“We must undergo a hard winter training and not rush into things for which we haven’t prepared.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 1.2.32
Tushukuru sana kwa nafasi hii nyingine nzuri ambayo tumeweza kuiona siku hii ya leo.
Siyo kwa akili zetu, wala uwezo wetu, bali ni bahati tu.
Hivyo tutumie vizuri bahati hii kwa kufanya kilicho sahihi na chenye maana na manufaa kwetu na wengine pia.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari PITIA MAFUNZO MAGUMU KWANZA…
Ni lazima upitie mafunzo magumu kwanza kabla hujapewa nafasi ya kufanya makubwa na magumu.
Hakuna mwanajeshi anayeenda vitani siku yake ya kwanza ya kujiunga na jeshi. Anapitia mafunzo magumu sana na yanayomuandaa kwa ushindi vitani.
Hakuna daktari anayeanza kufanya upasuaji siku ya kwanza ua kujiunga na fani ya udaktari. Ni lazima apitie mafunzo magumu sana ndiyo aweze kufanya upasuaji nw matibabu mwengine.
Hakuna mfanyabiashara anayepata mafanikio makubwa kwenye biashara yake ya kwanza kufanya. Ni lazima apitie mafunzo magumu kwanza ndipo aweze kufanikiwa kwenye biashara zinazofuata.
Hapa kuna vitu viwili tunapaswa kuvijua nw kuvitumia kila siku;
Moja; usikimbilie vitu vikubwa kabla hujapita kwenye mafunzo magumu, ni sawa na kujipeleka kwenye tundu la simba kwenye njaa, unaenda kuwa kitoweo. Pitia kwanza kwenye mafunzo magumu, upikwe na kuiva na ndiyo uweze kujaribu makubwa zaidi.
Kama hujawahi kufanya kabisa biashara, usianze na biashara kubwa kwa kuweka fedha nyingi, badala yake anza na biashara ndogo kwa kuweka mtaji kidogo kabisa na hapo utajifunza mengi sana.
Mbili; unapokutana na ugumu usiumie wala kukata tamaa. Badala yake shangilia kwamba unapitia darasa ambalo linakuandaa kuwa bora zaidi.
Kama kuna kitu unafanya na hukutani na ugumu wala changamoto yoyote, unapaswa kuwa na wasiwasi. Huenda siyo kitu sahihi au unakifanya kwa kiwango kisicho sahihi, na yote hayo yanakuweka kwenye hali ya hatari utakapofika kwenye mapambano ya kweli.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupitia mafunzo magumu yanayokuandaa kwa mapambano makubwa zaidi ya baadaye.
#NidhamuUadilifuKujituma #AfyaUtajiriHekima #KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1