Thomas Edison alijaribu zaidi ya mara elfu kumi kabla ya kuweza kutengeneza balbu ya umeme.
 
Colonel Sanders wa KFC aliuza wazo lake la upikaji tofauti wa kuku kwa watu zaidi ya elfu moja kabla ya kupata mmoja wa kukubali kufanyia kazi wazo lake na hapo ndipo mgahawa maarufu wa KFC uliopo duniani kote ulipoanzia.
 
Sasa wewe rafiki yangu, ambaye umeanzisha biashara mbili au tatu zikashindwa, au umeshindwa kazi maeneo matatu au manne unathubutu kabisa kusema kwamba umejaribu kila kitu lakini imeshindikana?
 
Huu ndiyo uongo ambao umekuwa unajiambia na unakukwamisha wewe usifanikiwe. Kujiambia kwamba umeshajaribu kila njia lakini imeshindikana na kujidanganya. Kwa sababu nina uhakika hujajaribu kitu chochote kile zaidi ya mara elfu moja. Kwa sababu ungekuwa umefikia idadi hiyo ya majaribio, ungeshakutana na wazo zuri la kukutoa hapo ulipokwama sasa.
 
Ujumbe wangu kwako leo rafiki yangu ni usikate tamaa pale unaposhindwa, bali endelea kujaribu tena, endelea kuweka juhudi. Kila hatua unayoshindwa jua ni darasa umepata la kukuwezesha kuwa bora zaidi.
 
Kila ambapo wazo la kwamba umejaribu ukashindwa au haiwezekani kwako linapokujia, liweke pembeni na rudi kwenye kuweka kazi.
 
Ushahidi ni mkubwa kwamba hakuna mtu aliyeng’ang’ana na kile alichotaka akakikosa. Hivyo kama wewe unataka kuishia njiani, ni tafsiri kwamba siyo ulichotaka kweli, na kama mpaka sasa hujajua unachotaka kweli, utapoteza muda na nguvu zako kujaribu vitu vipya kila siku.
 
Anza na kile unachotaka kweli, kile ambacho uko tayari kukipigania kufa na kupona, na kisha ng’ang’ana nacho mpaka utakapokipata. Na kamwe usijiambie umeshajaribu kila kitu lakini haiwezekani. Bado hujajaribu kila kitu, jifunze kwa kila unaposhindwa na jaribu tena kwa ubora zaidi.
 
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
 
Rafiki na Kocha wako,
 
Dr. Makirita Amani,