“Philosophy calls for simple living, but not for penance—it’s quite possible to be simple without being crude.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 5.5

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUISHI FALSAFA SIYO KUJITESA…
Watu wengi wamekuwa wanafikiri kuishi kwa falsafa au misingi fulani ni kujitesa.
Kwamba unajinyima uhuru wa kufanya kila unachotaka.
Na pale unapoteleza basi inabidi ujiadhibu sana na kujitesa.
Lakini hilo siyo sahihi.
Kuishi kwa falsafa au misingi yoyote siyo kujitesa, bali ni kuchagua kuwa na mwongozo sahihi kwenye maisha.
Na pale unapoteleza kwenye falsafa au misingi hiyo, haihitaji ujiadhibu au ujitese.
Badala yake jua kukosea ni ubinadamu na rudi kwenye mstari kwa kufanya kilicho sahihi.

Kadhalika kwenye kuishi misingi ya mafanikio,
Wengi huona ni maisha ya mateso,
Kwamba kujinyima ili uweke akiba na kuwekeza,
Kuacha kupoteza muda kwenye anasa mbalimbali,
Na kuachana na marafiki wasio na mwelekeo,
Wengi huchukulia haya ni mateso makali,
Lakini siyo mateso, badala yake ni kuchagua vipaumbele sahihi kwako.
Ambavyo vitakuwezesha kuwa na maisha unayoyataka.
Na pale unapoteleza, jikumbushe njia sahihi kisha ifuate, huna haja ya kujiadhibu na kujitesa sana.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kwa misingi uliyochagua, ambayo ina maana kubwa kwako na siyo ya kujitesa. Pia unapokosea, jisahihishe badala ya kujiadhibu.
#KuishiMisingiSiMateso #FurahaKwenyeMaishaSiKupataKilaUnachotaka #UtakoseaMaraNyingi

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1