Biashara kuu ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni umakini wa watu. Kadiri chombo kinavyokuwa na umakini wa watu wengi, ndivyo kinavyofanikiwa zaidi. Kwa sababu chombo kikishakusanya umakini wa watu wengi, kinaweza kuwatangazia vitu mbalimbali ambavyo watu wanakilipa chombo hicho kutangaza.

Hivi ndivyo mitandao ya kijamii na hata vyombo vya habari vinatengeneza kipato, kwa watu kutangaza kupitia vyombo hivyo. Na kigezo pekee ambacho mtu anayetaka kutangaza anatumia ni kuuliza tangazo langu litawafikia watu wangapi? Ni mchezo wa namba, kadiri tangazo linavyowafikia wengi, ndivyo mtu anavyolipa zaidi.

Kwa hisa unaona hapa chombo cha habari au mtandao wa kujamii inabidi ufanye nini ili kupata fedha zaidi! Kinahitaji kukusanya umakini wa watu wengi zaidi. Kadiri chombo kinavyokuwa na watu wengi wanavyokifuatilia, ndivyo kinavyoweza kupata fedha zaidi kupitia matangazo.

Sisi binadamu tunasukumwa na nguvu mbili katika kufanya au kufuatilia kitu, tamaa ya kupata kitu fulani au hofu ya kupoteza kitu fulani.

Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii imejenga msingi wake kwenye hofu, na hofu pekee ambayo wanaitumia vizuri ni hofu ya kupitwa. Hivi unafikiri kwa nini unapata msukumo sana wa kuingia kwenye mitandao hiyo? Kwamba usipoingia utakufa? Unafikiri nini kinakusukuma uhakikishe unafuatilia kila habari zinazoendelea? Kwamba usipokuwa na habari hizo maisha yanafika ukingoni?

Jibu ni moja tu, unasukumwa kuingia kwenye mitandao na kufuatilia kila aina ya habari kwa sababu unaona usipofanya hivyo unapitwa. Lakini huo siyo ukweli, hiyo ni hofu ambayo umetengenezewa ili uendelee kuwa bidhaa kwenye vyombo hivyo.

Rafiki, umakini wako unawindwa na wengi, umakini wako ni bidhaa ya wengine kutengeneza kipato, usikubali kuendelea kugawa umakini wako hovyo kiasi hicho.

Kumbuka umakini wako ndiyo kitu pekee unachomiliki, kitu pekee unachoweza kutumia kupiga hatua zaidi. Usipoteze umakini wako kwa wawindaji hao, peleka umakini wako kwenye kuzalisha matokeo bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha