Upo usemi wa waswahili kwamba wakati mzuri wa kukitumia chuma, yaani kuunda kitu kipya kutoka kwenye chuma, ni wakati chuma hicho bado ni cha moto. Huu ni ukweli kabisa, maana chuma kikiwa cha moto ni rahisi kukitengeneza utakavyo, lakini kikishapoa, kinakuwa kigumu kutengeneza utakavyo.
Sasa hapa nataka kukupa sehemu mbili za kauli hii, ambazo zitakusaidia sana kwenye mafanikio yako.
Sehemu ya kwanza ni kukitumia chuma wakati bado ni cha moto.
Pale unapokuwa na hamasa ya kufanya kitu, kifanye wakati huo huo, usiseme unasubiri sijui mpaka kitu gani kikae sawa. Fanya wakati huo huo, hapo ndipo chuma ni cha mto na rahisi kukitumia.
Pale unapopata wazo la kufanya kitu fulani, ambacho unaona kitakuwa bora sana kwako, anza kukifanya hapo hapo. Usisubiri chochote, angalia wapi unaweza kuanzia na anzia hapo, kwa wakati huo.
Unapoanza kufanya, unaanzisha mwendo, ambao unakuwa rahisi kuendeleza kuliko ukiwa hujaanza kabisa. Na wakati mzuri wa kuanza, ni wakati ambapo chuma bado ni cha moto, wazo bado ni la moto, hamasa bado ipo juu.
SOMA; UKURASA WA 970; Hamasa Haisubiriwi, Hamasa Inatengenezwa…
Sehemu ya pili ni kukifanya chuma kuwa cha moto wakati wote.
Kama umewahi kupata hamasa kubwa ya kuanza kufanya kitu, halafu ukaanza na hamasa ile ikapotea kabisa na ukashindwa kuelewa, utakubaliana na mimi kwamba hamasa siyo kitu cha kutegemea sana kwenye kuchukua hatua.
Ni kweli kabisa, hasa pale unapotaka hamasa ya mara moja ndiyo ikupeleke mwanzo mwisho.
Unahitaji kukifanya chuma kuwa moto mara zote, hamasa unayoanza nayo ndiyo unayopaswa kuendelea nayo. Hivyo chochote kilichoanzisha hamasa yako ya kuchukua hatua, endelea kukifanyia kazi. Kama ni mwandishi fulani ambaye ukisoma kazi zake unapata hamasa ya kuchukua hatua, soma kazi zake na rudia hata zile ambazo umeshasoma. Kama ni mafunzo fulani au maarifa fulani ambayo ukiyapata yanakupa hamasa kubwa, jipe mafunzo na maarifa hayo mara kwa mara.
Chochote kinachoanzisha hamasa ndani yako, usikiache, endelea nacho ili hamasa hiyo isife. Endelea kuchochea moto wa hamasa ndani yako ili uweze kuchukua hatua zaidi. Kwa sababu safari ni ndefu na ngumu, bila ya hamasa inayodumu, ni rahisi kuishia njiani.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,