Huwezi kufanikiwa kwenye maisha bila ya kupitia kushindwa.
Na tunaweza kusema kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wasiofanikiwa ni kushindwa.
Kila anayejaribu kufanya chochote kwenye maisha, lazima akutane na kushindwa.
Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wasiofanikiwa ni kinachotokea baada ya kushindwa.

Wasiofanikiwa, huacha baada ya kushindwa, huchukulia kushindwa kama kikwazo kikuu cha kufikia ndoto zao, wanakubaliana na kushindwa na kutojaribu tena.
Wanaofanikiwa, wanajua kushindwa ni sehemu ya ushindi, na wanatumia kushindwa kwao kama njia ya kufanikiwa.
Ukweli ni kwamba, kushindwa ni ujumbe mzuri kwetu, ndani ya kushindwa kuna ujumbe muhimu wa ushindi.
Unaposhindwa, maana yake kuna kitu hakijakaa sawa, ambapo kama ungefanikiwa huku kitu hicho hakijawa sawa, ingekuwa janga kubwa kwako.
Kushindwa ni njia ya asili ya kukuepusha na matatizo makubwa, kwa sababu mafanikio yanakuja na majukumu makubwa, kama hujajiandaa yatakupoteza.
Wote tunawajua watu ambao walikuwa na maisha mazuri kabla hawajapata fedha, ghafla wakapata fedha nyingi, maisha yao yakavurugika kabisa. Tunawajua watu ambao walikuwa vizuri kwenye kazi zao au maisha yao kabla hawajapata nafasi kubwa za uongozi, wanapata nafasi hizo na ghafla maisha yao yanakuwa ya hovyo.
SOMA; UKURASA WA 1087; Kigeugeu Cha Watu Inapokuja Kwenye Mafanikio Yako…
Kushindwa, hasa pale mtu unapojaribu kitu mwenyewe, ni ujumbe wa asili kwako kwamba kuna eneo ambalo bado hujawa vizuri, hivyo ukipewa unachotaka utajiharibu wewe mwenyewe na kuwaharibu wengine pia.
Hivyo kwa chochote unachoshindwa, kaa chini na jiulize asili inataka kukuambia nini? Ni ujumbe gani upo nyuma ya kushindwa kwako? Ni eneo gani ambalo bado hujawa vizuri, ambapo ukipata unachotaka mambo yatakuwa mabaya zaidi?
Tumia kila kushindwa kwako kama sehemu ya kupiga hatua zaidi, ya kujiimarisha zaidi na utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.
Kushindwa ni ujumbe wa asili kwako kwamba kuna maeneo hujajiweka vizuri, pata ujumbe huo na utumie kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog