“What assistance can we find in the fight against habit? Try the opposite!”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 1.27.4

Siku mpya,
Siku bora,
Na siku ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana kwetu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari JARIBU KINYUME CHAKE…
Mabaliko kwenye maisha mara nyingi hayahitaji nguvu kubwa sana,
Bali yanahitaji ufanye maamuzi ya tofauti na ulivyozoea kufanya.
Mfano kama kuna kitu ambacho umezoea kufanya kila siku na kinakuletea matokeo ambayo huyapendi, njia bora ya kupata matokeo tofauti ni kufanya tofauti na ambavyo umekuwa unafanya.
Hilo wala halihitaji ushauri mkubwa kutoka kwa wengine, ni wewe tu kufanya tofauti.

Mfano kama umekuwa unashindwa kuweka akiba kwa sababu ukipata fedha unatumia yote, hebu anza kuweka fedha pembeni kwanza kabla hujatumia.
Kama umekuwa unashindwa kuamka asubuhi na mapema kwa sababu unachelewa kulala, hebu anza kuwahi kulala.
Kama umekuwa unaingia kwenye migogoro ya mahusiano kwa sababu ya mabishano, hebu acha kubishana.
Kama umekuwa unachelewa kufika kwenye kazi au biashara yako kwa sababu ya kuchelewa kutoka, hebu anza kuwahi kutoka.
Kama kipato chako ni kidogo kwa sababu hujifunzi na unafanya kwa mazoea, hebu anza kujifunza na kufanya kwa mazoea.

Rafiki, chochote unachofanya sasa ambacho hakikupi matokeo unayoyataka, fanya maamuzi ya kufanya kinyume chake, na kwa hakika, utapata matokeo ya tofauti na unayopata sasa.

Wapo watu huwa wanasema hawawezi kufanikiwa kwa sababu hawana watu wazuri waliofanikiwa wa kuwashauri.
Na jibu ambalo huwa nawapa ni moja, kila eneo kuna watu ambao hawajafanikiwa, angalia nini wanafanya na wewe fanya kinyume na wao, na kwa hakika utafanikiwa sana.
Kama upo kwenye kazi, angalia wale walioshindwa wanafanya nini, na fanya kinyume na wanachofanya wao. Wanachelewa kazini wewe wahi, wanawahi kuondoka kazini wewe chelewa kuondoka, wanachelewa kukamilisha majukumu yao wewe kamilisha kwa wakati, wanalalamika wewe usilalamike.
Kadhalika kwenye biashara, mahusiano na maisha kwa ujumla, angalia kile ambacho walioshindwa wanapenda kufanya na acha kukifanya mara moja, fanya kinyume chake.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya kinyume yale ambayo hayakuletei matokeo mazuri na walioshindwa wanapenda kuyafanya.
#FanyaKinyume #MazoeaNiMabaya #KufanikiwaNendaKinyumeNaAmbaoHawajafanikiwa

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1