Habari kubwa katika kipindi hichi kwa upande wa fedha na uwekezaji ni cryptocurrency au kama inavyofahamika kwa Kiswahili fedha za kidijitali. Aina hii ya fedha imewavutia wengi siyo kwa sababu ya matumizi yake, bali kwa jinsi thamani yake inavyokua kwa kasi na hivyo wengi kuona ni sehemu rahisi ya kupata fedha nyingi bila ya kufanya kazi.

Lakini wengi ninaowaona wanakimbizana na fedha hizi za kidijitali, hawana uelewa wa kutosha. Wengi wanadanganywa na kushawishiwa kuingia kwenye kitu ambacho hawakielewi kwa matumaini kwamba watapata fedha nyingi. Ni kweli wapo watakaopata fedha nyingi, na pia wapo ambao watapoteza fedha nyingi kwenye aina hii ya uwekezaji.

Hivyo leo nimechukua muda, kukuandikia wewe rafiki yangu makala hii yenye kila unachopaswa kujua kuhusu cryptocurrency kwa ujumla, na tukiangalia kwa kina zaidi bitcoin ambayo ndiyo currency ya kwanza na yenye thamani kubwa zaidi. Nitachambua hili kwa lugha rahisi ambayo hata kama huna elimu kubwa utaweza kuelewa na kuweza kuchukua hatua.

Lakini kabla sijaingia kwenye kueleza kwa kina fedha hizi za kidijitali, naomba nikushirikishe hadithi tatu muhimu ambazo zitatupa mwanga wa nini kinaendelea.

Moja; TULIP MANIA 1630 – 1637.

Mnamo karne ya 17, kwenye Jamhuri ya Udachi (Dutch Republic), kulitokea hali ambayo haikuwa ya kawaida. Maua yanayojulikana kwa jina la Tulip yalianza kupata umaarufu ghafla. Maua haya yalikuwa na mwonekano mzuri na pia yalikuwa yana changamoto kwenye ulimwaji wake. Hivyo hili lilifanya watu wayathamini sana, na hili likapelekea bei yake kuwa juu. Kadiri bei ilivyokuwa inapanda, ndivyo wengi zaidi waliyataka maua hayo na bei kuzidi kupanda zaidi.

Ilifika wakati, thamani ya ua moja ikawa zaidi ya mara kumi ya kipato cha mwaka cha mfanyakazi wa kawaida kwenye nchi hiyo. Kutokana na kupanda huku thamani kwa maua aina ya Tulip, jamii nzima ilianza kuhamia kwenye maua hayo, ikafika wakati maua haya yakawa yanatumiwa kama fedha, badala ya dhahabu ambayo imekuwa inatumika wakati wote.

Ilifika hatua, watu wakawa wanalipia maua hayo hata kabla hayajakomaa, yaani yakiwa bado shambani. Kufikia Februari mwaka 1637 maua haya ya Tulip yalifikia bei ya juu kabisa na ghafla bei ikaanza kuporomoka. Bei iliporomoka kwa kasi kiasi cha kuyumbisha uchumi wa nchi nzima na watu wengi kupata hasara kubwa. Hii inasemekana kuwa anguko la kwanza la kiuchumi duniani.

tulip mania, dot com, bitcoin

Mbili; DOTCOM MANIA 1997 – 2001.

Mwishoni mwa miaka ya 1980 jambo kubwa lilitokea duniani ambalo ni matumizi ya mtandao wa intaneti kwa watu wa kawaida. Mwanzoni mwa miaka ya 1990 matumizi ya mtandao wa intaneti yalishika kasi na biashara nyingi zinazohusisha intaneti zilianzishwa.

Kwa kuwa intaneti ilikuwa kitu kipya, na ambacho kilionesha kuwa na nguvu kubwa, watu wengi walivutiwa na biashara zinazohusisha mtandao wa intaneti. Hivyo watu wengi walikimbilia kuanzisha biashara zinazohusisha intaneti. Inasemekana kwamba mwishoni mwa miaka ya 1990 na kuelekea mwaka 2000 watu wengi walikuwa wakiahidi kuanzisha kampuni zitakazokuwa kubwa na watu wakashawishika kuwekeza fedha zao bila hata ya kuwepo kwa ushahidi au uhakika wowote kwamba biashara inayokwenda kuanzishwa itakuwa imara kweli.

Watu waliingiwa na tamaa ya kufaidika haraka kupitia intaneti, kitu ambacho kilipelekea makampuni mengi kuwa na thamani kubwa kuliko uhalisia. Kilichotokea ni uchumi mzima unaohusisha mtandao wa intaneti kuanguka, makampuni mengi kutangaza hasara na watu wengi kupoteza fedha zao.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Winning The Loser’s Game (Mbinu Zisizopitwa Na Wakati Za Kufanikiwa Kwenye Uwekezaji).

Tatu; CRYPTO MANIA 2009 – …….

Mwaka 2009, Satoshi Nakamoto, haijulikani kama ni mtu, kikundi cha watu au taasisi, alikuja na wazo la tofauti kwenye mfumo wa fedha. Kama ambavyo wote tunajua, mzunguko wa fedha umekuwa unadhibitiwa na benki kuu ya nchi husika. Kwa mfano mzunguko wa shilingi ya Tanzania, unadhibitiwa na Benki Kuu ya Tanzania. Hivyo miamala yoyote ya kifedha lazima iweze kufuatiliwa na benki kuu. Satoshi ali/walipendekeza mfumo wa kuondoa udhibiti huo. Badala ya mzunguko wa fedha kudhibitiwa na mtu mwingine, udhibitiwe na watu wawili tu, anayelipa na anayelipwa.

Mfumo huu ulionekana ni mkombozi kwa matatizo mengi ya kifedha, ambayo yapo wazi, mfano nchi kuchapa fedha na hivyo mfumuko wa bei kuwa mkubwa, gharama za kufanya miamala na hata usalama kuwa mdogo, kama ambavyo tumekuwa tunasikia fedha feki kuwepo kwenye mzunguko. Mfumo wa Satoshi ulionekana ni bora kabisa, lakini wengi wakawa na wasiwasi kwamba ni mgumu kueleweka na kutumika.

Hivyo mwaka 2009 Satoshi ali/walikuja na mfumo wa fedha ya kidijitali uliokwenda kwa jina la Bitcoin. Hii ilikuwa sarafu ya kwanza kabisa ya kidijitali, ambayo ilikuwa na lengo la kurudisha udhibiti na usalama wa fedha kwa watumiaji.

Kwa kipindi cha mwaka 2009 thamani ya bitcoin moja ilikuwa dola 0.0001 ambayo kwa kipindi hicho, dola moja ilikuwa tsh 1330, hivyo bitcoin moja ilikuwa sawa na tsh 1 na senti 33. Mpaka kufika mwaka 2010, bado thamani ya bitcoin moja ilikuwa chini ya dola moja. Kuanzia mwaka 2011 bei ya bitcoin imekuwa inaongezeka kidogo kidogo, kutoka dola mia na kuendelea. Mpaka kufika januari 2017, bei ya bitcoin moja ilikuwa chini ya dola elfu moja. Lakini baada ya hapo bei ilianza kuongezeka kwa kasi, kufika oktoba 2017, bei ya bitcoin moja ilikuwa dola elfu 5.

bitcoin june 2009

Tarehe 17 mwezi disemba 2017 ndiyo ilikuwa siku ambayo thamani ya bitcoin ilikuwa juu sana, ambapo bitcoin moja ilikuwa sawa na dola elfu 19. Yaani sawa na zaidi ya shilingi milioni 40. Hebu fikiria hapo, kwamba kama mwaka 2009, ungepata nafasi ya kununua bitcoin moja kwa shilingi moja, mwaka 2017 ungekuwa na zaidi ya milioni 40!

Kwa nini hadithi hizi tatu?

Hadithi hizi tatu zinatufundisha kitu kimoja muhimu sana kwenye fedha na uwekezaji, kwamba mara nyingi tamaa ya watu ikishaingia kwenye kitu, thamani inapanda kuliko uhalisia, kitu ambacho kinatengeneza anguko baadaye. Ilitokea kwa maua ya Tulip, ilitokea kwa biashara za Dotcom na itatokea kwenye cryptocurrency kama ambavyo nitakueleza hapo chini.

Ili tuweze kuweza kuelewana vizuri, na kwa kuwa yapo mengi ya kujifunza kuhusu fedha hizi za kidijitali, tutakwenda kwa mfumo wa maswali na majibu.

Swali; bitcoin ni nini?

Jibu; bitcoin ni mfumo wa malipo wa kielektroniki ambao ni wa moja kwa moja kati ya mlipwaji na mlipaji bila ya kuhusisha upande wa tatu kama benki serikali na taasisi nyingine za kifedha.

Swali; mfumo huu unafanyaje kazi?

Jibu; kunakuwa na sarafu za kidijitali, ambazo zina idadi yanye ukomo. Sarafu hizi ndiyo zinazotumika kama thamani ya malipo. mfumo mzima ni wa kielektroniki na hivyo hakuna sarafu yoyote ya kawaida inayohusika. Badala yake mfumo wa kompyuta unaotoa na kudhibiti sarafu hizi ndiyo unaotumika.

Swali; zipi faida na ubora wa mfumo huu mpya wa malipo?

Mfumo wa kawaida wa fedha una changamoto nyingi ambazo tumekuwa tunaziona kila wakati. Sehemu kubwa ya changamoto hizo inaweza kutatiliwa na mfumo huu wa fedha za kidijitali.

Changamoto ya mfumuko wa bei ambayo imekuwa inasababishwa na serikali kuchapa fedha na hivyo kushusha thamani, unadhibitiwa na uwepo wa kiwango kamili cha sarafu za kidijitali. Kwa mfano kwa Bitcoin kuna sarafu 21,000,000 pekee, zikiisha hizo hakuna nyingine zinazoweza kuzalishwa na hivyo mfumuko wa bei hauwezi kutokea.

Changamoto ya usiri imetatuliwa na mfumo huu mpya kwa kufanya muamala kuwa baina ya watu wawili pekee. Katika mfumo wa kawaida, utamlipa mtu kwa njia ya benki, fedha taslimu au njia za mitandao, ambazo zote hazina usiri.

Changamoto ya gharama za miamala imeondolewa sana na mfumo huu, kwa mfumo wa kawaida, kila unapohamisha fedha eneo moja kwenda eneo jingine unakatwa malipo, na hii ni kwa sababu taasisi nyingi zinahusika. Lakini kwenye mfumo huu, hakuna uhusishaji wa taasisi nyingi, hivyo makato hakuna.

Changamoto ya usalama, tunajua namna ambavyo kuwa na kiasi kikubwa cha fedha ni hatari, pia hata benki siyo salama sana kuweka fedha. Kwa mfumo huu wa fedha wa kidijitali, usalama ni mkubwa, program ya kompyuta inayotumika kudhibiti mfumo huu ni dhabiti sana na haiwezi kuchezewa.

Changamoto ya fedha feki imedhibitiwa na mfumo huu. Kwa kila aina ya sarafu, kwenye mzunguko huwa kunakuwa na fedha feki nyingi. Lakini kwa mfumo huu wa fedha za kidijitali, hakuna namna ya kutengeneza sarafu feki.

Swali; je kuna sarafu za aina ngapi kwenye fedha hizi za kidijitali?

Jibu; Watu wengi wanajua zile sarafu kubwa za kidijitali kama Bitcoin, Ethereum, Ripple, Bitcoin Cash, Cardano, na Litecoin. Lakini mpaka kufika mwezi february 2018 kulikuwa na sarafu za kidijitali zaidi ya 1400, na orodha inaendelea kukua kila siku, kwa sababu yeyote anaweza kuja na sarafu mpya.

Swali; je cryptocurrency utakuwa mfumo kamili wa malipo?

Jibu ni ndiyo, lakini siyo sasa ni kwa baadaye. Lakini pia kama utakuwa mfumo mkuu wa malipo, basi kila serikali itatengeneza mfumo wake wa malipo kwa njia hiyo ya kidijitali. Hakuna serikali inayoweza kukubali kupoteza udhibiti wa fedha, kitu pekee kinafanya serikali ziwepo, tangu enzi za utawala wa roma, ni udhibiti wa fedha, na enzi hizo, dhahabu.

Swali; je Bitcoin itakuja kuwa sarafu ya dunia na kutumiwa na kila mtu?

Jibu ni hapana, Bitcoin imekosa sifa zote za sarafu ya kutumiwa na uma, kwa sababu thamani yake haijatulia, inapanda na kushuka kwa kasi mno. Pia watu wengi wameshaihodhi na hivyo uwezekano wa kutumiwa na kila mtu ni mdogo.

Swali; je soko zima la fedha hizi za kidijitali litaanguka?

Hapa ndipo muhimu sana unapaswa kuelewa. Kwa hizi sarafu nyingi, ukiangalia zilianza na thamani kidogo sana. mfano bitcoin kwa mwaka 2009 na 2010 thamani yake ilikuwa chini ya dola moja. Lakini baada ya watu kuisikia ilianza kupanda thamani na kufikia disemba 2017 ilifikia thamani ya juu kabisa ya sarafu moja kuwa dola elfu 19. Lakini baada ya hapo imekuwa unashuka na kupanda.

Ukuaji huu wa thamani ya sarafu hizi za kidijitali siyo wa kawaida, na unachochewa na tamaa ya watu kuona ni njia ya haraka ya kutengeneza utajiri. Tamaa hii itapelekea sarafu nyingi kuanguka na baada ya hapo zitasimama sarafu imara na ambazo thamani yake inaendana na hali ya uchumi.

Kama ambavyo TULIP ilianguka, na kama DOTCOM ilivyoanguka, CRYPTOCURRENCY pia itaanguka, lakini baada ya hapo zitaibuka sarafu ambazo ni imara na zenye thamani inayoendana na uchumi. Anguko la CRYPTOCURRENCY litawaumiza wengi sana na kuwanufaisha wachache.

ongezeko la thamani ya bitcoin kwa mwaka mmoja
Kwa kipindi cha mwaka mmoja kati ya machi 2017 mpaka mashi 2018, thamani ya bitcoin imeongezeka kutoka chini ya dola elfu moja mpaka dila elfu kumi na tisa. Ni ongezeko ambalo haliwezi kuelezewa vyovyote vile kiuchumi.

Swali; je kuna matumizi mengine ya teknolojia hii ukiacha malipo?

Teknolojia iliyopo nyuma ya sarafu hizi za kidijitali, ambayo ni BLOCKCHAIN ina matumizi mengine mengi na makubwa. Mfano inatumika kwenye kuandaa mikataba ya kidijitali, inatumika kwenye kutunza kumbukumbu za siri na kwenye usimamizi na udhibiti wa uwekezaji. Teknolojia ya blockchain inaweza kutumika kwenye kila eneo linalohitaji ufuatiliaji na udhibiti wa hali ya juu, kama kwenye afya, benki, makusanyo ya mapato na kadhalika.

SOMA; Tofauti Ya Fedha Kwenye Uwekezaji, Matumizi Na Kukopa.

Kwa nini BITCOIN siyo uwekezaji sahihi kwako kufanya kwa sasa?

Mpaka kufika hapa nina imani umeanza kupata picha ya hichi kitu kinachoitwa CRYPTOCURRENCY ni nini, kwamba ni mfumo wa malipo wa kidijitali ambao ni wa moja kwa moja na unaepuka changamoto nyingi za mfumo wa kawaida wa fedha. Pia utakuwa umejua BITCOIN ni moja kati ya sarafu zaidi ya elfu moja ambazo zinatumia mfumo huu. Kwa kipindi hichi BITCOIN ndiyo sarafu yenye thamani kubwa.

Sasa nimalize kwa kukuambia kwa nini BITCOIN siyo uwekezaji sahihi kwako kufanya kwa sasa.

Watu wengi wanahamasishwa sana kuwekeza kwa kununua bitcoin hasa pale ambapo thamani yake ilikuwa inapanda kwa kasi ya ajabu. Lakini wengi ambao wamekuwa wanatamani kuwekeza kwenye mfumo huu, hawapo tayari. Hapa nitataja makundi matano na kama upo kwenye moja ya makundi hayo usiwekeze kwenye cryptocurrency na bitcoin, badala yake endelea na uwekezaji wa kawaida ambao ni salama kidogo ukilinganisha na huu kwa sasa.

  1. Kama ndiyo umeielewa cryptocurrency na bitcoin leo, jipe muda wa kujifunza.

Nilichokushirikisha hapa kuhusu cryptocurrency na bitcoin ni kama tone tu la bahari ambayo unapaswa kuelewa kuhusu mfumo huu wa fedha na malipo. Hivyo kama umekuwa unasikia sikia kuhusu hizo bitcoin lakini leo ndiyo umeanza kupata picha basi huu siyo uwekezaji mzuri kwako kwa sasa.

Pendekezo langu ni chukua muda kusoma na kuelewa kwa kina, soma vitabu na siyo makala au kuwasikiliza watu wanaokuambia kwa nini ujiunge au usijiunge. Isome teknolojia hii uielewe kwa undani, kisha soma fedha, uchumi na uwekezaji ili kujua namna vitu hivi vinakwenda. Hapo utakuwa umepata mwanga wa kukusaidia kufanya maamuzi sahihi.

  1. Kama huwezi kumudu kupoteza fedha.

Pamoja na hatari ya cryptocurrency na bitcoin kwa sasa, bado ni kitu kizuri kujaribu, ila tu, ni rudie, ila tu unamudu kupoteza fedha. Yaani kama una fedha za ziada, ambazo hata ukizipoteza maisha yako hayatayumba, basi unaweza kujaribu aina hii ya uwekezaji.

Lakini kama bado hujafikia hatua ya kuwa na fedha za ziada, kama upo kwenye madeni na unafikiria aina hii ya uwekezaji itakutoa kimaisha, kaa mbali nayo, ni hatari kwako.

Na kama unawaza kwenda kukopa fedha uwekeze kwenye mfumo huu, huna tofauti na mtu anayevuta sigara huku anaweka petroli kwenye gari, siyo hatari kwako tu, bali na kwa wengine pia.

  1. Kama umri wako wa kuzalisha fedha umesogea.

Katika kila anguko la uchumi linalotokea duniani, watu wanaoathirika zaidi ni wale ambao umri wao umeenda na hawawezi tena kujitumikisha. Yaani kama umri umeenda, unakaribia kustaafu au umeshastaafu na una fedha zako za mafao, usiziweke kwenye mfumo huu wa fedha za kidijitali. Hata kama unaona kuna nafasi kubwa ya kuongeza kipato hicho, hatari unayochukua ni kubwa sana kwako, na nguvu za kupambana zimeshapungua.

  1. Kama elimu pekee uliyonayo ni ya kuambiwa.

Wapo watu ambao wanatoa elimu hizi za cryptocurrency na bitcoin, ila elimu wanayoitoa ni ya kuwaambia watu kwa nini wajiunge na kuwashawishi kwamba ni uwekezaji ambao hawapaswi kuukosa. Kama hii ndiyo elimu ambayo umekuwa unaipata pekee, hujawa tayari kuwekeza. Unahitaji kujifunza kwa kina, faida na hasara, usalama na hatari kwenye uwekezaji huu kabla hujachukua hatua.

NETWORK MARKETING

  1. Kama sababu pekee ya kuwekeza ni kwa sababu wengine wamekuambia ‘wanapiga hela’

Ipo sababu nyingine ambayo naona watu wanaitumia vibaya kuwekeza kwenye mfumo huu mpya wa fedha na malipo. Na sababu hiyo ni kwamba ona wengine wanapata hela. Na watu wanaonesha kweli wanapata fedha, na ni kweli siyo utani. Kama nilivyoeleza, hata pale sarafu hizi zitakapoanguka, wapo watakaonufaika na wapo watakaopoteza.

Sasa unapofikiria kupata tu, jua kwamba kuna kukosa pia. Hivyo ukiangalia wanaonufaika, usiache kuangalia uwezekano wa kukosa.

Rafiki, nimejaribu kukuelezea kwa lugha rahisi na inayoeleweka kuhusu mfumo huu mpya wa fedha za kidijitali, kama nilivyoeleza hii ni sehemu ndogo sana ya elimu kubwa unayopaswa kuwa nayo kama unataka kuwekeza kwenye mfumo huu. Wito wangu kwako ni uendelee kujifunza zaidi na kama una kiasi cha fedha unachoweza kupoteza, unaweza kujaribu kwenye aina hii ya uwekezaji, ukijua kwamba nafasi ya kupoteza ni kubwa kama ilivyo ya kunufaika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog