Rafiki yangu mpendwa,
Mimi kama kocha wako, kuna vitu vitatu ninavyohitaji kutoka kwako ili tuweze kwenda pamoja, ili ushirikiano wetu uweze kuwa na manufaa makubwa kwa kila mmoja wetu.
Vitu hivi vitatu ndivyo vigezo ambavyo nimekuwa navitumia katika kuchagua watu wanaoweza kunufaika na huduma mbalimbali za ukocha ninazotoa.
Kitu cha kwanza ni KUONEKANA (SHOW UP).
Ninahitaji wewe uonekane, uje kwangu ukiwa tayari unataka kupiga hatua kwenye maisha yako. Unapaswa kuwa na utayari ndani yako, msukumo wa kutaka kupiga hatua zaidi ya pale ulipo sasa.
Kama tayari umeridhika na hapo ulipo sasa sina msaada wa kukupa.
Kama inabidi mimi nikubembeleze kwamba unahitaji kutoka hapo ulipo sasa haitafanya kazi.
Lazima kiu ya kupiga hatua ianzie ndani yako, na kama wanavyosema, mwanafunzi anapokuwa tayari, mwalimu huonekana. Mwalimu tayari nipo, ni wewe kuwa tayari na tufanye kazi pamoja.
Kitu cha pili ni KUFANYA KAZI (WORK HARD).
Lazima uwe tayari kufanya kazi kwa akili, nguvu na juhudi kubwa ndiyo tunaweza kwenda pamoja. Lazima uamini kwenye kazi, lazima upende kazi, lazima uwe tayari kujituma na kwenda hatua ya ziada kwenye kila unachofanya.
Kama unaamini unapaswa kufanya kazi kwa akili pekee na siyo nguvu, hatuwezi kwenda pamoja.
Kama unaamini ipo njia ya mkato ya kufanikiwa bila ya kufanya kazi, umeshanipoteza.
Kama unafikiri ukishafanikiwa basi huhitaji tena kufanya kazi, kwa sababu unaweza kuwaajiri wengine wafanye kila kitu, hatutaweza kwenda pamoja kwa muda mrefu.
Unapaswa kuweka kazi, kazi ndiyo rafiki wa kweli, kazi haijawahi kumtupa yeyote, penda kazi.
Kitu cha tatu ni KUSIKILIZA (LISTEN).
Inabidi uwe msikivu ili tuweze kwenda pamoja. Katika dunia ya sasa ambayo ina kila aina ya kelele na usumbufu, usikivu ndiyo utakaokusaidia wewe na kukutofautisha na wengine.
Na ili uwe msikivu lazima uweze kulinda umakini wako na kuondokana na kelele na usumbufu unaokuzunguka.
Tunaposhauriana kitu na tukafikia makubaliano, inabidi uyafanyie kazi makubaliano hayo. Na siyo kuanza kuyachambua tena na kubadili ukiwa njiani.
Kama unataka ushauri halafu tunashauriana vizuri na kukubaliana ufanye nini, halafu baadaye unabadili mawazo yako, bila ya kushauriana upya hatuwezi kwenda pamoja.
Kwa kifupi sitakuwa na matumizi kwako kama hatutasikilizana, kama unajiona tayari unajua kila kitu na huhitaji kufundishwa au kushauriwa zaidi, uko mbali sana na mimi.
Rafiki, ni vitu hivyo vitatu tu, ONEKANA, WEKA KAZI, SIKILIZA. Havihitaji uwe na kipaji kikubwa, havihitaji uwe na elimu kubwa, havihitaji uwe tajiri au umetokea mazingira mazuri.
Ukiwa na vitu hivyo vitatu, na tukafanya kazi pamoja kupitia huduma za ukocha ninazotoa, utaweza kufanikiwa sana kwenye kitu chochote unachofanya kwenye maisha yako.
Jijengee tabia hizo tatu na karibu tuendelee kuwa pamoja kwenye safari hii ya mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha nitaendelea kuyafanyia kazi ili tuweze kwenda na kuwa wote.
LikeLike
Karibu sana Beatus
LikeLike
Ahsante Dr Amani kwa kaz zako.
LikeLike
Karibu Lema.
LikeLike
Asante kocha kwa vitu hivyo vitatu , nimejifunza kazi kwangu kufanyia kazi ili tuendelee kuwa pamoja , nahaidi kutokuwa mbali na wewe , maarifa yako yamenitoa mbali sana , asante ,asante sana
LikeLike
Karibu sana James.
LikeLike
Hakika Coach!inanibidi nijiongeze palipopungua katika KUONEKANA,KUWEKA KAZI na KUSIKILIZA.
LikeLike
Vizuri sana Yusuph
LikeLike