Sehemu ambapo akili zetu sisi binadamu zinashindwa kuelewa, ni pale tunapofanya kila tunachopaswa kufanya, lakini tunapata matokeo tofauti na tuliyotegemea kupata.

Tunaamini kama tunaweka juhudi fulani, basi tunapaswa kupata matokeo yanayoendana na juhudi hizo. Na pale matokeo tunayopata yanapokuwa tofauti, tunaona kama tumedhulumiwa au tumedanganywa.

Maisha

Lakini ukweli ni kwamba, mambo hutokea, na yanatokea kwa sababu yanatokea na siyo kwa sababu wewe umefanya au hujafanya unachopaswa kufanya.

Kwa mfano mafuriko yanapotokea kwenye eneo fulani, yanawaathiri wote, waliokuwa wanaweka juhudi kwenye kazi zao na ambao hawakuweka juhudi.

SOMA; UKURASA WA 992; Mambo Yangeweza Kuwa Mabaya Zaidi…

Kwa nje tunasema mambo mabaya hutokea hata kwa watu wazuri. Lakini kiuhalisia, ni mambo yanatokea, siyo mabaya na wala siyo mazuri, bali ni mambo yanatokea.

Ili kuepuka kuumizwa na matokeo unayopata ambayo hukutegemea kuyapata, jikumbushe kwamba mambo yanatokea, kwa sababu yanatokea na haijalishi wewe upo au haupo, haijalishi kama umetimiza wajibu wako au hujatimiza.

Unapotimiza wajibu wako, haikupi uhakika wa kupata unachopaswa kupata, wala haikupi kinga ya mabaya yanayotokea yasikudhuru, bali inakupa amani ya moyo, ukijua kwamba umeweka juhudi ulizopaswa kuweka.

Ukishaweka juhudi unazopaswa kuweka, lakini matokeo yakaja tofauti, hupaswi kukata tamaa, badala yake unahitaji kujifunza na kuendelea kuweka juhudi kubwa na bora zaidi. Matokeo yoyote unayopata, iwe unaona ni mabaya au mazuri, hakikisha hayawi kikwazo kwako kwa namna yoyote ile.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog