‘Kubwa ni bora’, huu ni usemi ambao ni maarufu sana kwenye biashara. Ukiwa unaashiria kwamba kadiri biashara inavyokuwa kubwa, ndivyo inavyokuwa bora kwa watu wote, kuanzia kwa mmiliki wa biashara ambaye anatengeneza faida zaidi, wafanyakazi wa biashara ambao wanapata kipato kizuri na hata wateja wa biashara ambao wanapata bidhaa au huduma bora na kwa bei rafiki.

‘Kama biashara haikui basi inakufa’, ni usemi mwingine maarufu kwenye biashara ambao unawasukuma wafanyabiashara kuhakikisha wanakuza biashara zao kwa namna yoyote ile. Kwa sababu kama biashara haionekani kukua, basi inakuwa inakufa. Lakini njia ambazo wafanyabiashara wamekuwa wanatumia kukuza biashara hizo, zimekuwa haziwaachi salama. Wengi wamekuwa wanachukua mikopo ambayo ina gharama kubwa kwa biashara au kukaribisha wawekezaji ambao wakishawekeza fedha zao wanachotaka ni kitu kimoja tu, faida.

Msukumo huu mkubwa ambao umewekwa kwenye ukuaji wa biashara umekuwa chanzo cha biashara nyingi kuharibika na hata maisha ya wafanyabiashara wengi kuwa magumu. Kuna biashara ambazo ni nzuri sana zikiwa ndogo, zinafanya vizuri na kutengeneza faida, lakini zikishakuwa kubwa mambo yanakuwa tofauti. Biashara hizi zinageuka kuwa ngumu na faida inakuwa vigumu kupatikana.

Kwa bahati nzuri sana, siyo kila biashara imeingia kwenye mtego huo wa kubwa ni bora au kama hukui basi unakufa. Zipo biashara ambazo zimechagua kuwa ndogo lakini zenye ubora, ambapo wafanyabiashara kwa makusudi kabisa walikataa kutumia fursa za kukuza zaidi biashara zao na kukubali kubaki na biashara ambayo ni ndogo.

small-giants.jpg

Mwandishi Bo Burlingham ametuchambulia biashara hizi ambazo zimechagua kubaki ndogo lakini zina mafanikio makubwa sana. Kwenye kitabu chake kinachoitwa Small giants: companies that choose to be great instead of big, Bo ametushirikisha jinsi kampuni hizo za tofauti zilivyoweza kuwa na mafanikio makubwa licha ya kuepuka njia za kawaida za ukuaji wa biashara.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kujifunza faida saba za kuchagua kuwa na biashara ndogo na kutokusumbuka kuikuza zaidi. Kwenye makala ya TANO ZA JUMA la 39 la mwaka 2019 tutakwenda kujifunza kwa kina jinsi ya kuchagua kuwa na biashara ndogo yenye mafanikio makubwa na kuziepuka changamoto zinazoletwa na ukuaji wa biashara.

Karibu uzijue faida hizi saba za kuchagua kuwa na biashara ndogo na kutokusumbuka kuikuza zaidi.

Moja; umiliki na udhibiti wa biashara.

Unapoanzisha biashara yako ndogo, wewe pekee au wale ulioanzisha nao ndiyo mnakuwa wamiliki wa biashara hiyo na hivyo mnakuwa na udhibiti mkubwa wa biashara. Na kadiri biashara inavyoendelea kuwa ndogo, ndivyo umiliki na udhibiti unavyobaki kwa waanzilishi wa biashara hiyo. Umiliki na udhibiti wa biashara unapobaki kwa watu wachache, unafanya biashara iweze kuendeshwa vizuri na kuweka vizuri vipaumbele vya biashara hiyo.

Lakini biashara inapokazana kukua, inalazimika kugawa umiliki kwa watu wengine, ambao wanaweza kuja kama wawekezaji. Pale ambapo watu wanawekeza fedha kwenye biashara, lengo lao huwa ni moja, kupata faida zaidi. Hawajali vipaumbele vya biashara hiyo ni vipi, wanachotaka ni faida. Na kama ikitokea biashara hiyo haizalishi faida kama wawekezaji walivyotarajia, basi uongozi unaweza kuondolewa, hata kama ndiyo waanzilishi wa biashara hiyo.

Tumeona mifano mingi ya makampuni yaliyoanza yakiwa madogo na kufanya vizuri, lakini baada ya kukaribisha wawekezaji mambo yakabadilika na hata kupelekea waanzilishi wa biashara hizo kufukuzwa kabisa.  Mfano mmoja ni kampuni ya Apple ambayo ilianzishwa na Steve Jobs na miaka ya 80 mwanzoni ikaingia kwenye soko la hisa, miaka ya 80 mwishoni Jobs akafukuzwa kwenye kampuni hiyo na wawekezaji.

Unapochagua kubaki na biashara ndogo, unabaki na umiliki na udhibiti wa biashara hiyo na kuweza kufanyia kazi vipaumbele sahihi vya biashara bila ya kushinikizwa na yeyote.

SOMA; USHAURI; Jinsi Unavyoweza Kufanya Biashara Yenye Mafanikio Ukiwa Bado Umeajiriwa.

Mbili; uhuru wa kufanya kile unachopenda.

Kama tulivyojifunza hapo juu, watu wanapowekeza kwenye biashara wanaangalia kitu kimoja tu, faida. Unapochukua mkopo wa biashara, ambao unapaswa kuurejesha kwa riba, kitu pekee unachoangalia ni kimoja, faida. Ni kweli kwamba lengo kuu la kufanya biashara ni kutengeneza faida, lakini kuna wakati ambapo biashara inabidi iepuke kufanya baadhi ya vitu ambavyo vingeleta faida kubwa.

Unapoanzisha biashara ndogo, pamoja na kwamba unakuwa unataka kutengeneza faida, lakini pia mara nyingi unakuwa unapenda kile ambacho unafanya kwenye biashara hiyo. Hivyo kuna wakati zitakuja kwako fursa za kutengeneza faida zaidi, lakini haziendani na kile unachopenda kufanya, na hivyo kuchagua kutokuzitumia.

Biashara inapokuwa ndogo na udhibiti uko kwako unaweza kufanya maamuzi ya aina hii na asiwepo yeyote wa kukusumbua. Lakini biashara inapokuwa kubwa na ina wamiliki wengi, hawawezi kukubaliana na wewe kuacha faida kwa sababu ya kuangalia mapenzi yako.

Kama unataka kuwa na biashara ambayo unafanya kile unachopenda na siyo kukimbizana na faida kubwa kila wakati, kuifanya biashara yako kubaki ndogo kuna manufaa zaidi kwako.

Tatu; mahusiano mazuri na wafanyakazi.

Kadiri biashara inavyokuwa kubwa, ndivyo mahusiano ndani ya biashara hiyo yanakuwa dhaifu. Hapa ni mahusiano baina ya uongozi na wafanyakazi na baina ya wafanyakazi na wafanyakazi waliopo idara moja au idara tofauti. Mahusiano yanapokuwa dhaifu ndani ya biashara huwa ndiyo chanzo cha changamoto na matatizo mbalimbali baina ya watu wanaofanya kazi kwenye biashara hiyo.

Kwenye biashara ndogo, ambayo ina wafanyakazi chini ya mia moja, mmiliki wa biashara anakuwa anamjua kila mfanyakazi kwa jina lake na sifa zake. Wafanyakazi wanakuwa wanajuana kwa majina na sifa zao. Hii inaleta ushirikiano mkubwa sana, watu wanashirikiana kama timu moja, kwa sababu wanajuana vizuri.

Biashara inapofikia ukubwa ambapo mmiliki wa biashara anakutana na mtu kwenye eneo la biashara na hajui kama ni mfanyakazi au mteja, matatizo mengi huwa yanazalishwa kutokana na wingi huo wa watu. Kwanza ni rahisi kuwa na watu ambao hawana ufanisi na uzalishaji mzuri na kuweza kujificha nyuma ya kivuli cha wengine.

Pia biashara inapokuwa ndogo na wafanyakazi kujuana, inaleta ile hali ya kujali zaidi, wafanyakazi wanajisikia kuwa ndani ya familia moja na siyo tu kuchukulia biashara kama sehemu ya kwenda kuingiza kipato. Hili linakuwa na manufaa kwa biashara kwa sababu wafanyakazi wanajituma zaidi.

Nne; mahusiano mazuri na jamii inayokuzunguka.

Mahusiano mazuri baina ya jamii na biashara ni nguzo muhimu sana kwenye uimara wa biashara yoyote ile. Biashara nyingi kubwa huwa zinayajenga mahusiano haya kupitia utoaji wa misaada na huduma mbalimbali za kijamii. Japokuwa hatua hii ni nzuri, lakini huwa haiweki wajibu baina ya pande hizo mbili.

Biashara ambazo ni ndogo na zinajihusisha na jamii ambayo zipo, huwa zinajenga mahusiano mazuri sana na jamii hizo, kiasi cha jamii kujiona ni sehemu ya biashara hizo. Jamii inazilinda na kuzitegemea biashara hizo kutokana na manufaa makubwa ambayo biashara hizo zinakuwa zimeleta kwenye jamii hizo.

Pamoja na kutoa ajira kwa wanajamii, kutoa bidhaa na huduma ambazo ni muhimu, lakini pia biashara ndogo zimekuwa zinajihusisha moja kwa moja kwenye shughuli za kijamii kama michezo, utoaji wa huduma mbalimbali, misaada kwa wenye uhitaji na mengine kama hayo. Hii inafanya biashara hizo kuwa sehemu ya jamii husika na kuthaminiwa zaidi ukilinganisha na biashara kubwa ambazo zinaonekana ni za nje ya jamii husika.

Tano; mahusiano mazuri na wateja na wasambazaji wa biashara.

Kadiri biashara inavyozidi kukua, ndivyo uongozi wa biashara unavyokuwa mbali na wateja wa biashara hiyo. Na kadiri uongozi unavyokuwa mbali na wateja, ndivyo sera mbalimbali za biashara hiyo zinavyoshindwa kuwanufaisha wateja.

Biashara inapokuwa ndogo, mmiliki wa biashara anakutana na wateja wa biashara hiyo kila siku na hivyo kusikia moja kwa moja kutoka kwao, kupata maoni yao, kujua changamoto zao na hata kuona fursa zaidi za kuwahudumia wateja hao. Biashara inapokua, uongozi unakuwa mbali na wateja na fursa zote hizo zinakosekana.

Hili limekuwa linaonekana wazi kwa biashara ambazo huwa zinaanza zikiwa ndogo na zinapendwa sana na wateja, kwa sababu wanajaliwa. Lakini biashara hizo zinapokuwa wateja wanakosa ile hali ya kujaliwa na hivyo kuacha kupata huduma kwenye biashara hizo.

Unapokuwa na biashara ndogo, ambapo wewe mmiliki bado unapata nafasi ya kukutana na wateja moja kwa moja, mahusiano na wateja yanakuwa bora na wanaitegemea zaidi biashara.

Kadhalika kwa wasambazaji wanaoiuzia biashara bidhaa na huduma mbalimbali, biashara inapokuwa ndogo mahusiano yanakuwa bora na yenye manufaa kwa pande zote mbili.

SOMA; Huyu Ndiye Mteja Bora Sana Wa Biashara Yako Ambayo Hupaswi Kumpoteza.

Sita; uhuru wa kuwa na uongozi unaotaka.

Biashara kubwa, zina uongozi wa aina moja, uongozo wa madaraja na unaotoa maelekezo kutoka juu kwenda chini. Kuna ngazi mbalimbali za uongozi na mawasiliano yanapaswa kupita kila ngazi. Mfano mfanyakazi wa mwisho hawezi kupeleka malalamiko au mapendekezo yake moja kwa moja kwa mkurugenzi mkuu, bali atapaswa kuyapitisha kwa meneja wake, meneja naye apitishe kwa aliye juu yake na huyo ndiyo apelekea kwa mkurugenzi. Mlolongo huu unafanya taarifa kuchelewa kufika sehemu husika lakini pia inafanya ukweli kubadilishwa kwa kila ngazi ambapo taarifa inapita.

Unapoendesha biashara ndogo, unachagua ni aina gani ya uongozi unaotaka kuwa nao kwenye biashara yako. Hulazimiki kufuata uongozi fulani kama makampuni makubwa ambayo yana wawekezaji na hivyo kuwa matakwa ya kisheria kuwa na uongozi wa aina fulani.

Wewe unachagua aina ya uongozi utakaoendana na biashara yako, utakaoruhusu taarifa kusambaa mapema na ukweli kutokubadilishwa. Biashara nyingi ndogo zimekuwa na uongozi wa mlango wazi, kwamba mkurugenzi au mmiliki wa biashara anamkaribisha mtu yeyote kwenye biashara bila ya kujali cheo au wadhifa wake kuleta mapendekezo, malalamiko na maoni yoyote na yeye anayapokea na kuyafanyia kazi. Kwa njia hii kunakuwa na uwazi mkubwa kwenye biashara.

Saba; uwezo wa kubadilika haraka na kutumia fursa vizuri.

Kadiri biashara inavyokuwa kubwa, ndivyo mabadiliko yanavyokuwa magumu. Inaweza kujitokeza fursa nzuri kwa biashara kuifanyia kazi, lakini mlolongo wa kupitisha mabadiliko yanayohitajika unakuwa mrefu, wakati mwingine kusubiri mpaka bodi ikae ndiyo iweze kupitisha maamuzi hayo. Mpaka hayo yafanyike, fursa hiyo inakuwa umeshapita na hivyo biashara haiwezi kunufaika tena.

Ukiwa na biashara ndogo, maamuzi yanafanywa na watu wachache, hivyo inapojitokeza fursa yenye manufaa, mnaweza kufikia maamuzi haraka na kunufaika na fursa hiyo.

Hizo ndizo faida saba za kuchagua kubaki na biashara ndogo na kutokusumbuka kuikuza. Ukweli ni kwamba, biashara ndogo ikiendeshwa vizuri, inakuwa na manufaa makubwa kuliko biashara kubwa. Hii ni kwa sababu ya ule ukaribu ambao biashara inakuwa nao kwa wateja na jamii na kutokuwa na presha ya nje ambayo inalazimisha biashara kutengeneza faida kwa hamna yoyote ile.

Kama umechagua kufanya biashara ambayo unaipenda, na ungependa kuendelea kuifanya kwa kipindi chote ambacho utakuwa hai na hata kuweza kuirithisha kwa wengine, basi chagua kuifanya kama biashara ndogo lakini yenye mafanikio makubwa. Biashara yako ndogo itakapoonesha mafanikio makubwa, watajitokeza watu na kukuambia unakopesheka, au wapo tayari kuwekeza au kuinunua biashara hiyo. Hapa ndipo majaribu makubwa yanapokuingia, ukikubaliana nao unakuwa umechagua kuipoteza biashara yako. Ukikataa na kuendelea na biashara yako wengi hawatakuelewa, lakini utabaki na biashara yenye mafanikio makuba.

Wewe kama mwanzilishi na mmiliki wa biashara ndiye unayepaswa kufanya maamuzi ya mwisho juu ya biashara yako. Fanya maamuzi ambayo yatakuwa bora kwako na kwa biashara yako pia.

Kwenye makala ya jula la 39 tutakwenda kujifunza kwa undani jinsi unavyoweza kuendesha biashara ndogo kwa mafanikio makubwa na kuachana na usumbufu wa ukuaji. Utajifunza jinsi ya kuboresha mahusiano, kutoa huduma bora, kuongeza ufanisi kwenye biashara na kuizuia biashara hiyo isife.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

WhatsApp Image 2019-07-13 at 18.40.50