“The great use of life is to spend it for something that will outlast it.” -William James
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo .
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maiha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MAISHA YA WANAOKUMBUKWA..
Muda wetu hapa duniani ni mfupi.
Ukilinganisha miaka labda 100 ambayo mtu akikazana sana anaishia, na miaka mabilioni ya uwepo wa dunia, muda wetu ni mdoho mno.
Watu wanazaliwa na watu wanakufa kila wakati.
Wapo ambao wakifa wanaendelea kukumbukwa na kuwa uwenye maisha ya wengine.
Na wapo ambao, kukumbukwa kwao ni mpaka watu waone kaburi na kuanza kujiuliza huyu ni nani na aliishije.
Ukiangalia maisha ya wanaoendelea kukumbukwa hata baada ya kufa, kuna kitu kikubwa walichofanyia kazi wakati wa uhai wao, ambacho kilikuwa kikubwa kuliko maisha yao.
Tutaendelea kumkumbuka Nyerere kwa sabau alipigania uhuru wa nchi.
Tutaendelea kumkumbuka Mandela kwa sababu alipigania haki na usawa kwa kila mtu.
Na wakati hao waliishi, kuna watu wengine walikuwepo, lakini leo hatuwajui kabisa kwa sababu hakuna makubwa waliyofanya.
Waliishi maisha yao ya kawaida na wamefutika baada ya kuondoka.
Lazima maisha yako yasukumwe na kitu kikubwa kuliko maisha yako, kama unataka kuendelea kubaki kwenye maisha ya wengine hata baada ya kufa.
Kama maisha yako yanasukumwa na unakula nini, unavaa nini na unalioaje madeni ya fedha ulizokopa kwa ajili ya kula na kuvaa, utafutika kwenye uso wa dunia kimya kimya.
Fanya yale ambayo ni makubwa kuliko wewe, ni magumu na yana changamoto, lakini zina maana kubwa kwako na kwa wengine pia.
Na muhimu, hufanyi ili uendelee kukumbukwa, bali unafanya ili kunufaisha wale wenye uhitaji wa kile unachofanya.
Nenda kachukie hatua za kuelekea kwenye ukubwa leo, kwenye kufanya makubwa, kwenye kugusa maisha ya wengine kwa namna ambayp hawawezi kukulipa na hawawezi kusahau, hiyo ndiyo njia itakayokufanya uendelee kuishi hata baada ya kufa.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha