Upo usemi kwamba mwanzo ni mgumu, na usemi huu unafanya kazi kwenye kila jambo, kuanzia ukuaji wetu mpaka shughuli zetu.
Pata picha ya mtoto mdogo ambaye anajifunza kutembea, anasimama na kuanguka, anapiga hatua moja anaanguka. Lakini mtoto huyu hasemi kutembea ni kugumu basi naachana nako. Bali anaendelea na baada ya muda anakuwa akitembea bila ya shida yoyote.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara, mwanzo ni mgumu, tena mgumu sana. Kama ndiyo mgeni kwenye biashara, utahitaji kujifunza mambo mengi kwa vitendo. Utakutana na changamoto nyingi ambazo hakuna aliyewahi kukuambia.

Na gumu zaidi, utahitaji kuvaa kofia nyingi kwa wakati mmoja. Yaani utakuwa mkuu wa vitengo vingi kwa wakati mmoja.
Kosa kubwa sana ambalo wafanyabiashara wengi wageni hulifanya, ni kulinganisha biashara zao na wafanyabiashara ambao tayari wameshakomaa. Kwanza kujilinganisha tu ni kosa, ila sasa kujilinganisha na wale ambao tayari wameshakomaa, ni kosa kubwa zaidi.
Hii ni kwa sababu biashara mpya na biashara iliyokomaa zinatofautiana sana. Wewe mwenye biashara mpya, huenda hata bado hujawa na wateja wa uhakika. Wakati mwenzako ambaye ana biashara iliyokomaa, anaweza kuwa tayari ana kiwango fulani cha wateja wa kuaminika.
SOMA; BIASHARA LEO; Kuwa Makini Unapoingia Kwenye Biashara Mpya, Hata Kama Umeshazoea Biashara…
Hivyo yale unayopaswa kufanya wewe, siyo sawa na wale ambao tayari wapo kwenye biashara. Hata mitindo yenu ya maisha, haiwezi kufanana hata kidogo. Wewe unaweza kuwa unavaa kofia nyingi kwa wakati mmoja, wakati mwenzako ana wasaidizi kwenye baadhi ya maeneo, hivyo anavaa kofia chache kwa wakati mmoja.
Unapokuwa mgeni kwenye biashara, unahitaji kujua kwamba pamoja na ushauri mzuri unaopata kutoka kwa wengine, pamoja na namna unavyoona wengine wakiongoza biashara zao, bado wewe una jukumu la kuhakikisha biashara yako inasimama. Hivyo kuna wakati utahitajika kufanya mambo ambayo hujawahi kufundishwa au kuwaona wengine wakifanya, na hayo ni muhimu ili biashara yako iweze kupona.
Kuna mengi kuhusu biashara ambayo hutayaona kwa wale ambao tayari biashara zao zimeshasimama na wala washauri wa biashara hawatakumbuka kukueleza hayo. Hayo unajifunza kadiri biashara yako inavyoenda na kutokana na kila hatua unayopiga.
Usiache kuchukua hatua kwa sababu hujaona wengine wakichukua hatua hiyo, au kwa kuwa hujaona mtu akishauri hilo. Kama ni muhimu, halali na linahitajika ili biashara ivuke changamoto, fanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog