For many men, the acquisition of wealth does not end their troubles, it only changes them. – Lucius Annaeus Seneca

Asubuhi mpya ya siku mpya ni nafasi mpya kwetu kwenda kuishi kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.
Bila ya kisahau KUTATUA, KUAMUA NA KUONGOZA ili kuweza kifanya makubwa sana kwenye siku hii ya kipekee ya leo.

Asubuhi ya leo tutafakari FEDHA HAIMALIZI MATATIZO, INAYABADILI…
Hakuna kitu kinachowaletea watu mvurugano wa ndani kama fedha.
Hii ni kwa sababu mtu akiwa hana fedha, anaamini akishazipata basi hatakuwa na matatizo tena, ataishi namna anavyotaka na kufanya kile anachotaka kwa wakati anaotaka.
Ni mpaka mtu anapopata fedha ndipo anagundua kwamba sasa matatizo yake siyo ya kutokuwa na fedha, bali fedha zimekuja na matatizo mapya.

Mtu anajikuta ana fedha, lakini sasa hawezi kufanya kile anachotaka kwa namna anavyotaka.
Anajikuta kadiri fedha zinavyokuwa nyingi, ndivyo pia anavyozidi kuhitajika na hata majukumu yake yanakuwa mengi zaidi.
Kama alifikiri akishakuwa na fedha hatahitaji tena kufanya kazi, anajikuta kwa kuwa na fedha anahitajika kufanya kazi zaidi na zaidi.

Ukweli ni kwamba, hakuna kiwango chochote cha fedha ambacho kitamaliza na kufuta kabisa matatizo yake.
Badala yake fedha inakuja na matatizo yake, fedha inayabadili matatizo uliyonayo.
Na kadiri fedha zinapokuwa nyingi, ndivyo matatizo mapya yanakuwa makubwa.

Tafakari hili kwa kina na kama umewahi kuwa na ndoto kwamba siku ukifikia kiwango kikubwa cha fedha matatizo yako yote yatafutika, achana na ndoto hizi na angalia uhalisia.

Sikuambii hili ilo uachane na kutafuta fedha, badala yake nataka ujiandae, uwe unajua kabisa kwamba kupata fedha hakufuti matatizo yako yote, badala yake kunakuja na matatizo mapya.

Kama umewahi kusikia watu wakisema fedha hainunui furaha, hao ndiyo wale waliofikiri kupata fedha nyingi kutafuta matatizo yao yote.
Fedha ni fedha, na kadiri unavyokuwa nazo nyingi, matatizo yanakuwa mapya.
Jiandae kwa ajili ya matatizo mapya yanayokuja na fedha.
Usijidanganye kwamba ukishakuwa nazo basi kila kitu kitakuwa mteremko, kuna mambo yatakuwa magumu kwako ukiwa na fedha nyingi kuliko ukiwa huna fedha.

Tukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha