Moja ya mahangaiko ambayo sisi binadamu tumekuwa tunafanya, ni kwenda mbali kutafuta kitu ambacho tayari kipo pale tulipo. Halafu pamoja na kwenda mbali hatupati tunachotafuta, mwishowe tunaona maisha ni magumu na kukata tamaa.

Angalia mifano mingi na utajionea mwenyewe.

Mtu anaondoka kwenye kazi moja na kwenda kwenye kazi nyingine akiamini ndiyo itakuwa bora zaidi kwake, lakini baada ya muda ile kazi mpya inakuwa sawa na ya zamani.

Mtu anaacha biashara moja na kwenda kwenye biashara nyingine akiamini ndiyo biashara itakayokuwa na faida kwake, lakini anajikuta akiwa na changamoto zaidi kwenye biashara hiyo mpya kuliko hata ile ya zamani. Na fedha alizofikiri atapata, hazipati.

Taaluma

Mtu anaachana na mke au mume wake, akiamini atapata mwingine ambaye ni bora zaidi, ambaye hana mapungufu kabisa, anapata mwingine na mambo yanakuwa yale yale.

Ukweli ni kwamba, chochote unachotafuta kwenye maisha, kipo hapo ulipo sasa, hapo hapo, huhitaji kupiga hata hatua moja kwenda kukitafuta.

SOMA; UKURASA WA 761; Ukweli Haulazimishwi…

Unataka fedha na utajiri, hebu angalia kazi unayoifanya sasa, je unaifanya kwa viwango vya juu sana kiasi kwamba kila mtu mwenye shida anatamani wewe ndiye umsaidie? Kama jibu ni hapana, bado hujaona ukweli ambao unakuzunguka. Angalia biashara unayoifanya, je unatoa huduma bora sana kiasi kwamba watu wanasafiri mbali na wanasubiri kwenye foleni kusubiri huduma yako? Kama jibu ni hapana usijidanganye kubadili biashara ili kupata fedha.

Unataka mahusiano mazuri na mwenza wako, wala usianze kuangalia wapi unapata asiye na mapungufu. Angalia mapungufu gani uliyonayo wewe kwenye mahusiano hayo, pia angalia manufaa unayopata kutoka kwa mwenza wako, kisha linganisha hayo mawili na mapungufu yake. Utaona kila sababu ya kuweka juhudi kuboresha mahusiano yako zaidi.

Unataka kujifunza zaidi? Wala usifikirie kusafiri kwenda wapi, au kwenda kuanza shule wapi, anzia hapo ulipo, jifunze kwa mazingira, wanaokuzunguka, walioshindwa na hata walifanikiwa. Kwa mfano kama hutaki kuwa masikini, angalia masikini wanafanya nini na usifanye. Je hilo linakuhitaji wewe usafiri?

Usitange tange kutafuta ukweli, ukweli upo hapo ulipo sasa, fungua macho kuuona ukweli huo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog