Sababu Muhimu Zinazosababisha Wanandoa Wengi Kuishi Maisha Ya Ujane Wakati Wenza Wao Bado Wako Hai.

Habari ya wakati huu mpendwa rafiki na msomaji wa amka Mtanzania? Natumaini uko salama rafiki na unaendelea vizuri kuhakikisha unatimiza wajibu wako wa kila siku. Hongera pia, kwa zawadi ya siku hii ya leo natumaini pia umeinza siku yako kwa ushindi na furaha. Pole pia rafiki, kwa changamoto zote unazopitia katika maisha hakuna hali ya kudumu katika maisha. Hivyo basi, vumilia, kabiliana na changamoto unazopitia wala usizikimbie na kamwe usikate tamaa katika maisha yako kwani bado hujachelewa kama bado uko hai. Napenda kuchukua nafasi hii kukualika mpendwa msomaji wa amka Mtanzania tuweze kujifunza kwa pamoja makala nzuri niliyokuandalia siku hii ya leo.

 

Katika makala yetu ya leo tutakwenda kujifunza mambo ya mahusiano hususani maisha ya ndoa na mengine. Maisha yetu yametawaliwa sana na mahusiano hivyo ni muhimu sana kujifunza mambo ya mahusiano kwani mahusiano ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Kila mtu kwanza ametokea katika mahusiano hivyo basi kiasili kabisa binadamu tuna mahusiano ya vina saba yaani DNA. Maisha yetu yanakuwa yanaenda vizuri kama mahusiano yetu nayo yako vizuri. Wanandoa wengi wanajikuta wameingia katika shimo na badala ya kuacha kuendelea kuchimba na kutoka lakini bado wanaendelea kuzama na hatimaye inakuwa ni ngumu sana kutoka kama umeshajichimbia shimo refu. Kabla ya kuingia katika maisha ya ndoa ni vema kwanza ukachunguza vizuri mtu unayetaka kuja kuishi naye kwani makosa ya watu wengi wanaongozwa na hisia katika kutafuta wenza wao badala ya kuongozwa na akili.

SOMA; Hizi Ndizo Hazina Saba (07) Muhimu Katika Maisha Ya Ndoa.

Rafiki, kuongozwa na hisia katika kutafuta mwenza inasababisha watu wengi kuingia katika shimo na baadaye anajikuta tayari ameshazama na hawezi kutoka tena. Katika malengo mahususi ya somo letu la leo ni kutaka kujua kwa nini wanandoa wengi wanaishi maisha ya ujane wakati wenza wao bado wako hai? Waswahili wanasema nyumba usiyolala hujui hila yake ni kweli kabisa kama Waswahili wanavyosema. Wapo wanandoa wengi wanaishi maisha ya ujane lakini wenza wao bado wako hai. Kwanini hali hii inatokea? Sababu kubwa moja ni watu wanaoishi maisha ya ndoa kila mmoja hawajibiki katika nafasi yake kwa mfano kama baba hasimami katika nafasi yake na kuwajibika ipasavyo kama baba vivyo hivyo mama naye. Kwa mfano, baba ni mlevi hajishughulishi na kitu chochote kuhusu familia mzigo wote wa familia kuwatunza watoto na kuhakikisha wanapata mahitaji yote ya msingi anamwachia mama.

Mpendwa msomaji, unakuta wanandoa wengine tokea waingie katika mahusiano yao yeye hajawahi kusikia kitu kinachoitwa upendo katika familia. Unakuta wanaume wengine ndani ya nyumba wao ni sauti tu na kutoa maagizo na amri ndani ya nyumba na kushindwa kuvaa nafasi yake katika familia. Mpaka hapa rafiki umeshaanza kupata mwanga kwa nini wanandoa wengi wanaishi maisha ya ujane wakati wenza wao bado wako hai. Inafikia mahali watu wanajuta hata kwa nini hata alijiingiza katika mahusiano na mtu aliye naye sasa hivi. Unaweza ukawa umeshakufa katika mioyo ya watu tayari kabla hata bado hujafa na inapotokea tu pale unapokuwa umekufa kweli watu watalia tu ili mradi waonekane nao wamelia wasije wakaambiwa wao ndio wameshiriki katika kifo.

SOMA; Hizi Ndiyo Njaa Mbili Zinazowasumbua Wanandoa Katika Maisha Yao Ya Ndoa.

Sasa, kwa nini wanandoa wanakuwa wanaishi maisha ya ujane wakati bado wako na wenza wao ni kwa sababu wenza wao wanakuwa tayari wameshakufa mioyoni mwao na hawapo tena. Hii ni mbaya sana mwenza wako anaona tayari umeshakufa katika moyo wake na haupo kabisa mko mnaishi lakini moyoni hakuna kitu kabisa. Hata ikitokea moja wa wenza kufa mwenzake anaona alishakufa siku nyingi katika moyo wake kwa hiyo ataona ni hali tu ya kawaida hivyo itabidi tu avae uso wa huzuni ili watu wasije wakamuona yeye ndiye aliyeshiriki kumuua kama akiwa hana uso wa huzuni. Hivyo kama wewe uko katika mahusiano ya ndoa huenda mke wako au mume wako katika moyo wake umeshakufa tayari siku nyingi. Kama uko hai na watu wanaona umeshakufa katika mioyo ya watu tafadhali badili mwenendo wa maisha yako.

SOMA; Hawa Ndio Maadui Wakubwa Wawili Wa Uchumba Au Ndoa Yako.

Huenda umeshakufa tayari katika mioyo ya watu katika jamii yako, katika familia yako kama wewe ni mama au baba watoto tayari wameshakuona umekufa katika mioyo yao wakati bado uko hai. Pengine uko katika kazi zako wateja wanakuona siku hizi umeshakufa katika mioyo yao kulingana na huduma mbovu unayotoa. Unafanya kazi kimazoea bosi na wafanyakazi wenzako wanakuona tayari umekufa katika mioyo yao. Huenda umeshakufa siku nyingi katika mioyo ya watu bila hata ya wewe kujijua hivyo ni wakati wa kuchunguza na kutathimini mwenendo wa maisha yako kila idara unayoijua wewe na kuweka mambo sawa.

Hatua ya kuchukua leo. Jichunguze na jitathimini na fanya tafakuri na siyo tafakari ingia ndani zaidi katika maisha yako huenda umeshakufa siku nyingi katika mioyo ya watu. Huenda umeshakufa siku nyingi katika moyo wa mpenzi wako, huenda umeshakufa siku nyingi katika mioyo ya marafiki zako kulingana na mwenendo wa maisha yako, jamii kwa ujumla na watu wanaokuzunguka. Huwezi kufa katika mioyo ya watu kama unasimama katika nafasi yako na kuwajibika ipasavyo. Hata kama wewe ni kiongozi jichunguze huenda umeshakufa siku nyingi katika mioyo ya wananchi wako wanakusubiria ufe tu kabisa wakuzike na kukusahau. Usikubali kufikia hatua hii katika maisha yako badilika leo.

Kwa hiyo, ndugu msomaji, somo letu la leo limetualika sisi sote kujichunguza maisha yetu kwa ujumla huenda tunaishi tunaonekana tuko hai kumbe siku nyingi tulishakufa katika mioyo ya watu. 

Kila mmoja anajua wajibu wake na madhaifu yake ni vema kurekebisha ile sehemu ambayo unahisi haupo tena katika mioyo ya watu na ulishakufa siku nyingi. Wajibika ili tuifanye dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: