Siku mpya,
Siku bora
Na siku ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu rafiki kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari SIYO KUSHINDWA, NI KUJIFUNZA…
Rafiki,
Watu wote wanaotumia neno kushindwa ni waongo.
Ndiyo, hata kama wewe ni mmoja wa watu wanaojiambia umeshindwa kitu fulani, unajidanganya tu.
Labda hutaki kuweka juhudi zinazostahili kuwekwa ili upate unachotaka.

Hivi unafikiri mtoto anapokuwa anaanza kutembea akaanguka, akasimama tena akaanguka, akajaribu tena na kuanguka, unadhani mtoto huyo atajiambia nimejaribu sana kutembea lakini nimeshindwa?
Hakuna kitu kama hicho, ataendelea kujaribu mpaka ataweza kutembea mwenyewe bila ya msaada wowote.

Lakini wewe unaanzisha biashara moja inakufa na bila ya aibu unawatangazia watu nimekazana sana na biashara lakini nimeshindwa. Kweli?
Upo kwenye ajira moja miaka mingi, haikulipi kiasi cha kukutosha na huoni aibu kusema nimejaribu sana lakini nimeshindwa.

Chochote unachojiambia umejaribu na kushindwa siyo kweli kwamba umeshindwa, bali umejifunza.
Sasa kwa kuwa labda haupo tayari kujifunza, kwa kuwa haupo tayari kuweka juhudi zaidi ili kuepuka makosa ya awali, utakimbilia kusema umeshindwa.

Na nikuambie tu rafiki yangu, hutafanikiwa kwa kusema umeshindwa, bali utafanikiwa kwa kujifunza na kuchukua hatua.
Haijalishi umeanza biashara na ikafa mara ngapi, unachopaswa kujua kuna makosa unafanya, na kama usipoyajua na kuepuka makosa hayo, utaendelea kuua kila biashara unayoanzisha. Sasa hapo ni kushindwa au kujifunza?

Jiambie utakavyo kwamba umeahindwa, lakini sisi tukikuangalia kwa nje tunajua hutaki kujifunza, u mzembe na mvivu, usiye na hamasa ya kupiga hatua zaidi.

Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya ushindi zaidi au kujifunza na siyo kushindwa.
#Fanya #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha