Hili ni swali muhimu sana kujiuliza kwenye kila jambo unalofanya, swali ambalo litakuwezesha kujiandaa vizuri na pia kukuondolea hofu.
Iko hivi rafiki, mambo mengi mabaya yanaweza kutokea kwenye chochote unachofanya.
Ni uwezekano wa mambo haya mabaya kutokea ndiyo unawapa wengi hofu ya kujaribu vitu vipya. Kwa sababu wanafikiria kama mabaya yatatokea basi watapoteza kila walichonacho na kukosa mengi pia.
Lakini swali muhimu sana kujiuliza ni je kipi kibaya kabisa kinaweza kutokea?
Kwenye chochote unachofanya, jiulize kipi kibaya zaidi kinaweza kutokea. Kama kila kitu kitashindwa kabisa, ni matokeo gani mabaya kabisa unaweza kupata?

Unapojiuliza swali hili, unatafakari majibu yako kwa kina na kuona kila kinachoweza kutokea na hatari yake kwenye kile unachofanya.
Sasa ukishapata majibu, unajiandaa kwa matokeo mabaya kabisa. Kiasi kwamba kama mambo yatakuwa vibaya kabisa, basi utakuwa umejiandaa. Haitokei kama ajali au dharura, bali unakuwa ulishaona matokeo hayo na kuwa na maandalizi ya hatua utakazochukua.
SOMA; UKURASA WA 962; Dawa Kamili Ya Hofu Ya Kushindwa….
Unafanya zoezi hili siyo kujipa hofu, bali kujiandaa kwa mabaya yanayoweza kutokea, na mabaya yanatokea kila wakati.
Kama kuna kitu unafanya, halafu yakatokea matokeo mabaya kabisa na yakakushangaza, basi hukuwa umejiandaa, hukua umetafakari kwa kina na kujua kila hatua unayopaswa kuchukua.
Usikubali kufanya kitu chochote, ambacho hujatafakari kwa kina matokeo mabaya yanayoweza kutokea na ukajiandaa kwa hatua za kuchukua kwenye matokeo hayo.
Matokeo mabaya yanatokea kila wakati, kuwa na maandalizi ya kutosha ili yasiwe kikwazo kwa mafanikio yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,