Pale ambapo watu wawili wanakuwa wamekwazana na wote wanaongea, msuguano unakuwa mkubwa na mawasiliano yanakuwa mabovu. Ni vigumu sana kusikilizana na kuelewana pale watu mnapokuwa mmeudhika na wote mnaongea.

Ni lazima mtu mmoja anyamaze kwanza, mwingine aongee mpaka amalize na kisha kupeana nafasi ya kusikilizana. Hapo ndipo mawasiliano yanaweza kukamilika vizuri na kufikia muafaka mwema.

Kila unapojikuta kwenye hali ya kutokuelewana na wengine, kuwa wa kwanza kukaa kimya wakati mwingine anaongea, mwache aongee mpaka amalize, huku ukisikiliza kwa makini na kisha chukua nafasi ya kutatua vyema kile kilichotokea na namna ulivyomsikia mwenzako alivyoelezea.

Mpaka watu wawili wanafikia hali ya kutoelewana, kunakuwa na makosa kwa kila upande, hivyo muhimu siyo kutafuta lawama ziende kwa nani, bali muhimu ni kutafuta njia gani bora ya kutatua kilichotokea. Na ili kuweza kutatua, lazima mpeane nafasi ya kusikilizana kwanza.

Kwa kupeana nafasi ya kusikilizana, matatizo mengi yanapata suluhisho. Mawasiliano bora ni suluhisho la matatizo mengi, hasa kwenye mahusiano. Weka kipaumbele kwenye mawasiliano bora na utapunguza changamoto nyingi za kimahusiano na wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha