Rafiki yangu mpendwa,

Ukiondoa simu janja (smartphone) za mkononi, tv ni kifaa cha pili ambacho kimekuwa kinatumia muda wa watu wengi, lakini kina manufaa kidogo sana kwenye maisha yao.

Karibu kila familia ina tv katika sebule au chumba chochote kwenye nyumba, ambapo watu hukutana kwa pamoja kuangalia habari, tamthilia na hata vitu vingine ambavyo watu wanaweza kuangalia kupitia televisheni.

Kwa sehemu kubwa, vitu ambavyo watu wamekuwa wanatumia muda mwingi kuangalia kwenye tv, havina manufaa makubwa kwao, vinawapotezea muda na haviongezi chochote kwenye maisha yao.

Leo tunakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kuitumia tv yako kwa manufaa, kitu ambacho wengi hawakijui au hawajawahi kukifikiria.

WhatsApp Image 2019-08-22 at 19.00.45.jpeg

Swali la kuanza nalo hapa ni hili; je unajua ya kwamba unaweza kunufaika sana na tv uliyonayo nyumbani kwako leo?

Groucho Marx amewahi kunukuliwa akisema “I find television very educational, every time someone switches it on I go into another room and read a good book”, kwa tafsiri rahisi anamaanisha kwamba amegundua tv ni moja ya vitu vyenye mafunzo makubwa sana kwa sababu pale mtu anapoiwasha, yeye huenda kwenye chumba kingine na kusoma kitabu kizuri.

Hebu fikiria kama na wewe ungeweza kufanya hivi, kwamba kila wakati mtu anapowasha tv kuangalia, basi wewe unakwenda kwenye chumba kingine na kusoma kitabu, je unafikiri ungebaki hapo ulipo sasa, ambapo umekaa kwa muda mrefu?

Tafiti nyingi zimekuwa zinaonesha kwamba kwa siku watu wanatumia siyo chini ya masaa matatu kwenye tv zao, vipi kama utatumia muda kama huo kujisomea vitabu? Kwa hakika utapiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Sasa mimi rafiki yako, ninakushirikisha njia rahisi na bora sana kwako kunufaika na tv uliyonayo nyumbani kwako, ambayo wala haihusishi kwenda kwenye chumba kingine pale mtu anapowasha tv.

Badala yake, njia ninayokwenda kukushirikisha hapa, inakwenda kubadili utamaduni wa nyumba nzima inapokuja kwenye kuangalia tv au kujifunza kwa kusoma vitabu.

Njia ninayokushirikisha hapa ni kutengeneza maktaba ndogo pembeni ya tv yako. Una tv kwenye nyumba yako, basi pembeni ya tv hiyo tengeneza maktaba ndogo ambayo utaitumia kuweka vitabu muhimu kwa mafanikio yako.

Fanya vitu hivi viwili, tv na maktaba yako viwe karibu kabisa, kiasi kwamba wewe au mtu mwingine anapokuwa anaangalia tv basi pembeni yake anaona vitabu.

Siyo lazima maktaba hii iwe kubwa sana, unaweza kutengeneza sheflu moja au mawili na kisha kupanga vitabu vyako. Muhimu ni kila unapoangalia tv basi pembeni yake uone vitabu.

SOMA; TAARIFA MUHIMU; Vitabu Vipya Viwili Vimetoka, Elimu Ya Fedha Na Tano Za Juma. Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuvipata.

Kwa kuweka maktaba ndogo pembeni ya tv yako, unanufaika kwa njia zifuatazo;

Moja; unabadili kabisa utamaduni wako na wengine waliopo kwenye nyumba yako. Kuviona vitabu kila wakati kunawafanya watu wafikiri tofauti na wasipoviona vitabu.

Mbili; inakupa kitu cha tofauti kufanya pale ambapo hakuna cha maana kwenye tv. Najua kuna wakati unaweza kuwasha tv na usione kitu cha maana, ukabadili stesheni mbalimbali lakini usipate kipindi kizuri cha kuangalia. Huu ni wakati mzuri kwako kuzima tv na kufungua kitabu.

Tatu; inawafanya wageni kwenye nyumba yako kupata mtazamo wa tofauti kuhusu wewe na familia yako. Wengi wamezoea kuona tv na vitu vingine vya burudani sebuleni, wanapokutana na vitabu, inawafanya waone ni kitu cha tofauti na hata kuthamini pia.

Nne; unaondoa ugumu wa kujifunza, kwa sababu ni rahisi kusema hujifunzi kwa sababu hupati vitabu au muda wa kusoma. Sasa unapokuwa unaangalia tv na pembeni yake kuna vitabu, hutajidanganya kwamba huna muda, badala yake utachukua hatua sahihi.

Tano; unapata msukumo wa kukuza zaidi maktaba yako. Kama unatumia tv, unajua ni jinsi gani unavyoshawishiwa kulipia kifurushi cha king’amuzi kila mwezi ili uweze kuona vipindi unavyovipenda. Hivyo pia ndivyo itakavyokuwa kwenye maktaba yako, kadiri unavyoiangalia kila siku, ndivyo unavyopata msukumo wa kununua vitabu na kuviweka hapo. Unapokuwa na shelfu za vitabu ambazo ni tupu mbele yako, unasukumwa kuweka vitabu kwenye shelfu hizo, na hivyo unakuwa na fursa zaidi ya kujifunza.

Rafiki, kuna manufaa mengi sana kwako kuweka maktaba ndogo ya vitabu pembeni ya tv yako, fanyia kazi hili leo hii na utabadili kabisa utamaduni wako na wale wanaokuzunguka.

Siyo gharama kubwa kulitekeleza hili, kama umeweza kununua tv, basi pia unaweza kutengeneza shelfu la vitabu na kuweka pembeni ya tv yako, fanyia kazi hilo sasa.

Na katika maktaba yako, anza na vitabu viwili muhimu sana kwako, ambavyo vitakuwa na manufaa makubwa kwako na kwa familia yako. Vitabu hivyo ni ELIMU YA MSINGI YA FEDHA na TANO ZA MAJUMA 50 YA MWAKA. Kuvipata vitabu hivi, piga simu namba 0678 977 007.

OMBI; Rafiki, naomba tusaidiane kutengeneza utamaduni mpya wa usomaji wa vitabu kwenye jamii zetu. Naomba kama una maktaba (hata kama ni ndogo) nyumbani kwako, basi nitumie picha yako ukiwa pembeni ya maktaba hiyo. Na kama utafanyia kazi wazo hili la kutengeneza maktaba pembeni ya TV yako basi piga picha na nitumie kwa barua pepe maarifa@kisimachamaarifa.co.tz au wasap namba 0717 396 253.

Ni wakati wako sasa wa kunufaika na tv uliyonayo nyumbani kwako, weka maktaba ndogo pembeni ya tv hiyo weka vitabu na utatengeneza utamaduni wa tofauti kabisa. Chukua hatua sasa ili usiendelee kupoteza muda kwenye tv yako na hata simu janja.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha