Kwenye jambo lolote lile, iwe ni kazi, biashara na hata mahusiano, uaminifu na gharama zina uhusiano unaokwenda kwa utofauti. Yaani pale uaminifu unapokuwa mkubwa, basi gharama inakuwa ndogo na mambo yanakwenda haraka. Lakini uaminifu ukiwa mdogo, gharama zinakuwa kubwa na jambo linachukua muda sana kufikiwa maamuzi.

Dunia ya Sasa

Angalia hili na utaliona kila mahali, kwamba kama uaminifu ni mkubwa, hakuna haja ya kuanza kuchunguza, kuangalia kama ni kweli na mambo mengine. Makubaliano yanafikiwa haraka na kila mtu ananufaika.

Lakini uaminifu ukiwa mdogo, kila mtu anakuwa na wasiwasi, inahitajika kuchunguza na kujiridhisha kama ni kweli, hilo linaongeza gharama na kuchelewa kufikia maamuzi.

SOMA; UKURASA WA 1057; Mkataba Hautakulinda, Uchaguzi Wa Watu Ndiyo Utakulinda…

Hivyo kwa chochote unachofanya, kazana sana kujijengea uaminifu na wale unaojihusisha nao. Hakikisha hufanyi chochote ambacho kinawapa watu wasiwasi juu ya uaminifu wako. Kazana kuwa mwaminifu wa hali ya juu. Fanya neno lako kuwa sheria, hata kama itakugharimu wewe.

Kadiri watu wanavyokuamini, ndivyo inavyokuwa rahisi kwao kukupa kile unachotaka na kufikia maamuzi haraka.

Lakini ukishakuwa na chembechembe ambazo zinatia mashaka uaminifu wako. Ukishakuwa mtu ambaye unasema vitu ambavyo siyo kweli, unaahidi vitu ambavyo hutekelezi na unatafuta njia ya kunufaika zaidi ya wengine, unajiweka kwenye mazingira magumu ya kupata chochote unachotaka.

Jenga uaminifu wako, utapunguza gharama na kurahisisha maamuzi yoyote unayotaka yafikiwe na wengine kuhusu wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog