Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio kwenye biashara na ujasiriamali hayaanzii kwako mwenyewe, bali yanaanza kwa wale ambao unawahudumia. Hii ina maana kwamba, kama unataka kufanikiwa kwenye biashara na ujasiriamali, basi unapaswa kwanza kuwawezesha wengine wafanikiwe.
Biashara na ujasiriamali ni eneo ambalo halihitaji ubinafsi hata kidogo. Ni eneo ambalo linakutaka ujali kwanza kuhusu wengine kabla hujajali kuhusu wewe mwenyewe. Ni eneo ambalo kama unataka kutatua matatizo yako, basi inabidi utatue kwanza matatizo ya wengine.
Changamoto kubwa inayowazuia wengi kufanikiwa kwenye ujasiriamali ni kutokuyajua mahitaji ya watu wanaowahudumia. Wajasiriamali wengi hasa wachanga huwa wanajisahau, wanafikiri wapo kwenye biashara kwa ajili yao na siyo kwa ajili ya wateja wao. Na hapa ndipo wanapochukua maamuzi kwa kujiangalia wao na siyo kuangalia wateja wao.
Ili kufanikiwa kwenye biashara na ujasiriamali, kila maamuzi unayoyafanya yanapaswa kuanza na mteja kabla hujajiangalia wewe. Hata kama kuna kitu wewe unakipenda kiasi gani, kama mteja hakipendi, kukifanya ni kujidanganya.
Leo nakwenda kukushirikisha mahitaji makuu manne ya watu ambayo kila mjasiriamali anapaswa kuyafahamu. Mahitaji haya yamekuwepo tangu enzi na enzi na yataendelea kuwepo kadiri watu watakavyoendelea kuwepo hapa duniani.
Wewe kama mjasiriamali, unapaswa kuyajua mahitaji haya manne na kuona jinsi gani kile unachouza kinatimiza mahitaji haya kwa wateja wako.
Karibu tujifunze mahitaji makuu manne ya watu na jinsi ya kuyatimiza kupitia biashara zetu.
Hitaji la kwanza; USHAWISHI.
Je kile unachouza kinamwezesha mteja kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine na wale anaojihusisha nao kwenye kazi na hata maisha yake? Watu huwa wanasukumwa kufanya maamuzi kwa kufikiria jinsi ambavyo wengine watawachukulia kwa maamuzi hayo.
Na hii ndiyo sababu bidhaa au huduma za anasa huwa zinapata wateja hata kama hazitofautiani sana na zile ambazo siyo za anasa. Kwa mfano hakuna tofauti kubwa kwenye mwili mtu anapovaa mkufu wa fedha (silver) na mkufu wa dhahabu. Lakini watu hupendelea zaidi kuvaa dhahabu kwa sababu hilo litatoa ujumbe kwa wengine kwamba watu hawa ni wa hadhi ya juu na hilo litawapa ushawishi zaidi kwa wengine.
Angalia bidhaa au huduma unayouza inawezaje kumpa mteja wako ushawishi mkubwa zaidi kwa wengine na mweleze mteja kuhusu ushawishi huo atakaoupata kwa kununua unachouza.
Watu wanapenda kusifiwa, watu wanapenda kuonekana wamefanya maamuzi sahihi na watu wanapenda kuonekana ni wa hadhi ya juu. Angalia jinsi kile unachouza kinaweza kutimiza hayo kwa wateja wako na utaweza kuuza zaidi na zaidi.
SOMA; Ngazi Nne Za Kuchukua Hatua Na Kiwango Halisi Cha Hatua Unazopaswa Kuchukua Ili Kufanikiwa.
Hitaji la pili; MAJIBU.
Hitaji la pili la watu ni kupata majibu ya tatizo kubwa ambalo limekuwa linawasumbua. Mpaka mteja anakuja kwako kununua, tayari ana majibu au mahitaji ambayo yanamsumbua. Mpaka anakubali kutengana na fedha zake ambazo huenda amezipata kwa taabu, ana msukumo mkubwa ndani yake wa kutatua tatizo linalomsumbua.
Hivyo lazima ujue kwa hakika ni tatizo au mahitaji gani ya mteja bidhaa au huduma unayouza inatatua. Lazima uelewe hilo kwa kina na umweleze mteja vizuri jinsi anavyonufaika kwa kununua bidhaa au huduma yako.
Pia mfanye mteja wako aonekane shujaa kwa kupata suluhisho la changamoto au mahitaji ambayo amekuwa nayo kwa muda mrefu. Kama alishasumbuka sehemu nyingi bila ya kupata majibu sahihi, hakikisha kwako anapata majibu ambayo yatamfanya awe shujaa kwa wengine.
Ni muhimu sana kujua mahitaji na matatizo ya wateja wako na jinsi biashara yako inayatatua kisha kuhakikisha wateja wako wanaelewa kwa kina nini wananufaika nacho wakinunua kwako.
Hitaji la tatu; MUDA.
Naweza kusema hili ndiyo hitaji kubwa sana kwenye zama tunazoishi sasa. Ipo kauli kwamba watu hawajui nini wanataka, lakini wakishajua, wanakitaka jana. Watu hawana muda, watu wana haraka, watu hawana subira. Kitu kikubwa ambacho biashara yako inapaswa kuwapatia wateja wako ni muda, kuwapa muda zaidi wa kufanya mambo muhimu kwenye maisha yako.
Hivyo angalia ni kwa namna gani bidhaa au huduma unayouza inawawezesha wateja kuokoa muda wao au kutokupoteza muda zaidi. Mweleze mteja ni muda kiasi gani anaokoa kwa kununua kwako kuliko akienda kununua kwa wengine. Au kwa kununua bidhaa au huduma fulani ukilinganisha na bidhaa au huduma nyingine.
Kama bidhaa au huduma unayouza inamtaka tena mteja kuweka muda mwingi ndiyo anufaike nayo, hutaweza kuiuza sana, kwa sababu hakuna mwenye muda.
Jali sana muda wa wateja wako na waoneshe ni jinsi gani chochote unachowauzia kinakwenda kuwapa muda zaidi kwenye maisha yao.
SOMA; Hii Ndiyo Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuwashawishi Wateja Kununua Chochote Unachouza.
Hitaji la nne; MARAFIKI.
Sababu kubwa inayopelekea maeneo ya starehe kupata wateja wengi ni ile hali ya urafiki ambayo mtu anaipata kwa kukutana na wengine ambao wanapendelea vile ambavyo mtu anapendelea. Watu wanapenda kutengeneza na kukuza mtandao wa watu wanaojuana nao.
Hivyo ni muhimu sana kile unachouza kiwe kinamwezesha mteja wako kutengeneza marafiki zaidi, kujulikana zaidi na kukuza mtandao wa watu anaojuana nao.
Inaweza kuwa ni kwa matumizi ya unachouza hadhi ya mteja wako inapanda zaidi au kwa kutumia kitu hicho anakutana na wengine wanaotumia kisha wanafahamiana na kuwa marafiki.
Kwa vyovyote vile, hakikisha bidhaa au huduma unayouza inawawezesha wateja wako kuwa na marafiki zaidi, inawawezesha kukuza mitandao yao na kujulikana zaidi. Ni kitu ambacho watu wanakihitaji sana.
Rafiki, mahitaji hayo manne makuu ya watu, yafanyie kazi kwenye biashara yako. Na kila bidhaa au huduma unayouza, angalia inatimizaje mahitaji hayo ya watu. Pia unapokuwa unatangaza biashara yako au kuwashawishi wateja kununua, wakumbushe jinsi ambavyo kile unachowauzia kitawatimizia mahitaji hayo manne.
Unaweza kutumia kauli kama, ukinunua hii itakufanya uonekane ni mtu muhimu zaidi au mtu wa juu zaidi, au itakusaidia kuokoa muda wako zaidi (ukitaja kiwango cha muda itasaidia zaidi) au unaweza kumwambia kwa kununua atakutana na watu wengine ambao wamenunua na watakuwa marafiki. Wewe unaijua biashara yako vizuri, tumia haya uliyojifunza kutengeneza ushawishi mpya kwa wateja wako ili waweze kununua zaidi.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge