Habari za leo rafiki yangu,

Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo ambapo tumepata nafasi ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana. Kama ambavyo nimekuwa nakuambia kila wakati, MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA, wewe mwenyewe ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kwenye maisha yako ya mafanikio.

Leo nakwenda kuongea moja kwa moja na vijana wanaotafuta ajira na pia waajiriwa wote ambao kazi zao zimewachosha. Pia barua hii itakuwa na nakala kwa wale waliojiajiri lakini wanaona kama mambo hayaendi hivi.

Tukianza na hali ya mambo ilivyo;

Juma hili kumekuwa na habari iliyoshika hisia za wengi sana, ilikuwa kuhusu usaili wa kazi uliofanywa na TRA, ambapo zilitangazwa nafasi za kazi 400, lakini walioomba walikuwa zaidi ya watu elfu 50. Lililowasumbua watu zaidi ni kitendo cha watu elfu 30 kuitwa kwenye usaili. Na kilichosumbua zaidi na zaidi ni aina ya usaili uliofanyika, palikuwepo na mtihani ambao ni mgumu mno.

Watu wamelalamikia sana hili kila kona, cha kushangaza ni kwamba wananchi wanalalamika, wanaoomba ajira wanalalamika na hata viongozi nao wanalalamika. Hii inapelekea kila mtu kuongea lake la moyoni lakini hakuna suluhisho la kudumu linalozalishwa, zaidi ya kila mtu kuendelea na mambo yake.

FB_IMG_15041092544925818
Watu waliokwenda kufanya usaili wa kazi TRA, ambapo watu elfu 30 walikuwa wakiomba kupata nafasi 400

Tatizo la ajira ni kubwa nchi hii, wala hatuhitaji kuona watu wengi kwenye usaili ndiyo tushtuke kwamba mambo siyo mazuri. Ni kitu ambacho kipo wazi, kwa sababu wahitimu wamekuwa wanazalishwa kila mwaka ila nafasi za ajira haziongezeki sawa sawa na ongezeko la wahitimu.

Tatizo linazidi kuwa kubwa kutokana na mfumo wetu wa elimu na matarajio ya kijamii. Mtu mpaka anahitimu, anatumia zaidi ya miaka 16 darasani, na miaka yote hiyo anafundishwa kuhusu kuajiriwa, tena anafundishwa na watu alioajiriwa. Akirudi kwenye jamii, jamii inamfanya aone kama hajaajiriwa basi maisha yake bado hayajawa na maana.

Tatizo linapamba moto zaidi kutokana kukosa watu wa mfano katika nafasi za uongozi. Kila mtu analalamika kwamba viongozi wameshindwa kuzalisha ajira, au viongozi wameshindwa kutengeneza mazingira mazuri ya watu kujiajiri. Lakini hebu tuangalie vizuri hao viongozi, je ni wangapi kati ya hao ambao walishafanikiwa kujiajiri kwa mafanikio? Ukiangalia viongozi wengi, wamekuwa wakihama kutoka ajira moja kwenda nyingine. Labda alikuwa mfanyakazi wa serikali, akatoka na kwenda kugombea ubunge akachaguliwa kuwa waziri au nafasi nyingine yoyote. Au alikuwa mfanyakazi wa serikali, akapandishwa cheo na kuwa katibu au nafasi nyingine. Huyu ni mtu ambaye ameishi maisha yake yote kwenye ajira na hivyo kumpelekea lawama kwamba kwa nini hatengenezi ajira au hawezeshi watu kujiajiri, ni kujisumbua, maana hilo kwake mwenyewe ni tatizo.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Wahitimu Ambao Bado Wanatafuta Ajira.(Kama Bado Unazunguka Na Bahasha Soma Hapa)

Hivyo basi, katika kuondokana na hali hii ya malalamiko na kukata tamaa, nimeandika barua hii kwa watu wa aina tatu, ambao nina maneno machache nataka kusema na ninyi.

Kwa vijana ambao wanatafuta ajira lakini hawapati.

Kwanza nianze kwa kuwapa pole kwa changamoto hiyo kubwa. Ni wakati mgumu sana kwenye maisha ya mtu. Hasa pale mategemeo yako makubwa yanapobadilika na kuona kama ulidanganywa, ulitegemea ukihitimu masomo upate ajira nzuri kama ambavyo ulikuwa unaahidiwa. Huenda pia umekuwa unaona wengine wachache waliosoma ulichosoma wewe, ambao wana ajira nzuri na maisha mazuri pia.

Karibu kwenye maisha ya uhalisia, maisha ambayo hayatabiriki kama maisha ya shule yalivyokuwa. Haya ni maisha halisi, ambapo nafasi za ajira ni chache kuliko wenye uhitaji.

Sasa hapa sitaki nikuchoshe na mambo ambayo tayari unayajua, bali nataka nikuambie mambo haya mawili;

Moja; kama ndiyo umemaliza masomo siku za karibuni, ndani ya mwaka mmoja au miwili na unatafuta ajira, usiyasimamishe maisha yako. Namaanisha kwamba usisimamishe kila kitu mpaka upate ajira.

Kwa sababu wengi huona kama maisha hayajaanza mpaka pale watakapokuwa wamepata ajira. Hivyo huacha muda uende huku wakijaribu kuomba sehemu mbalimbali ajira.

Ninachokushauri hapa, wakati unaendelea kutafuta ajira, endelea kujishughulisha. Endelea kufanya shughuli ndogo ndogo ambazo zinaweza kuongeza thamani kwa wengine, ambazo unaweza kuanza kufanya hata bure, lakini baadaye ukapata nafasi ya kulipwa kupitia hicho unachofanya.

Anza na elimu uliyoipata, mazingira yanayokuzunguka na mambo unayopendelea kufanya. Hapo angalia ni vitu gani unaweza kuwasaidia wengine na wao wakawa tayari kukulipa hata kama ni kidogo.

Kama unaweza kupata sehemu ya kujitolea kufanya kazi, fanya hivyo.

Wito wangu kwako ni kwamba, kama bado huna kazi, basi usianze kuchagua kipi kinakufaa kufanya na kipi hakikufai. Fanya kila unachoweza kufanya, usianze kujiwekea vigezo kwa sababu ya elimu uliyopata, muhimu ni ufanye vitu vyenye kuongeza thamani kwa wengine, na dunia itakulipa. Kwa sababu ni sheria ya asili kwamba thamani lazima ilipwe.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Vijana Wanaotafuta Ajira. Soma Hapa Uone Fursa Unazoweza Kutumia.

Mbili; kwa wale ambao wamehitimu masomo na wamekuwa wanatafuta ajira kwa zaidi ya miaka miwili bila ya mafanikio, basi nawashauri kufanya maamuzi mengine muhimu ya maisha yao. Kama kwa miaka zaidi ya miwili mfululizo unazunguka na bahasha kuomba kazi, kama kila usaili umehudhuria na kadiri muda unavyokwenda unaona usaili unaohudhuria una watu wengi zaidi, ni wakati wa kukaa chini, kujitafakari na kuchukua hatua kubwa.

Hapa sasa unahitaji kuchagua kuacha kuweka nguvu zako zote kupata ajira na uanze kuweka nguvu zako katika kutengeneza thamani zaidi kwa wengine. Hapa unahitaji kuchagua kitu ambacho unaweza kukifanya vizuri kwa wengine na weka nguvu na akili zako zote pale kuhakikisha unatengeneza thamani kubwa kwa wengine.

Iwe utachagua kujiajiri kwa kutoa huduma mbalimbali, au utachagua kuanza na biashara ndogo, angalia wapi unaanzia na kuwa na ndoto kubwa ambayo unaifanyia kazi kila siku. Ni lazima uchukue maamuzi haya kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda ndivyo nafasi ya wewe kupata ajira inavyozidi kuwa ngumu kutokana na wingi wa wanaohitaji ajira.

Kwa walioajiriwa lakini hawafurahii ajira zao.

Kabla ya kuajiriwa, watu huwa na mategemeo makubwa sana. Huamini kwamba wakishaajiriwa basi kila kitu kitakwenda vizuri. Maisha yatakuwa bora na shida ndogo ndogo ndiyo zimeisha.

Ni mpaka pale mtu anapoingia kwenye ajira ndipo anauona ukweli kwa macho yake. Kipato hakitoshelezi ukilinganisha na gharama za maisha, kazi inakuwa na changamoto na wafanyakazi wengine nao ni changamoto kwake. Hapa mtu anaingia kwenye madeni na ndiyo anakuwa amejiweka kwenye kifungo kikubwa cha maisha yake.

Kama upo kwenye hali hiyo, ya ajira kukuchosha na maisha kuzidi kuwa magumu, usikazane kutafuta ajira nyingine, badala yake kazana kununua uhuru wa maisha yako.

Uhuru pekee unaohitaji kwenye maisha yako ni kufanya kile unachopenda na kuwa na uhuru wa kifedha. Vyote hivi unaweza kuvitengeneza kwa kuamua kuchukua hatua sasa. Endelea na kazi hiyo kwa muda, kwa sababu una maisha yanahitaji kuendelea, hivyo kipato hata kama ni kidogo, kitakusaidia kwa sasa.

Unachohitaji kufanya ni kuchagua kitu cha kufanya nje ya ajira yako. Anza kutoa huduma ambazo watu wanaweza kukulipa hata kwa baadaye. Anza kwa biashara ambayo ni ndogo kabisa na weka juhudi na muda kuikuza mpaka ifanikiwe.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Wafanyakazi Wote, Mambo Matatu (03) Muhimu Unayohitaji Kufanya Unapokwenda Kuadhimisha Siku Ya Wafanyakazi Duniani.

Ninachotaka kukusisitiza hapa ni kwamba, popote ulipo sasa, hakuna aliyekufungia hapo. Unaweza kuondoka hapo ulipo, kama utaamua wewe mwenyewe. Lakini kama hutaamua, utaendelea kuwa hapo, miaka itaendelea kwenda na unakuja kustuka muda umekwenda sana na huoni tena ufanye nini.

Angalia hatua unayoweza kuchukua na anza kuichukua, usiishi kwa mazoea kama wengi wanavyoishi, badala yake jua maisha yako unataka yaende wapi na chukua hatua.

fb instagram

Kwa wale waliojiajiri na mambo ni magumu.

Kwanza kabisa nikupe ukweli kama ulivyo, haijalishi watu wanatukuza kujiajiri kiasi gani, siyo rahisi kama wengi wanavyofikiri. Hivi wewe unafikiri kwa nini hata wengi wanaowafundisha wengine kujiajiri nao wameajiriwa? Kujiajiri au kufanya biashara ni kitu kigumu mno duniani.

Kuna changamoto za kila aina, mambo hayaendi kama ulivyopanga na hakuna jambo lolote unaloweza kuwa na uhakika nalo. Unaweza kuweka mipango yako mikubwa na mizuri, lakini unachopata ni tofauti kabisa na matarajio yako.

Unapochagua kujiajiri kwanza acha kabisa kujaribu, kama unajiajiri kwa kujaribu, jaribio lako litashindwa, tena litashindwa vibaya mno. Kwa sababu changamoto ni nyingi na zitakukimbiza.

Hivyo fanya maamuzi kwamba umeamua kujiajiri au kuingia kwenye biashara, na hakuna chochote kitakachokuondoa kwenye maamuzi hayo.

Baada ya maamuzi haya, angalia eneo hili muhimu sana ambalo ni fedha. Tofauti ya kuajiriwa na kujiajiri ni kwamba kwenye kuajiriwa, mshahara hata kama ni kidogo, una uhakika kila mwisho wa mwezi utaupata. Lakini kwenye kujiajiri hakuna uhakika wa aina hiyo. Mwezi mmoja unaweza kupata kiasi kikubwa cha fedha mpaka ukajiona utakuwa bilionea siku si nyingi, mwezi unaofuata usipate fedha kabia, unaufuata ukapoteza fedha nyingi. Huo ndiyo uhalisia na kama hujaujua, utapata taharuki na kuona kama mambo hayaendi.

SOMA; USHAURI; Mambo Ya Kuzingatia Kabla Ya Kuacha Ajira Na Kuingia Kwenye Ujasiriamali.

Kwenye kujiajiri kipato kinapanda na kushuka kulingana na mambo yanavyokwenda. Hivyo lazima eneo la fedha ulipangilie vizuri na uwe na nidhamu ya hali ya juu linapokuja swala la fedha. Zijue gharama zako za maisha kwa mwezi, kisha hakikisha una akiba ya kuendesha maisha yako angalau miezi sita ijayo. Hili litakufanya wewe uwe mtulivu na kufanya kazi zako vizuri. Kwa kukosa hali hii utashindwa kutulia kwa sababu hujui hela ya kula kesho au mwezi ujao inatoka wapi.

Eneo la pili la kuzingatia ni ufanyaji wako wa kazi. Unapokuwa kwenye ajira, unasukumwa kufanya kazi. Hata kama hutaki, utalazimika kufanya la sivyo utapewa barua za onyo na hata kufukuzwa kazi. Lakini kwenye kujiajiri hakuna wa kukusukuma, ufanye usifanye hakuna anayehangaika na wewe. Sasa sisi binadamu kwa asili ni wavivu, hatupendi kuumia, tunapenda kufanya vitu rahisi, tunapenda starehe, tunapenda kulala mpaka tutosheke.

Ili ufanikiwe kwenye kujiajiri na biashara, lazima uende kinyume na asili yako. Lazima ujisukume kufanya kazi hata kama mwili hautaki, lazima ujinyime usingizi, lazima ujinyime starehe. Unahitaji kutenga kipindi cha muda ambacho utafanya kazi zaidi ya mtumwa. Hutakuwa na mapumziko makubwa wala mapumziko ya mwisho wa wiki kwako hayatakuwepo. Huo ni wakati wa kujenga msingi wako wa kujiajiri, ambao utakuwezesha kujitengeneza wewe kwenye eneo lako na kuweza kupata wateja unaowahitaji.

Hii safari siyo rahisi, imewashinda wengi, mpaka maprofesa wenye elimu kubwa, wengi wanakazana kujaribu na wanashindwa. Na wapo ambao wanaenda tu wasijue wanaelekea wapi na nini hasa wanataka. Wewe kuwa tofauti, jitoe kweli, weka juhudi na jenga nidhamu kubwa sana kwenye fedha, muda na ufanyaji wako wa kazi.

Ninachokuambia rafiki, popote ulipo sasa, iwe huna ajira, iwe una ajira lakini haikuridhishi au iwe umejiajiri lakini mambo hayaendi kama ulivyotegemea, jua wapi unapotaka kwenda na weka juhudi. Mambo siyo rahisi, lakini yanawezekana. Chukua hatua zaidi ya wengine, na jijengee nidhamu ya hali ya juu sana. Toa thamani kubwa kwa wengine na utalipwa sawasawa na thamani unayozalisha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

fb instagram

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.