Mpendwa rafiki yangu,

Asili yetu sisi binadamu ni kupenda vitu bora hata kama sisi wenyewe tunajijua hatuna ubora hatupendi pia vitu visivyokuwa na ubora.

Kila mzazi anatamani mtoto wake awe vizuri na wazazi wengi wanatamani na wanaamini kuwa urithi mzuri wa mtoto ni elimu. Hivyo kila mzazi anatamani mtoto wake apate shule bora ili aweze kupata elimu bora.

Wazazi huwa wanapeleka watoto shule kadiri ya kiwango cha ada au ubora wa shule wanayoitaka. Nimekuja kuona ni namna gani wazazi wanapata shida pale wanapotaka kuwapeleka watoto wao shule. Wengine hawana uelewa juu ya shule ni shule gani bora ambayo anaweza akampeleka mtoto wake.

Kama mzazi unataka mtoto wako kusoma shule bora basi hakikisha kwanza unamjengea msingi bora wa elimu tokea akiwa mdogo. Tumia gharama ya kumlea na kumwandaa mtoto tokea akiwa shule za msingi una hakikisha anakuwa bora kweli kweli.

Wazazi wengi wanajidanganya sana wanaacha kuwajengea watoto msingi bora huku wakiamini kwamba wakiwa na fedha kila kitu kitawezekana. Ni kweli fedha ni muhimu lakini siyo kila mahali fedha inaweza kuingia.

Kwa mfano, unataka kumpeleka mtoto shule ambayo inafanya vizuri sana kitaifa na ili uweze kupata shule hiyo ni lazima ukidhi vigezo na masharti sasa kwenye vigezo na masharti hapa ndiyo panakuwa pagumu kwa wazazi wengi. Unakuta mzazi fedha anayo kabisa ya kulipa ada, yaani kwake ada siyo tatizo lakini unakuja kukuta mtoto hana uwezo wa kusoma yule anayotaka kwa sababu ya kukosa sifa au ubora wa kusoma hiyo shule.

SOMA; Vitu Viwili Ambavyo Mtoto Anapaswa Kuvijua Kutoka Kwa Mzazi

Labda mzazi anataka mtoto wake asome shule x, sasa unakuta mtoto hana uwezo wa kusoma shule x kwa sababu shule x wameweka vigezo vyao, ili usome shule x sharti uwe na wastani wa alama A.  Kama huna wastani huo hawana haja na wewe hata siku moja.

Hapo ndiyo ule usemi unakuja siyo kila mahali fedha inaweza kuingia, utakua na fedha kweli lakini mtoto akawa hana sifa za kusoma shule bora unayotaka.

Hivyo basi, wazazi mkusanye fedha lakini msisahau kuwasimamia watoto wenu vizuri kwa kuwapa misingi bora ya elimu tokea wakiwa wadogo. Kama tunataka kuwa na watoito bora basi tukubali kulipa gharama.

Watoto wanashindwa kufanya vizuri shuleni kwa sababu ya kukosa mwongozo sahihi kutoka kwa wazazi au walezi wao. Tuwe na muda wa kuwasikiliza watoto wanataka nini na kisha kuwasaidia. Usiwe mzazi wa kulipa ada tu na mambo mengine unawaachia walimu, wajibika na wewe kujua maendeleo yake kila siku.

Hatua ya kuchukua leo; mzazi soma na mwanao,hakikisha kila siku unajua maendeleo ya mtoto wako na ni somo au changamoto gani anapitia halafu msaidie kutatua hiyo changamoto kwa kufanya hivyo itamsaidia sana kujua ubora na udhaifu wake uko kwenye nini na ukijua hilo ni rahisi kufanyia kazi.

Mwisho, ili tuwe na jamii bora lazima kwanza tuwe na familia bora. Familia bora ndiyo itaweza kuzaa watoto  bora na tukishakuwa na familia bora tunakuwa tumepata jamii bora.  Lipia gharama unazopaswa kulipa sasa kwa mtoto wako na ukidharau utakuja kulipa kwa riba kitu ambacho unaweza kukizuia kwa sasa.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana