Jambo kubwa linalowashangaza wengi wanaoianza safari ya mafanikio, ni namna watu ambao waliwategemea wawape moyo wanakuwa wa kwanza kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa.
Watu ambao walikuwa wanakuambia unaweza kufanikiwa, unaweza kufanya makubwa na kauli nyingine kama hizo, wanapokuona unaanza kufanya wanakuwa wa kwanza kukuambia unakosea, au huwezi au utashindwa.
Hii ni hali inayowashangaza wengi kwa sababu hawakuitegemea. Leo nataka nikuambie ya kwamba, tegemea na jipange kwa hili, kwa sababu litatokea kwenye kila siku ya maisha yako. Usishangazwe na hili linapotokea.
Unapoamua kuishi maisha yenye maana kwako, yale maisha ambayo yanakupa furaha na kuwezesha kutoa mchango mkubwa kwa wengine, watu watakusema vibaya. Watu wataangalia makosa yako madogo madogo na kuyakuza sana kama vile ni wewe pekee unayekosea. Kila utakachofanya watakuwa na njia ya kuonesha kwamba siyo kizuri, au unakosea, au utashindwa.
Nimekuwa najifunza hili kwa watu wengi waliofanikiwa, kuna watu watakuja na ushahidi wa mabaya yao. Wengine watasema wana roho mbaya, wengine watasema walikuwa wanyonyaji na mengine mengi. Lakini kikubwa ninachokuja kuona ni kwamba wale wanaofanikiwa wana tabia ambazo ni tofauti na watu wengine na tabia hizi ndiyo zinawafanya wafanikiwe. Sasa kwa sababu wengine hawajazoea tabia hizo wanazichukulia ni mbaya.
Kwa mfano wengi waliofanikiwa sana wanafanya kazi muda mrefu kuliko wasiofanikiwa. Hutawakuta wamekaa wikiendi nzima wanafuatilia mipira, au wakishinda baa na marafiki kupata vinywaji, au kuwakuta kwenye kila kijiwe na kila mtandao wakibishana mambo yasiyo na maana kwao. Sasa wale wanaofanya hivyo kila siku, wanawaona wasiofanya wanakosea, watawaambia punguza kazi na upate muda wa kuwa na wengine, na maneno mengine kama hayo.
Sasa leo nataka nikuambie kitu kimoja rafiki, chochote kikubwa utakachotaka kufanya, watu hawatakosa la kuongea juu ya kitu hicho. Hivyo wewe usiendeshwe na watu hawa, badala yake fanya maamuzi yako kulingana na malengo na mipango yako.
Fanya kile ambacho ni muhimu kwako, fanya kile ambacho unapenda kufanya, na fanya kile ambacho kina mchango mkubwa kwa wengine. Wakusema wataendelea kusema vyovyote watakavyo, wewe siyo wa kusema, wewe ni wa kufanya. Hivyo. Fanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK