegemea, badala yake jifunze kwa kila hatua na boresha zaidi.

Utakapofanya maamuzi ambayo ni tofauti na ushauri na mategemeo ya wazazi na familia, ukikutana na changamoto watasema tulikuambia sisi, sasa kama na wewe utakuwa mtu wa kujilaumu, utayaharibu maisha yako. Fanya maamuzi na kuwa tayari kupokea lolote ambalo litakuja kwenye maisha yako. Chagua kufanya kile ambacho upo tayari kukifanya kwa moyo wako wote, hata kama kipato siyo kikubwa mwanzoni.

SOMA; Kama Utafanya Uamuzi Huu Leo, Utabadilisha Hali Yako Ya Kipato Kabisa.

Fanyia kazi mambo hayo matano tuliyoshauriana ili kuweza kufanya maamuzi bora ya maisha yako. Chochote unachofanya, kumbuka wewe ndiye mhusika mkuu, wengine wanaweza kukushauri, lakini wewe pekee ndiye unayepaswa kufanya maamuzi ya maisha yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz  

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: