Kuna sababu kwa nini huwa zinaitwa njia za mkato, na sababu yenyewe ni kwamba huwa hazifanyi kazi.
Kama njia hizo zingekuwa zinafanya kazi basi zingekuwa ndiyo njia kuu, na siyo njia ya pembeni na ya mkato. Kwa sababu tunajua kila mtu anapenda mafanikio, na kama kuna njia rahisi ya uhakika ya kuyafikia, kila mtu atapenda kuitumia.
Njia za mkato huwa zina faida kwa upande mmoja, ule upande ambao unatoa njia hizi na siyo upande unaotumia njia hizo. Wale ambao wanakuonesha njia ya mkato, hao ndiyo wanaonufaika, na siyo wewe unayeitumia njia hiyo.
Kwa chochote unachofanya, mtu anapokuja kwako na kukuambia ana njia ya mkato ya wewe kufanikiwa, mwambie kwa nini asiitumie mwenyewe na akuletee wewe? Je yeye hayapendi mafanikio? Na kama anakuambia anaitumia, basi iwe anatumia ile njia anayokuambia, na siyo amefanikiwa kwa kuwaambia watu njia hiyo. Maana huo ndiyo upande wao wa kufanikiwa.
Halafu kuna ile hali ya kujidanganya sisi wenyewe, kujiambia kwamba safari hii mambo ni tofauti, kwamba njia hii inaweza kufanya kazi acha tuijaribu. Huku ni kujidanganya ambapo kunawaumiza wengi, kwa kuona hakuna watakachopoteza wakijaribu. Lakini utapoteza mengi, muda, nguvu na hata fedha.
Njia pekee ya kufanikiwa ni moja, tangu enzi na enzi na hakuna dalili kwamba itabadilika siku za karibuni. Njia hiyo ni hii; JUA KILE UNACHOTAKA, JUA GHARAMA UNAYOPASWA KULIPA ILI KUKIPATA NA KISHA JITOE KULIPA GHARAMA HIYO.
Mtu anayekuambia kuna fursa ya wewe kufanikiwa bila ya kulipa gharama, jua wewe ndiyo fursa kwake, kaa mbali sana na watu au vitu vya aina hiyo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ni kweli kocha hakuna nafanikiwa yanayopatikana kirahisi kulipa gharama ni lazima.
LikeLike