Kama unatumia muda wako mwingi kufuatilia habari au mitandao ya kijamii, picha uliyonayo kuhusu wewe binafsi, wengine na hata dunia itakuwa picha ambayo ni mbovu sana.

Kuna kweli tatu muhimu ambazo dunia haitaki wewe uzijue, kwa sababu ukizijua utakuwa huru na hakuna atakayeweza kukutumia kwa manufaa yake.

Kadiri ambavyo wengi hawazijui kweli hizi tatu, ndivyo wachache wanavyonufaika, kwa sababu inawalazimu kutegemea wengine na kununua vitu fulani ili kuyakamilisha maisha yao, ambayo wameshaoneshwa kwamba siyo kamilifu.

Ukweli wa kwanza ni kwamba wewe ni wa kipekee, wewe ni bora sana.

Huu ni ukweli wa kwanza ambao dunia haitaki uujue. Dunia imekuwa inakuambia wewe siyo bora, wewe ni mkosaji na usiyestahili na tena imekuwa inakazana kukuambia wewe ni wa kawaida, kama walivyo watu wengine.

Fungulia chombo chochote cha habari au tembelea mtandao wowote wa kijamii na utakutana na kila aina ya ujumbe wa kukuonesha kwamba wewe siyo bora kama unavyofikiri. Utakutana na matangazo ya bidhaa na huduma mbalimbali ambazo zinakuonesha wewe hujakamilika mpaka utumie kile kinachotangazwa.

Huo ni uongo uliotengenezwa ili kukufanya wewe uwe tegemezi kwa wengine, jua ukweli ambao ni wewe ni bora sana na wa kipekee, una uwezo wa kipekee wa kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Ukweli wa pili ni watu ni wazuri na wana nia njema kwenye kila wanachofanya.

Kuna watu wachache sana ambao watakuumiza wewe kwa makusudi, na wanaofanya hivyo huwa wanakuwa na ugonjwa wa akili. Lakini watu wengi ambao unakutana nao kwenye maisha yako ya kila siku, ni watu wazuri na wenye nia njema kwa chochote wanachofanya.

Lakini katika kufanya yao, kuna namna watakukwaza au kukukwamisha, kitu ambacho utaona ni kibaya, kwa sababu dunia inakuonesha kila anayekuzunguka ni mbaya na unapaswa kujihami.

Fungulia chombo chochote cha habari au tembelea mtandao wowote wa kijamii na ujumbe utakuwa wazi kwako, watu ni wabaya, jihami na jilinde wasikudhuru.

Ukweli ni kwamba, pale wengine wanapofanya kitu ambacho kinakuumiza, kukukwaza au kukukwamisha wanakuwa hawajadhamiria kufanya hivyo. Wanakuwa wametingwa na maisha yao na hawajui kama wanachofanya kina madhara kwako. Ukiwaelewa watu kwa namna hii utakuwa huru sana, utaweza kuwaamini wengi na hata watu pia wataweza kukuamini wewe.

Ukweli wa tatu ni dunia ni sehemu salama na bora sana ya kuishi.

Fungulia chombo chochote cha habari na habari utakazozisikia zitakufanya uone kama dunia imefika mwisho. Habari hasi za mambo mabaya yanayoendelea duniani ndiyo zimetawala vyombo hivyo. Lakini kwa kila jambo baya moja linalotangazwa sana, kuna mambo mengine mazuri zaidi ya 100 yametokea pia, lakini hayo hayatangazwi.

Dunia inataka wewe uamini kwamba dunia siyo sehemu salama ya kuishi, ili ukose uhuru na kuwategemea watu fulani kwa usalama wako. Ujione kwamba huna cha kufanya zaidi ya kutegemea wengine kuchukua hatua juu yako.

Ukweli ni kwamba dunia ni sehemu salama na bora sana ya kuishi sasa ukilinganisha na siku za nyuma. Licha ya changamoto zilizopo, lakini kiwango cha usalama na uhakika wa maisha sasa ni kikubwa kuliko kipindi cha nyuma. Hivyo kuwa huru kuishi maisha unayotaka na usikubali kujazwa hofu zozote zile kuhusu ubaya wa dunia.

Zijue kweli hizo tatu, kuhusu wewe mwenyewe, wale wanaokuzunguka na dunia kwa ujumla na utakuwa huru kuishi maisha unayoyataka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha