Meli inakuwa salama sana inapokuwa imetia nanga bandarini, ndege inakuwa salama kabisa ikiwa imetua kwenye uwanja wa ndege. Ni mpaka pale meli inapotoa nanga na kuanza kuelea, au ndege inaondoka uwanjani na kuanza kupaa ndipo hatari zinaweza kujitokeza. Kwa meli kukubwa na dhoruba na kuzama au ndege kukutana na hali mbaya ya hewa na hata kupelekea kuanguka.
Pamoja na kwamba meli ipo salama bandarini na ndege ipo salama uwanjani, hayo siyo matumizi yake. Meli haikutengenezwa ikae bandarini muda wote, wala ndege haikutengenezwa itue uwanjani wakati wote. Vifaa hivyo vilitengenezwa ili kusafiri na katika kusafiri huko, kuna hatari zake.

Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu ya kila siku.
Usifanye kitu chochote, hakuna anayehangaika na wewe, hakuna wa kukukosoa wala kukuambia utashindwa.
Fanya mambo yako kwa kawaida, kwa mazoea, kama ambavyo kila mtu anafanya na hakuna atakayehangaika na wewe, kila mtu atakuwa anaendelea na mazoea yake na wewe utakuwa mwenzao, huna madhara wala usumbufu wowote.
Lakini pale utakapojaribu kufanya makubwa, pale utakapoanza kufanya kwa utofauti, pale utakapoanza kuweka juhudi kubwa sana na kuwa na maono makubwa, hapo ndipo utakapomwamsha kila mtu. Hapo ndipo utakapokaribisha kila aina ya maoni, kila aina ya ukosoaji na ukatishwaji tamaa.
SOMA; UKURASA WA 999; Unapoukaribia Ukweli, Hofu Inaongezeka…
Utashangaa hata watu ambao hawajawahi kukushauri lolote kuhusu ufanye nini au ufanye vipi, watakuwa wa kwanza kukuambia kwamba unakosea, au utashindwa au huwezi. Utashangaa kila mtu ana kitu cha kukuambia, na wengi siyo kitu chanya bali hasi.
Hivyo upo salama kama hutafanya makubwa, kama utaendelea kufanya kwa mazoea. Lakini sasa, hukuja hapa duniani kutokufanya chochote, hukuja hapa duniani kufanya kwa mazoea au kufanya kama ambavyo kila mtu anafanya.
Umekuja hapa duniani kuacha alama, kuleta tofauti. Ndani yako una kitu ambacho hakuna mwingine ambaye anacho. Kama utataka kuwa salama, kwa kufanya kwa mazoea hutaweza kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako, na hivyo kuishia kuwa kawaida na kutokufanikiwa.
Ni rahisi kuepuka kukosolewa, lakini hilo siyo lengo kuu la maisha yako. Piga hatua kubwa kwenye maisha yako, kuwa tayari kukosolewa, kuwa tayari kukatishwa tamaa, lakini jua utaweza kupiga hatua kubwa sana kama utakuwa tayari kukosolewa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Asante sana kwa ujumbe huu, ili mradi naishi hakuna usalama lazima nikabiriane na kila kitu. Asante
LikeLike
Vizuri.
LikeLike
Ahsante sana SANA kocha,
Hakika hakuna atakae hangaika na wewe mpaka utakapo amua kufanya tofauti na wengine.
LikeLike
Hakika
LikeLike