Sisi binadamu huwa tunapenda kuwa na raha na furaha muda wote. Kila wakati tunapenda kuwa kwenye hali ya hisia chanya, hizia za upendo, ujasiri, matumaini na furaha.
Lakini siyo mara zote maisha yanakwenda kama tunavyotaka sisi, siyo kila wakati mambo yanakwenda kama tulivyopanga, na hapa ndipo chimbuko la hisia hasi linapoanzia.
Mara kwa mara huwa tunajikuta na hisia hasi, hisia za hasira, hofu, kukata tamaa, wivu na hata wakati mwingine chuki.
Hisia hizi hasi zina nguvu kubwa ya kutuzuia kuendelea kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yetu, hivyo wengi tumejifunza kuzikimbia au kuzikandamiza, kitu ambacho hakitatui hisia hizi.
Twende na mfano huu mfupi, kama kuna sehemu unaona inatoa moshi, kufunika ili usione moshi huo hakuondoi kabisa moshi huo, badala yake moto unaozalisha moshi huo unaendelea kukolea na itafika wakati huwezi tena kuzuia moshi huo, maana utakuwa unatokea kila mahali. Njia pekee ya kuondokana na moshi huo ni kujua chanzo chake, yaani moto uko wapi kisha kuuzima.
Kwenye hisia zetu pia ndiyo pako hivyo, siyo hisia tunazozipata zina shida, ila kuna shida ipo ndani, ambayo inaibua hisia hizi hasi. Hivyo kukandamiza hisia hizi hakutatui shida ambayo ipo ndani, bali kunaifanya iendelee kuwa kubwa.
Chukulia mfano wa hisia hasi ya wivu, unapokuwa na wivu kwenye maisha ya wengine, ni rahisi kukandamiza hisia hiyo. Lakini hilo halitaondoa kile ambacho kimepelekea wewe uwe na hisia hiyo, ambacho kinaweza kuwa ni kujilinganisha na wengine au kutaka maisha yako yawe kama ya wengine. Kuondokana na hisia kama hii unapaswa kujua kwamba hakuna watu wawili wanaofanana kwa kila kitu hapa duniani, hata mapacha. Kwamba kila mtu ana njia yake maalumu ya kupita hapa duniani na kitu pekee kukazana nacho kwenye maisha ni kuwa wewe, kuweza kufikia uwezo mkubwa uliopo ndani yako.
Unapoingiwa na hisia hasi, usikazane kuikandamiza, badala yake jua chanzo chake, jua mzizi wake ni upi. Tafakari kwa kina kwa nini unajisikia vile unavyojisikia, je ni kitu gani ulitaka kiende kama unavyotaka wewe. Kisha jikumbushe ni nguvu kiasi gani unayo au unayokosa kwenye kupanga mambo yaende kama unavyotaka wewe mwenyewe. Angalia uhalisia na siyo matakwa yako mwenyewe. Kwa mfano pale unapokasirishwa na matendo ya wengine, badala ya kuangalia kile kilichokukasirisha, hebu mwangalie yule aliyekukasirisha kama mtu ambaye ana mapungufu yake. Mtu ambaye anajaribu kufanya kile anachofikiri ni bora na siyo kwamba amefanya kwa kusudi. Kwa njia hii utaweza kutatua tatizo hilo la hasira lisijirudierudie kwa sababu kile unachokipata kwa mtu mmoja, utakipata kwa wengine pia.
Usikandamize hisia hasi zinazoingia kwenye fikra zako, badala yake jua chanzo chake na kielewe na kukitatua ili uweze kuwa huru na hisia hizo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha, kwa haya uliyosema, kwa hii Elimu ninayoipata toka kwako hakika naimani itanifikisha pale ninapotaka kufika, lazima niache alama yangu na ya mwalimu wewe, kwa sasa nakaribia kumaliza mwaka tangu kujiunga ndani ya kisima cha maarifa, nayaona mafanikio makubwa hasa kwa kuanza kujenga misingi mizuri. Asante sana.
LikeLike
Vizuri sana Beatus kwa msingi huo mzuri wa mafanikio unaoendelea kuujenga ndani yako.
Endelea kuweka juhudi zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa zaidi.
Kocha.
LikeLike